28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Jaji Samatta: Rais Mstaafu anaweza kushitakiwa

*Awaasa wenye siasa za malengo, tamaa Ikulu

NA AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

JAJI Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inaonyesha kuwa Rais Mstaafu anaweza kufunguliwa mashtaka mahakamani na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kutokana na kile kinachoitwa ‘kinga ya urais’ kuwa na mipaka yake.

Jaji Samatta  ambaye amepata kuwa Jaji Mkuu kwa takribani miaka saba kabla hajastaafu mwaka 2007 alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwasilisha mada  ya ‘Uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa katika vyombo vya dola pamoja na utekelezaji wa sheria na utoaji wa haki’ katika kipengele cha wajibu wa Ofisi Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) na Takukuru kwa wanafunzi wa Shule ya Sheria nchini.

Akiwasilisha mada hiyo katika mkutano wa uwajibikaji ulioandaliwa na taasisi isioyo ya serikali ya Wajibu, Jaji Samatta ambaye amekuwa akisifika kwa misimamo na kusimamia haki alirejea Ibara 46(3) ya Katiba akisema kinga aliyopewa Rais katika ibara hiyo haihusu vitendo Rais alivyovifanya akiwa  Rais lakini inahusu vitendo  alivyofanya kama Rais.

 “Ni ukweli kuwa chini ya Katiba ya nchi hii Rais Mstaafu  anaweza kufunguliwa  mashtaka Mahakamani na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).Ni muhimu sana ukweli huu ukaeleweka.

“Ni sahihi kabisa kusema kuwa chini ya Ibara  46(3) ya sheria mama hiyo rais aliyeacha madaraka ana kinga dhidi ya mashtaka, hata hivyo kinga hiyo ina mipaka. Inahusu tu “jambo …..alilofanya……kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka  ya Rais kwa mujibu wa katiba…..”kinga hii haihusu vitendo alivyofanya Rais akiwa Rais,lakini inahusu vitendo alivyofanya kama Rais,”alisema Samatta.

Alisema kuna tofauti kubwa na iliyo wazi kati ya maneno ya ‘akiwa’  na ‘kama’,kwa mujibu wa kifungu hicho cha Katiba aliyekuwa rais hana kinga dhidi ya mashtaka kuhusu jambo lolote ambalo hakufanya kama Rais.

“Kuhusu jambo la aina hiyo Mkurugenzi wa mashtaka ana mamlaka ya kumfungulia  mashtaka na mahakama zina mamlaka ya kusikiliza  na kuamua kesi  hiyo kama ilivyo kwa kesi za jinai zinazoweza kufunguliwa dhidi ya watu wengine nchini.

 “Kwa mfano kama alipokuwa madarakani Rais aliamua siku  moja kuendesha gari yeye mwenyewe  na akamgonga mtu na kusababisha kifo chake kutoakana na  uzembe mkubwa kinga chini ya Ibara 46(3) ya Katiba haitamwokoa kutokana kwenye mashtaka ya kitendo hicho,vitendo vya ufisadi navyo vitakosa kinga hiyo,”.

Katika hilo hilo, Jaji Samatta alikwenda mbali na hata kuwaasa wale aliowaita wenye siasa za malengo au tamaa ya kuwa mpangaji Ikulu akiwataka watambue fika  kwa faida ya nchi,ukweli huo.

Alisema  watawala pia wanapaswa kuzingatia kuwa safari yao ya kuelekea huko na wakati wote watakapoongoza nchi kwenye jumba hilo kwamba  ukweli ni kuwa Rais aliye madarakani hana mamlaka ya kutoa msamaha kwa mhalifu yeyote kabla hajapatikana na hatia mbele ya mahakama isipokuwa tu kama ibara ya 45(1) ya Katiba itabadilishwa  kumpa mamlaka hayo.

Alisema hakuna shaka yeyote  kuwa ofisi ya DPP ni moja ya ofisi kuu muhimu  ndani ya dola hivyo jinsi Katiba inavyoelekeza ndivyo inavyopaswa kuwa  katika nchi yenye kufuata utawala wa sheria.

“Ofisi ya DPP  ikiyumba na utawala huo utatereka vibaya, hilo likitokea hakuna mwananchi ambaye hataathirika kwa namna moja au nyingine, moja ya malengo ya sheria ni kumpa DPP uhuru katika kutumia mamkala yake na kuhakikisha hakuna woga, uonevu au upendeleo katika kuamua mshukiwa ashtakiwe au mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo yafutwe au laa,”alisema Jaji Samatta.

Alisema utenganisho huo wa mamlaka hayo pia unalenga kuzuia siasa kuingilia au kutumika katika masuala hayo nyeti na kitaalamu.

Alisisitiza kuwa ofisi ya DPP haipo kwa lengo la kuhakikisha kuwa mshukiwa lazima ashitakiwe au mshitakiwa lazima aonekane na hatia.

Alisema DPP   na maafisa walio chini yake ni watumishi wa nchi  ambao wajibu wao ni kulinda maslahi ya umma  yakiwemo yale yanayohitaji mtu asiye onyeshwa na ushahidi kuhusika  na utendaji wa kosa la jinai hashtakiwi na mshitakiwa ambaye ushahidi dhidi yake hauthibitishi kwamba alitenda kosa hatiwi hatiani.

Alisema kutumia njia za uonevu  na udanganyifu hakuwezi kuyafanya mapambano dhidi ya uhalifu likiwemo  kosa la rushwa yafanikiwe kinyume chake hatua hizo zitafanya mapambano dhidi ya uhalifu kutofanikiwa  na chuki dhidi ya watawala kujengeka.

“Mwananchi aliyeshitakiwa na kosa la rushwa na inaonekana na mahakama kuwa haijathibitishwa kutenda kosa hilo ana haki ya kuachiliwa ,kama mshitakiwa aliyeshitakiwa  na kosa lingine lolote na ushahidi dhidi yake unaposhindwa kulazimisha atiwe hatiani.

“Wakati mwingine siku hizi ninaposikiliza taarifa ya habari kupitia vituo vya televisheni napata picha kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wanateka mamlaka ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, bila shaka yoyote hatua hizo ni kinyume  cha Katiba na zinaweza kusababisha viongozi wakahukumiwa kama watafunguliwa kesi za madai mahakamani  na kuwalipa wanaonewa,”alisema Jaji Samatta.

Alisema hatua hizo za watawala zinaweza kusababisha kuharibika kwa kesi ambazo vinginevyo zingeweza kuthibitisha hatia za washtakiwa, uovu huo unaweza kutokea hata kwenye kesi za rushwa na mapambano dhidi ya uovu huo lazima yafanyike kisheria  na si vinginevyo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa taasisi ya Wajibu ambaye ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu, Ludovick Utouh alisema a alisema lengo la taasisi hiyo ni kuongeza ushirikishwa wa wananchi katika suala zima la uwajibikaji.

Alisema aliamua kumualika Jaji Samatta kwakuwa ni mmoja kati ya viongozi waadilifu ambao wanaongea na kutenda vitu ambavyo wanaviamini na kwamba ni miongoni mwa watu wanaochukia rushwa kutoka moyoni.

Alisema mkutano wa jana ambao ni wa tatu baada ya kufanyika mikutano mingine mwishoni mwa mwaka jana katika Chuo Kikuu Dodoma pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe kilichopo Morogoro ni muendelezo wa kutoa  elimu kuhusu uwajibikaji kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles