31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hasimu wa Maalim Seif awa Katibu Mkuu CUF

NA EVANS MAGEGE-DAR ES SALAAM

BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limemchagua Khalifa Suleiman Khalifa anayetajwa kuwa hasimu wa Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho.

Khalifa aliyewahi kuwa Mbunge wa Gando kisiwani Pemba kwa takribani miaka 20 alitajwa na Maalim Seif mwaka jana kuwa  ni miongoni mwa maswaiba wake watano waliomsaliti na kukisaliti chama hicho.

Maswaiba wengine aliowataja Seif ni pamoja na Seif Ali Iddi, Mohamed Mnyaa, Hamad Rashid pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CUF iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Lipumba, alisema wajumbe walioshiriki uchaguzi huo walikuwa 48.

Baada ya kura kupigwa, Khalifa, alishinda kwa idadi ya kura 37 huku mpinzani wake Masoud Said Suleiman akiambulia kura 11.

Alisema katika uchaguzi huo hakuna kura iliyoharibika na Khalifa ndiye aliyechaguliwa na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho akimrithi Seif.

Pia alisema baraza hilo limemchagua Magdalena Sakaya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara).

Alisema Sakaya alipata ushindi wa kura zote baada ya mshindani wake Zainabu Mdolwa kujiondoa kwa kuwaambia wanachama wate wampigie kura Sakaya.

Pia wajumbe wa baraza hilo wamemchagua Faki Suleiman Khatib kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Zanzibar.

“Faki kapata ushindi wa kura zote baada ya mpinzani wake Mohamed Buuai kujiondoa dakika za mwisho kwa kuwaomba wajumbe wampe kura zote za ndio Faki.

“Baada ya uchaguzi huu maana yake uongozi wa chama umekamilika na kifuatacho ni kazi ya kuwaunganisha wanachama kuwa wamoja chini ya ajenda yetu ya ‘furaha na haki sawa kwa Mtanzania,” alisema.

Lipumba alisema baada ya uongozi huo kukamilika kwa sasa chama hicho kinaingia katika mipango ya kutafuta ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na baadaye Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kwa upande wake, Khalifa aliwashukuru wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kwa kumchagua.

Alisema chama kimeishapata uongozi mpya, kilichobaki ni wanachama kusameheana na kujenga umoja mpya kwa maendeleo ya chama.

Alisema CUF kimepita katika mikwaruzo mingi hivyo wanachama wanatakiwa kuweka ubinadamu mbele kwa kuachana na yaliyopita kwa sababu hayajengi.

“Kwa wanachama walioondolewa uanachama wao na mkutano mkuu siwezi kuzungumza lolote kwa sababu huo ni uamuzi wa wajumbe wa mkutano mkuu lakini kwa wengine waliobaki tusameheane.

“Watusamehe na sisi tuwasamehe kwa sababu tumepita kwenye mikwaruzano mikubwa, tumeshambuliana vya kutosha, tumesemana vya kutosha na mimi kwa nafasi yangu napenda kuwaambia wanachama kwamba yaliyopita si ndwele tugange ya jayo kwa maendeleo ya CUF yetu,” alisema Khalifa.

Akizungumzia ni lini ataanza kutumia Ofisi Kuu za CUF upande wa Zanzibar ikizingatiwa kuwa ni ngome ya Maalim Seif, alisema hataanza kuitumia ofisi hiyo leo (jana) au kesho (leo) lakini siku yoyote kuanzia Jumatatu (kesho) ataanza kuitumia.

“Hili ni suala la kisheria kwa hiyo ofisi yetu ya Zanzibar si mali ya Maalim Seif bali ni mali ya wanachama, kwa hiyo utaratibu uko wazi, hakuna wa kujimilikisha mali ya wanachama,” alisema Khalifa.

Naye Sakaya alishukuru kwa wajumbe wa Baraza la Uongozi kwa kumuamini na kumchagua kwa mara nyingine katika nafasi hiyo.

Alisema siku zote ndani ya chama hicho ameishi bila kuyumbishwa na hatoyumba kwa sababu CUF ni Katiba pia ni taasisi na si mali ya Maalim Seif.

Alisema kwa sasa kikubwa kinachotakiwa ndani ya chama hicho ni umoja na mshikamano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles