25.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

JPM na dhana shirikishi ya kuimarisha uchumi wa Watanzania

Na MWANDISHI MAALUM-DAR ES SALAAM

BAADA ya awamu ya tano kuingia madarakani ilikutana na mwelekeo wa  muunguko mkubwa wa thamaniya fedha ya Tanzania. 

Mtakumbuka kuna baadhi ya masoko ya fedha yalifikia mahali  kuanza kuuza dola moja ya kimarekeni kwa takribani shs 2,500. 

Historia inaonyesha kuanzia dola ya kimarekani ilipokuwa inauzwa kwa shilingi 800 miaka ya 1992 kila ilipopanda haikuwahi kushuka tena.

Thamani ya dola ni muhimu sana kuitazama kwa kuwa hadi sasa ndio fedha kuu ya kimataifa. 

Kila tunachonunua nje ya nchi kinawekwa kwenye dola. 

Hivyo kama ulikuwa unaweza kununua matairi ya gari kwa dola 50 kipindi ambacho dola moja ni sh 800 ina maana kwa fedha za Tanzania itakuwa ni sawa natsh 40,000 kwa tairi moja. 

Na inapokuwa thamani ya Shilingi ni 2,500 kwa dola moja tairi hilohilo litanunuliwa kwa shilingi 125,000.

Kwa mantiki hiyo hiyo kushuka kwa thamani ya shilingi ina athari kubwa sio kwa wafanyakazi tu bali kuanzia kwa wafanya biashara hadi wakulima. 

Madawa na mbolea vyote vinapanda bei, vifaa vya ujenzi na madawa halikadhalika na hivyo kuwaathiri wakulima na wafanyakazi.

Kuna sababu nyingi za mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ta fedha zetu, lakini moja kubwa ni kubadili mifumo ya mishahara na kupandisha mishahara holela. 

Kimsingi kupandisha mishahara holela ni njia ya taifa lililokata tamaa kutafuta njia nyepesi za kuimarisha maisha ya wananchi wake kwa muda mfupi.

Kuimarisha maisha kwa muda mfupi kwa kuwa ukipandisha mishahara kila idara ya kimaisha inaongeza bei na matokeo yake pamoja na kuwa na fedha nyingi ila unaishia kununua kitu cha thamani yake ile ile. 

Matokeo ya kuchapisha fedha ili kukidhi mabadiliko ya muundo ndio inasababisha mfumuko wa bei kuwa kubwa.

Mfano mzuri wa mfumuko wa bei ni nchi ya Zimbabwe kuchapishwa kwa fedha kwa noti ya 100 trillion(100,000,000,000,000) ambapo bado haina uwezo hata wa kununu gari aina ya corolla.

 Uendeshaji huu wa kiuchumi wa kubadili miundo ya fedha ndio huongeza mfumuko wa bei kwenye mzunguko wa fedha bila kwenda sambasamba na uzalishaji.

Kwa nchi zilizoendelea na zenye nia thabiti ya kuendelea kubadili miundo ya mishahara kila Mei Mosi zilikwisha acha zamani sana.

Kinachofanyika ni juhudi za ujenzi wa uchumi wa uzalishaji na kuimarisha thamani ya fedha zao. 

Badala ya kuwapandisha mishahara unaipandisha thamani fedha waliyonayo. 

Mfano mzuri ni nchi ya Kenya, mara ya mwisho Bodi ya Mishahara imepandisha mishahara mwaka jana kwa ajili ya miaka mitano ijayo.

Kwenye uchumi wa kupandisha muundo wa mshahara kila mwezi ndio ulipelekea nchini Zambia kuondoa sifuri moja ya fedha zao za Kwacha. 

Fedha inakuwa nyingi kuliko uwezo wa uzalishaji wa nchi. Kwa wale wenzangu waliokuwa wakisafiri na wazazi wao wanakumbuka kuwa kwacha 100 ya Zambia ilikuwa sawa na shs 200 ya Tanzania miaka ya 1980 hadi 1990.

Leo hii Sh 100 ya Tanzania ni sawa na kwacha 400 za Zambia na hapa ni baada ya Zambia kuondoa sifuri moja kwenye fedha yao. 

Kuondoa sifuri moja maana yake ni kuchapisha fedha mpya kwa kuwa fedha imeshafika hatua haina thamani tena, sasa kwenye fedha mpya wanabadilisha na za zamani. 

Kama una noti ya 100,000 ya zamani, unapewa 10,000 mpya. 

Kama 10,000 ya zamani basi unapewa1,000 mpya na kuendelea.

Ukijikita kwenye dhana hii ya kupandisha mishahara bila kuangalia kukuwa kwa uzalishaji na uchumi ndio unaingia kwenye historia ya uharibifu wa uchumi wa nchi. 

Uganda walichapisha fedha kupata sifa ya kuwapa wafanyakazi mshahara mkubwa matokea yake uchumi wote ukaharibika. Wafanyakazi wachache wanaumiza maisha ya wakulima na wafanyabiashara wa nchi nzima.

Kurekebisha kwa kufuata hatua inachukua zaidi ya miongo mitatu na bado haujarudi mahali ulipokuwepo.

Lakini pia kubadili miundo ya fedha hakujawahi kutoa nafuu ya uchumi kwa mfanyakazi hata siku moja, ila kuimarisha thamani ya fedha inawezakubadili. 

Mathalani, umeweka benki fedha yako Sh 7,000,000 leo kununua sementi mifuko 500 kwa ajili ya ujenzi mwakani. 

Thamani ya fedha inaposhuka kwa kupandisha mishahara unajikuta unaishia kununua mifuko 300 kwa akiba yako ya miaka 3. 

Lakini ingebakia vilevile mipango yako ingebakia sawa, na thamani ikiongezeka basi unakuta fedha ileile unanunua mifuko 550.

Hii inamaanisha kubadilika kwa miundo ya fedha ina muumiza mfanyakazi na pia inauwa tabia ya kutunza fedha kwa mfanyakazi bila kujielewa.

Matokeo yake riba kubwa za wakopeshaji fedha kwa kuogopa thamani kushuka kila siku lakini ina haribu uchumi wa nchi nyingi sana kwa ajili ya kujifurahisha.

Viongozi makini duniani ni wale wanaongoza nchi bila kujali kuwa uamuzi wao unaweza kuleta manung’uniko. 

Kuongoza ni sawa na kumuamsha mtoto asubuhi wakati wa baridi kwenda shule, analia lakini kama mzazi lazima aamke na kwenda shule kwa faida yake. 

Uongozi ni sawa na kumchoma sindano mtoto ya homa ya mapafu apone. Faida yake ni kuwa na familia iliyo bora na yenye afya.

JPM kasimama kama kiongozi, kajua kuwa ili nchi ivuke ni lazima tupitie hatua za kufunga mikanda. 

Na mikanda haiwezi kufungwa na abiria mmoja ndani ya ndege bali wote. 

Kwa kufunga mikanda ndio nchi yetu inasonga mbele na kuona maendeleo. Maendeleleo hayawezi kuja kwa kula bata na kujenga uchumi.

Zamani wakati ninakuwa nakumbuka ilikuwa ni dhana kabisa watu wakiona viatu vimeisha shule na hupewi na wazazi wako vingine unaulizwa baba yako anajenga? Kwa kuwa suala la kujenga kila mwaka familia ilikuwa inahusika kwenye kupambana kwenye nafasi yake. 

Wewe ni nani hadi wenzako wajenge ilihali wewe unaendela kunywa bia zile zile bar.

Tunaposema tunajenga nchi yetu tuna maana gani? Tuna maana kuwa tunapeleka elimu kwa wananchi wetu, tunapeleka miundo mbinu ya afya na barabara, tunapeleka wataalamu wa afya na njia umeme kuwafikia watu wengi zaidi, tunapeleka uwezo wa kujenga viwanda na kukuza ajira kupitia mapinduzi ya viwanda.

Nchi hii haiwezi kujengwa na mabeberu tangu tunapata uhuru hadi mwaka 2015 takribani miaka 54 tuliweza kujenga vituo vya afya 105 lakini ndani ya miaka 5 ya JPM tumeweza kujenga vituo vya afya 255. 

Tuna uhakika walau sasa ndugu zetu walioko wilayani na vijijini wamesogezewa huduma. Mzigo wakuwasafirisha ndugu zetu vijijini kupata matibabu umepungua.

Umeme ilikuwa ni anasa ya mjini. Vijiji 2,300 tu vilikuwa na umeme tangu tunapata uhuru hadi mwaka 2015. Lakini ndani ya miaka 5 ya JPM vijiji zaidi ya 8,249 vimefikiwa na umeme. 

Vijana wanaweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo na hata kazi za kujipatia kipato zianazohitaji matumizi ya umeme.

Bado tunaendelea kujiuliza nani anagharamia mambo haya makubwa kwa wakati mmoja.

Dhana ya utashi kwa kiongozi kujenga vituo hivi vya afya na kuweza kuhakikisha kazi hizi zinafanyika sio jambo rahisi. 

JPM kama kiongozi asingeshindwa kupata huduma bora za afya bila hata kujenga zahanati moja.

Angeweza kuwajaza mapesa na kuacha uchumi ukiharibika na watu wachache wakineemeka huku wananchi wakigeuka watwana na kushangilia wakifa kwa shida zao.Lakini aliamua kujitoa sadaka kwa ajili ya nchi hii.

Upande wa wafanyakazi, ni kweli kuna kipindi nyongeza(increments) haikutoka, lakini je hatuoni kuwa ni wajibu wetu kufunga mikanda ili kuendeleza nchi yetu. Hatujaona vituo vya afya vilivyojengwa nchi nzima kusaidia ndugu zetu? hatujaona umeme uliosambazwa vijiji vyetu vyote? Ni kweli hatuoni fahari kuwa tumejifunga mkanda kwa ajili ya nchi yetu?.

Nchi itajengwa na wananchi wenyewe, tunafunga mikanda kama wazazi wale waliokuwa wakishindwa hata kununua viatu kwa ajili ya kujenga nyumba za familia zao, hakuna mtu wa kuijenga Tanzania zaidi ya sisi wenyewe.

Increments zetu zimechangia kwenye maono ya Tanzania mpya, pamoja na Rais Magufuli tutajikuta tuko ndani ya nchi yenye uchumi bora Afrika Mashariki.

Wafanyakazi watembee kifua mbele kuwa wametoa mchango wao na kumkabidhi kiongozi mwenye maono,  aliyedhibiti matumizi na wezi na kuhakikisha nchi inasonga mbele. 

Sasa yule anayeamini kuwa ni makosa kutumia increments zake kujenga nchi anakosa sifa ya kuwa mzalendo. 

Mzalendo ni mtu ambaye yuko tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya taifa lake. 

Unashindwajekutoa nyongeza ndogo ya mshahara wako kwa ajili ya umeme wa ndugu zetu na huduma za afya na elimu.

Tunapokuwa tunangoja misaada ya wazungu lazima ujue kuwa zile pia ni kodi za wananchi wao. 

Na wanatupatia kwa kuachia baadhi ya mambo muhimu.

Tunatakiwa kujua kuwa hata kwao wahisani kuna masikini wanalala nje, kuna walemavu wanaomba misaada lakini wanaleta misaada kwenye nchi masikini, hivyobasi ni aibu kwa sisi wenyewe kutojisikia fahari kuungana na kiongozi aliyeweza kubadili nchi ya Tanzania.

Natoa rai kwa watu wote, viongozi wenye uchungu na Nchi zao kama JPM hawapatikani kirahisi, huwa hawazaliwi hovyo hovyo. Na kama anakutanana wananchi wenye utashi basi kwa pamoja nchi inaweza kujengwa. 

Ni bahati mbayasana kuwa demokrasia zilizoletwa kwetu zinamlazimisha hata kiongozi bora kupita na kuanza kuomba kura kwa ajili ya watu aliojitoa sadaka kwenye maisha yao.

Mwalimu wangu wa taaluma alipata kuniambia kuwa kwa namna anavyosimamia nidhamu na watoto kusoma mkipiga kura leo nani ni mwalimu bora nitaishia kupata kura 10 dhidi ya kura 300 za mwalimu wa starehe na michezo.

Lakini baada ya nyie kuwa kazini na kutambua thamani yangu mngepata nafasi yakupiga kura tena ni wazi mngenipa kura zote. Tunapaswa kuitambua thamani ya kiongozi wetu sasa na kuipa heshima yake. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles