31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUPIGA KAMBI  BAA KUPIMA UKIMWI

 

GABRIEL MUSHI Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


KATIKA kukabiliana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) serikali imepanga kupiga kambi kwenye baa na sehemu nyingine za starehe nchini kuwapima wahudhuriaji wa maeneo hayo.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni   Dodoma jana na Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto. Dk. Faustine Ndungulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambale, Masoud Abdalah Salimu (CUF).

Katika swali la msingi, Salimu alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa ziada kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu (TB).

Akijibu swali hilo, Dk. Ndungulile alisema mojawapo ya mikakati ya serikali   kwa sasa ni kuwapima TB watu wanaoshi na Virusi Vya Ukimwi (Waviu).

 

Alisema pamoja na hilo, serikali itaweka kambi katika baa mbalimbali nchini kuwapima wateja wa baa hizo Ukimwi hususan wanaume.

“Pia kufanya upimaji wa TB kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) na kufanya uchunguzi kwa wafanyakazi migodini na kwa mahabusu,” alisema.

Hata hivyo, alisema mtu yeyote anaweza kuambukizwa na kuugua TB lakini makundi yaliyopo hatarini zaidi kuugua ni WAVIU na watoto wadogo chini ya miaka mitano.

Wengine ni wazee, watu wanaougua magonjwa ya muda mrefu ikiwamo saratani, kisukari, wenye utapiamlo, wafungwa, wachimbaji wadogo wadogo migodini na watu wanaotumia dawa za kulevya.

Alisema wizara inatoa wito na kuwahimiza wabunge kushiriki kwa uikamilifu katika mapambano ya kutokomeza TB kwa kuhakikisha TB inakua ajenda yao ya kudumu katika vikao vyote wanavyoviendesha na kuhutubia.

Alisema serikali inaingiza teknolojia mpya nchini ya upimaji na ugunduzi wa uhakika na haraka wa vimelea vya TB.

Alisema hadi sasa zimefungwa  mashine 97  kwa ajili ya kupima ugonjwa wa Kifua Kikuu(TB) katika Hospitali za Mikoa na baadhi ya halmashauri.

“Mashine nyingine 90 zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kufungwa kwenye hospitali za wilaya zilizobakia.

“Pia miongoni mwa mikakati ni kuingiza teknolojia mpya nchini ya upimaji na ugunduzi wa uhakika na haraka wa vimelea vya TB,” alisema.

Alisema mashine hizo zilizofungwa zitawezesha majibu ya vipimo kupatikana baada ya saa mbili badala ya siku tatu kwa vipimo vilivyokuwapo   awali.

“Pia mikakati mingine ni kuyawezesha maduka ya dawa muhimu na waganga wa tiba asili kufanya utambuzi wa dalili za TB na kutoa rufaa kwa wahisiwa wote,”alisema

Hata hivyo sera ya Ukimwi ambayo inaendelea kutumika hadi sasa inatambua upimaji wa hiari wa VVU.

Juni mwaka 2016 Serikali ilisema inakusudia kufanya utafiti kwa kupima virusi vya Ukimwi (VVU) nyumba kwa nyumba kuanzia ngazi ya kaya   kupata takwimu sahihi kuhusu hali ya maambukizi mapya ya ugojwa huo   nchini kwa sasa.

Vyombo vya habari vilimnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa akisema  utafiti huo utakaotumia teknolojia ya kisasa, unalenga kupima viashiria na matokeo ya UKIMWI nchini, kujua ni kiwango gani Tanzania imepiga hatua katika kupamban na ugonjwa huo.

”Utafiti huo utafanyika kwa kutumia sampuli wakilishi ya kaya takriban 15, 800 za Tanzania Bara na Zanzibar kwa kufikia walengwa 40,000 wakiwamo watoto wasiopungua 8, 000,”

 alinukuliwa Mkurugenzi huyo wa NBS.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles