24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

GWIJI WA HABARI KUAGWA LEO DAR

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


MWILI wa gwiji wa habari nchini, Chrysostom Rweyemamu maarufu ‘Mwalimu’ (64), unatarajiwa kuagwa leo nyumbani kwake Mbweni   Dar es Salaam.

 Rweyemamu alifariki dunia Jumamosi saa 2:30 usiku katika Hospitali  ya Taifa Muhimbili (MNH),   kwa mujibu wa maelezo ya daktari kwa watoto na mke wake ambao walijulishwa taarifa za kifo hicho juzi alfajiri walipokwenda kumjulia hali.

Ratiba iliyotolewa na familia jana  ilieleza kuwa shughuli za kumuaga zitaanza saa 4.00  asubuhi nyumbani kwake   ambako viongozi na wanahabari mbalimbali wanatarajiwa kushiriki.

  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African,  Absalom Kibanda, alisema jana kuwa shughuli hiyo itafanyika  saa 4 hadi 5 asubuhi kwa kuwa na ibada fupi nyumba kwa marehemu Mbweni kwa Masanja.

“Baada ya ibada fupi mwili wa marehemu utapelekwa Kanisa Katoliki Mbweni ambako baada ya ibada  itakayoanza saa 5 hadi 6, mwili utasafirishwa kwend wilayani Muleba mkoani Kagera kwa mazishi yatakayofanyika keshokutwa,” alisema Kibanda

Alisema Rweyemamu   alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni  kwa kama wiki tatu hivi kabla ya kulazwa Ijumaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji, kabla ya  hali yake kubadilika baadaye na akafariki dunia Jumamosi usiku.

Akizungumzia msiba wa baba yake, mtoto mkubwa wa marehemu, George Chrysostom alisema kilikuwa kifo cha ghafla kwa sababu hadi   wanaondoka   Muhimbili Jumamosi jioni  hali ya baba yakr ilikuwa ikiendelea vema.

Alisema   baba yake alikuwa akizungumza vizuri  baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe tumboni.

“Baba alikuwa mzima na alikuwa akizungumza na hata kuwatambua watu wote waliokuwapo pale na aliweza kwenda kuoga vizuri  jioni ya jana (juzi) kabla ya wao kuondoka,” alisema George.

Alisema kwa mujibu wa maelezo waliyopewa na daktari aliyekuwa akimtibu, baba yake kabla ya kufikiwa na mauti alianza kupata shida ya kupumua ghafla hatua iliyosababisha daktari aliyekuwa akimhudumia kuitwa   kujaribu kuokoa maisha yake lakini haikuwezekana.

Alisema daktari aliwaeleza kwamba upo uwezekano mkubwa kwamba  marehemu alipata tatizo la damu kuganda katika mapafu hali iliyosababisha apate mshituko wa moyo uliochukua maisha yake.

Mtoto huyo wa marehemu alisema   mwili wa baba yake unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda kwao, Kishanda katika Kijiji cha Iyunga Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambako mazishi yatafanyika keshokutwa.

Mwalimu Chrysostom Rweyemamu ameacha mjane na watoto watatu wa kiume.

Marehemu Chrysostom Rweyemamu, alijiunga na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Oktoba mwaka 1999 wakati huo ikijulikana kama Habari Corporation na kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Maarifa Media Trust. (MAMET)

Jana wanahabari mbalimbali wakongwe waliowahi kufanya kazi na marehemu Chrysostom, walikuwapo nyumbani kwake,  wakiwamo Jenerali Ulimwengu, Dk. Gideon Shoo, John Bwire na Mayage S. Mayage.

Kabla ya kukutwa na umauti, Jumamosi ya wiki iliyopita marehemu alifanyiwa upasuaji wa uvimbe  siku ya Ijumaa na hali na alitoka vizuri katika upasuaji huo na kuamka salama lakini hali yake ilibadilika baadaye.

Mwakyembe amlilia

Waziri wa Habari,, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema amepokea kwa mshtuko kifo cha mwanahabari Chrysostom  Rweyemamu kwa sababu  anamfahamu gwiji huyo wa habari kutokana na uhodari wake katika masuala ya habari.

“Ninapenda kutoa salamu zangu za pole kwa Kampuni ya magazeti ya New Habari (2206) Ltd, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wana tasnia ya habari   na watanzania wote nchini. Ninawaomba muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na gwiji huyu wa habari,” alisema Dk. Mwakyembe katika taarifa yake.

Hadi mauti yanampata marehemu Chrysostom,  alikuwa Mhariri wa Mafunzo wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles