25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MCHANGA WA MADINI WACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI

MAREGESI PAUL-DODOMA na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


MCHANGA wa dhahabu uliozuiwa katika makontena Bandari ya Dar es Salaam, umezua mjadala bungeni baada ya wabunge wa CCM na Chadema kupingana juu ya uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kuyazuia kusafirishwa nje ya nchi.

Hayo yalitokea jana wabunge walipokuwa wakichangia hotuba ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa na Waziri Balozi Augustine Mahiga.

Wakichangia bajeti hiyo, wabunge wawili wa Chadema, Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Godbless Lema (Arusha Mjini), walisema uamuzi wa Rais Magufuli utalisababishia taifa hasara na kuwafukuza wawekezaji wa nje.

Naye Lema alisema amepata taarifa kwamba wamiliki wa mgodi wa Acacia ambao makontena yao yamezuiwa, wamefungua kesi katika Mahakama ya London, Uingereza, kulalamikia uamuzi huo wa Serikali.

“Katika hatua ya kulinda rasilimali ya nchi, ni mwendawazimu anayeweza asipongeze, lakini lazima tujue ni namna gani unalinda rasilimali hizo bila kuligharimu taifa.

“Wote tunafahamu taifa letu lina mgogoro na Acacia Minning ambao kwa sura ya kwanza, mgogoro huo unajenga hisia za siasa ndani ya nchi na sura ya pili ya mgogoro huo unapunguza kasi ya wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini.

“Leo (jana) tunapongeza alichokifanya Rais, tuelewe wakati Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anaanza sera ya kunyang’anya watu mashamba na kuwakandamiza wawekezaji, alipigiwa makofi na watu wake kama ambavyo sisi tunapiga makofi leo.

“Matokeo yake leo Zimbabwe hawana noti yao, hawana fedha yao na ni taifa ambalo halina ‘identity’.

“Katika suala hili ni muhimu mumshauri Rais kwa sababu  gharama za uamuzi wake ni kubwa, ikizingatiwa Acacia leo wamekwenda mahakamani London na kwa hali ya kawaida, taifa hili litaingia kwenye gharama kubwa kama tulivyoingia kwenye minofu ya samaki,” alisema Lema.

 

TUNDU LISSU

  Lissu alisema amekuwa akipinga sera mbaya za uwekezaji tangu mwaka 1999 na kwamba uamuzi alioufanya Rais Magufuli si mzuri na ataupinga kama ambavyo amekuwa akipinga sera zote ambazo zimelifikisha taifa pabaya.

Alisema uamuzi wa kuzuia makontena hayo unalichafua taifa kimataifa na kuwaogopesha wawekezaji wa nje.

“Suala siyo Acacia watafanya nini, suala ni watu wote tunaohusiana nao kwenye uchumi kama Wachina ambao ndiyo taifa kubwa duniani kwa uwekezaji watafanya nini.

“Fikiria, Jumuiya ya Ulaya, Japan na Marekani watafanya nini kwa sababu ya kuwanyang’anya mchanga wa dhahabu Acacia.

“Sisi tunazungumza masuala ya diplomasia ya uchumi wakati hatujui lolote kuhusu diplomasia ya uchumi, ndiyo maana tunafanya haya tunayoyafanya. Kwa hiyo, waziri nakuomba usikubali hizi kelele kwa sababu hivi sasa nchi yetu ina hali mbaya kwenye diplomasia.

“Tulichokifanya ni makosa katika sheria, mikataba ni makosa kwa mujibu wa sheria za mataifa. Kwa taarifa yenu, gharama tutakazolipa katika jambo hili ni kubwa kuliko huo mchanga wa Acacia.

“Tutakuwa na kesi kama Zimbabwe, tusishabikie uamuzi uliofanyika kwa sababu tu umefanywa na Rais,” alisema Lissu.

Hatua hiyo ilimfanya Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Jenister Mhagama, aombe mwongozo kwa mwenyekiti wa Bunge kutokana na lugha kali aliyokuwa akitumia mbunge huyo (maneno hayo makali hatukuyaandika).

Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alimtaka Lissu afute maneno hayo makali, jambo ambalo alilikubali ingawa alisisitiza kupingana na uamuzi wa Rais Magufuli.

 

WABUNGE WA CCM

Wabunge wa CCM nao waliamua kujibu mapigo kwa kusema uamuzi uliofanyika ni sahihi kwa kuwa nchi ilikuwa ikiibiwa.

 

SHONZA

  Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza, aliwashamnbulia Lema na Lissu akisema hawaaminiki kwa kuwa walikuwa wakimsema vibaya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa ni fisadi, lakini alipohamia Chadema wakampigia kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Wewe Lissu na Lema, mlikuwa mkimsema vibaya Lowassa ni fisadi, alipokuja kwenu mkaanza kumsafisha. Je, huo siyo uamuzi mbaya?

“Yaani nyie kila kinachofanywa na Serikali mnaponda kwa sababu mmejipa vyeo vya mtoto wa kambo. Eleweni nchi hii inahitaji Rais kama Magufuli, nyie wenzetu endeleeni kutetea wezi, sisi tumeshawazoea.

“Tunamuomba Mheshimiwa Rais aendelee kuchapa kazi, nyie wenzetu muendelee kulalamika, sisi hapa kazi tu,” alisema Shonza.

 

SERUKAMBA

  Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisema uamuzi uliofanywa na Rais Magufuli ni sahihi na utaigwa na mataifa mengine duniani.

Alisema kuna haja ya Watanzania kushirikiana katika uamuzi huo kwa masilahi ya taifa.

 

COSATO CHUMI

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi, aliwatoa hofu Watanzania kwa kusema kama Acacia watakwenda mahakamani, Serikali itakwenda pia kwa kuwa jambo hilo linawezekana.

“Tutabishana hapa kutafuta umaarufu kwa sababu kama ni mahakamani tutakwenda pia. Hata mtu wa kawaida ukimwambia jambo hilo alilofanya Rais atakuunga mkono na nawaomba tusipinge kila kitu kwa sababu ya itikadi zetu,” alisema Chumi.

Wengine waliounga mkono uamuzi wa Serikali huku wakitaka Watanzania washirikiane katika jambo hilo, ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Mwanjelwa, Ester Mahawe na Rose Tweve.

 

MWANASHERIA MKUU

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliwataka wabunge wasishabikie suala la wawekezaji hao kwenda mahakamani kwa sababu wakienda huko hawataishtaki CCM bali wataishtaki Tanzania.

“Nawaomba waheshimiwa wabunge muiunge mkono Serikali katika jambo hili kwa masilahi ya Taifa, nchi ikishtakiwa, haitashtakiwa CCM.

“Kilichofanyika hakina makosa kwa mujibu wa sheria kwa sababu mkataba una kipengele kinasema unaweza kupitiwa upya baada ya miaka mitatu, kwa hiyo nawaomba tushirikiane,” alisema Masaju.

 

SOKO LA HISA

Katika hatua nyingine, bei ya hisa za Kampuni ya Acacia katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeshuka kwa asilimia 32.7.

Hali hiyo inatokea ikiwa ni wiki moja baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya uchunguzi wa mchanga (makinikia) wa kampuni hiyo.

Akizungimza Dar es Salaam jana, Meneja Mauzo wa DSE, Patrick Mususa, alisema kampuni nyingine ambazo hisa zake zimeshuka ni pamoja na Uchumi kwa asilimia 28.6 na JHL asilimia 17.8.

Alisema kushuka huko kumesababisha kupungua ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa sokoni kwa Sh trilioni 1.5 kutoka Sh trilioni 19.9 hadi trilioni 18.4.

"Pamoja na idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa kuongezeka kutoka hisa milioni 1.1 hadi milioni 2.2, lakini thamani ya mauzo ya hisa imepungua kutoka Sh bilioni 8 hadi bilioni 2.6.

"Kampuni zilizoongoza katika mauzo ya hisa ni TBL kwa asilimia 77.3, Benki ya CRDB 13.3 na TOL asilimia 8.4," alisema Mususa.

  Mususa alisema mtaji wa kampuni za ndani umeongezeka kwa Sh bilioni 13 kutoka Sh trilioni 7.056 hadi trilioni 7.069, baada ya kuongezeka kwa bei ya hisa za Benki ya CRDB asilimia 2.7.

Alisema mauzo ya hati fungani yalipungua kutoka Sh bilioni 29.5 hadi bilioni 2.9, baada ya hati fungani saba za Serikali zenye thamani ya Sh bilioni 3.8 kwa gharama ya Sh bilioni 2.9.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles