22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Hali ya hewa yamtisha mkuu wa wilaya

sebastian-waryubaNa FLORENCE SANAWA, TANDAHIMBA

MKUU wa Wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, ameshtushwa na taarifa ya hali ya hewa inayoonyesha kutakuwa na mvua chache mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, amewaagiza madiwani wilayani hapa kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima mazao ya muda mfupi kwa ajili ya kukabiliana na njaa.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa maagizo hayo juzi wakati wa kikao cha baraza la madiwani.

Kwa mujibu wa Waryuba, kitendo cha wakulima wilayani hapa kutegemea korosho kama zao la biashara, kinaweza kusababisha uhaba wa chakula utakaoathiri wananchi wengi.

“Madiwani hakikisheni mnatoa elimu itakayowasaidia wananchi kupanda na kukuza mazao mengine yasiyokuwa ya biashara kama mihogo, mahindi na mtama.

“Nasema hivyo kwa sababu taarifa iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa, inasema mvua zitakuwa chache ndiyo maana nasema taarifa hiyo inapaswa kufanyiwa kazi ili kuondoa tatizo la njaa linaloweza kuikumba halmashauri yetu kama hatua hazitachukuliwa haraka.

“Ufikie wakati wakulima wasione aibu kupanda mihogo kwa sababu tumeshuhudia mashamba mengi ya korosho yakiwa na nafasi kubwa kati ya mkorosho na mkorosho.

“Tutumie nafasi hizo kwa kupanda mazao tofauti sehemu ambazo kivuli hakitaweza kuathiri mazao hayo,” alisema Waryuba.

Naye Diwani wa Kata ya Mchichira, Ashunga Ngope, alisema wakulima wengi wilayani humo wamekuwa na kawaida ya kulima korosho peke yake na kusahau kilimo cha mazao mchanganyiko.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakulima hao waanze kulima na mazao mengine ili waweze kukabiliana na njaa inayoweza kutokea wakati wowote.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Said Msomoka, alisema agizo hilo la mkuu wa wilaya lazima lifanyiwe kazi kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu hiyo ili kuongeza uelewa katika kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles