23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ASHTUKIA MCHEZO GAWIO LA SERIKALI

 Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, ameshangazwa na gawio linalotolewa na Benki ya NMB kwa Serikali kufanana kwa miaka mitatu mfululizo na kusema kuwa huenda kuna mchezo mchafu unachezwa.

Aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa jengo la Mfuko wa Pensheni wa PSPF na tawi jipya la Benki ya NMB lililopo Barabara ya Chimwaga mjini Dodoma.

Alifafanua kuwa mwaka 2012/13 benki hiyo ilitoa gawio la Sh bilioni 10.8, 2013/14 (Sh bilioni 14.3), 2014/15 (Sh bilioni 16.5), 2015/16 (bilioni 16.5) na 2016/17 (Sh bilioni 16.5),

“Hapa ndipo nina maswali, haiwezekani kama benki inafanya faida gawio liwe hivyo kwa miaka mitatu kwa sisi wenye hisa za asilimia 32.

“Hili mkurugenzi na mwenyekiti mlifanyie kazi limeniumiza, kuna mchezo mchafu wa aina fulani ambao haujatekelezwa vizuri, najua meseji ‘sent and delivered’.

“Watu mnaotuwakilisha mkafanye hesabu vizuri, hata kwa vilaza wa darasa la saba wanaweza wakapiga hesabu vizuri.

“Tunahitaji faida zitakazoweza kwenda kutoa huduma zingine kwa wananchi, na hili ndio lilikuwa lengo kubwa la kubinafsisha hii benki.

“Ubinafsishaji umekuwa na faida lakini tusiridhike na faida zinazotolewa, lazima tufike mahali tujiulize zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka watu watakaoteuliwa kufanya kazi kwenye tawi hilo kuzingatia maadili kama alivyokuwa baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Watakaoteuliwa kufanya kazi kwenye tawi hili wazingatie maadili ya mwenye jina (Kambarage), huo ndio wito wangu.

“Itasikitisha sana kama wateja watacheleweshwa kuhudumiwa au kuwapo kwa dalili za rushwa wakati baba wa Taifa alivichukia vitu hivi.

“Kwa vile mmekubali kuchagua jina la Kambarage basi pawe na ‘reflection’ ya utendaji kazi unaoendana na baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,” alisema.

MIFUKO

Rais Magufuli alisema mifuko ina ukwasi wa thamani ya Sh trilioni 12.23 na kwamba hicho ni kiasi kidogo kwa kuzingatia ukubwa wa nchi.

“Tuna zaidi ya benki 50 na mifuko ya jamii saba lakini takribani Watanzania milioni 4.7 ndio wana akaunti za benki na wanachama wa mifuko ni milioni 2.2, idadi hiyo ni ndogo sana.

“Hivyo taasisi za fedha ziongeze idadi ya wanachama ili kuongeza mitaji,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia mifuko ya jamii kuna tatizo la ucheleweshaji wa malipo na hata viwango vya mafao bado viko chini ndio maana Serikali imeamua kuiunganisha ili kuwa na mifuko miwili.

AOGOPA KUFUTA VIWANJA

Rais Magufuli alisema hawezi kutumia madaraka yake kufuta viwanja ambavyo viliombwa kwa mujibu wa sheria na akawataka PSPF kujadiliana na majirani zao ili wawanunue.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya PSPF, Mussa Iyombe, kumwomba Rais Magufuli afute hati za viwanja vilivyoko mbele ya jengo hilo ili eneo hilo litumike kuegesha magari kwa wapangaji wake.

“Kuhusu viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya ubalozi na wizara, zungumzeni na majirani zenu muwanunue ili mjenge majengo mnayoyataka.

“Kutumia madaraka yangu kufuta viwanja ambavyo havina makosa na wao waliomba kwa mujibu wa sheria siwezi nikaingilia,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu kodi katika zao la zabibu, alishauri suala hilo likajadiliwe bungeni na kutolewa maamuzi.

“Haiwezi kuingia akilini wakulima wa korosho kodi inapandishwa kwa mazao yao na kuwakatisha tamaa kwa sababu ambazo zinaweza kutatuliwa.

“Muangalie pia katika mazao mengine, mazao ya ngozi, maziwa, ‘crude oil’ ili tuweze kuendeleza kilimo katika nchi yetu,” alisema.

Alisema pia Serikali inasimamia yale iliyoahidi na kwamba si lazima yote yafurahishe.

“Wapo wengine watatumika na mbinu za mabeberu hivyo nataka kukuhakikishia mtoto wa Baba wa Taifa (Makongoro Nyerere) sisi tuko imara na tutafika tukiwa imara,” alisema.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Ashatu Kijaji, alisema benki hiyo imekuza mtaji na kuiwezesha Serikali kupata gawio kubwa kwa sababu inaendeshwa kwa weledi.

Hata hivyo alisema ina kiwango kidogo cha mikopo chechefu ikilinganishwa na benki zingine kubwa nchini na kwamba inatakiwa isizidi asilimia ya mikopo yote lakini NMB ni asilimia 6.4 ya mikopo yote iliyotolewa na benki.

MKURUGENZI NMB

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema waliamua kufungua ofisi na matawi mawili mkoani Dodoma ili kutoa huduma hasa kwa watumishi wa umma.

“Tunaona shughuli nyingi zinaongezeka Dodoma hasa za kilimo na biashara baada ya Serikali kuhamia hapa ndiyo maana nasi tumeamua kuleta huduma zetu,” alisema Bussemaker.

Alisema hadi sasa benki hiyo ina matawi 218 na mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 800 nchi nzima na kwamba ni benki pekee ambayo iko katika wilaya zote nchini.

“Wakala wanahudumia zaidi ya wateja 700,000 kwa mwezi kwa Dodoma wako mawakala 250. Na tunapanga kuongeza idadi ya mawakala na kufikia 10,000 mwaka huu,” alisema.

Alisema kila mwaka benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida ambayo ni zaidi ya Sh bilioni moja kusaidia jamii katika sekta za elimu na afya.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mwaka jana walitoa madawati 6,000 na kompyuta 300 mashuleni na hospitali 60 zilisaidiwa vitanda vya kawaida na vile vya kujifungulia.

“Ni utamaduni wetu kila tunapofungua tawi jipya kutoa msaada kwa jamii na leo (jana) tutatoa hundi ya Sh milioni 50 kwa Mkoa wa Dodoma ambazo zitatumika katika miradi ya elimu na afya,” alisema.

Alisema pia kiwango cha mikopo kwa wakulima wadogo kimefikia Sh bilioni 100 na wanawafikia zaidi ya wakulima wadogo milioni moja.

MKURUGENZI PSPF

Naye Mkurugenzi wa PSPF, alisema mfuko huo ulipewa viwanja vya mradi huo na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Dodoma (CDA), mwaka 2002 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kuendeshea shughuli za mfuko na biashara.

Alisema kazi ya usanifu na ujenzi ilianza Julai 2015 na kukamilika mwaka huu na kwamba walisaini mkataba wa Sh bilioni 37.02 na hadi sasa wametumia Sh bilioni 30.56.

Alisema jengo hilo litatumika kwa shughuli za ofisi na kibiashara na kwamba hadi sasa limeshajaa.

MAKONGORO NYERERE

Mtoto wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere, aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli badala ya kumbeza.

“Wenye tabia ya kubeza wanaofanya vizuri hawaishi na wapo kila nchi duniani, sisi tumuunge mkono rais wetu.

“Wewe utakuwaje kiongozi mzuri halafu unapendwa na kila mtu, au kuna dosari kwa kila mtu au wewe una tatizo, huwezi kupendwa na kila mtu haiwezekani.

“Hawa ni watu na kwa kawaida huwa ni wachache, wanacheza dili na mara zote wanafanikiwa wakigawa watu walio wengi kwa dini, fitina, kabila na uongo.

“Utabezwa, utatishwa, utatukanwa, watapiga uongo, lakini mambo ambayo umeyafanya yanaonekana, aliye na macho haambiwi ona kwa muda mfupi ni mengi sana,” alisema Makongoro.

Alisema wanaomkatisha tamaa Rais Magufuli wako wengi na kwamba mbinu zao zinajulikana kwani hawakuanza sasa.

“Mimi waliwahi kunifuata wakaniuliza, huyu mheshimiwa yukoje nikawauliza kwani vipi. Wakasema tangu ameanza hajakupa kazi, walitaka nichukie lakini mimi ni mchezaji nipo nafasi yangu inaitwa benchi la akiba,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles