VIPAUMBELE VYA IGP SIRRO HIVI HAPA

0
664

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


MKUU mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kupambana na uhalifu na kuboresha nidhamu ya watendaji ndani ya jeshi hilo.

Rais Dk. John Magufuli juzi alimteua Sirro kushika wadhifa huo, huku akisema kuwa aliyekuwa IGP, Ernest Mangu, atapangiwa kazi nyingine.

Akizungumza baada ya kuapishwa jana, Sirro alisema atahakikisha Watanzania wanaishi kwa amani na utulivu na kuboresha nidhamu kwa sababu bila nidhamu ni vigumu kupambana na uhalifu.

“Napata kigugumizi sababu ya furaha, namshukuru Rais kwa kuniamini na kunipa nafasi hii, amewiwa na utendaji wangu.

“Kazi yetu kubwa ni kulinda watu na mali zao, nawaomba wananchi wanipe ushirikiano, uhalifu hauwezi kupungua kwa kutegemea Jeshi la Polisi peke yake,” alisema Sirro.

Kuhusu mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, alisema kunahitajika nguvu ya pamoja kuweza kuishinda vita hiyo.

“Najua tuna changamoto kubwa ya Ikwiriri, Rufiji na maeneo mengine ya Pwani, tuko vizuri na tutaingia kufanya kazi kuhakikisha kwamba Wanapwani wanaishi kwa amani na utulivu.

“Wananchi watuamini, watupe taarifa kwa sababu ‘information is power’, wasipotupa taarifa itakuwa ni kazi ngumu,” alisema.

 

MANGU

Kwa upande wake, Mangu alisema katika uongozi wake kitu ambacho hawezi kukisahau ni aina ya uhalifu ambao alidai kuwa hajawahi kuushuhudia nchini.

“Viko vingi, lakini nakumbuka tulipambana na uhalifu ambao sijawahi kuushuhudia katika nchi yetu,” alisema.

Akimzungumzia IGP Sirro, alisema ana uzoefu wa kutosha ndani ya jeshi hilo na anaamini kwamba ataweza kukabiliana na changamoto ya uhalifu nchini.

“IGP mpya si mgeni ndani ya Jeshi la Polisi, alikuwa katika nafasi ya juu, hivyo anaelewa changamoto zilizopo na hatua za kuchukua, naamini amejipanga kukabiliana na changamoto ya uhalifu uliopo nchini.

“Nawaombeni waandishi wa habari mumpe ushirikiano kama mlivyofanya kwangu ili aweze kukabiliana na majukumu yake kwa ufanisi,” alisema.

 

DALILI ZA MABADILIKO

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba mabadiliko hayo yamekuja huku Jeshi la Polisi likikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo wizi wa silaha na mauaji dhidi ya raia na polisi katika matukio mbalimbali.

Matukio mengine ni mauaji ya baadhi ya viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na raia katika wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

Mathalani matukio ya majambazi kuvamia vituo vya polisi na kuua yalimkera Rais Magufuli ambaye alilitaka Jeshi la Polisi kuwadhibiti ili kukomesha vitendo viovu katika taifa.

Juni 25, mwaka jana wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Jamii, Rais Magufuli alisema: “Inashangaza jambazi anavamia kituo cha polisi anaua na anaondoka wakati polisi wapo na wana silaha na risasi wanazo, lakini wanashindwa kumnyang’anya silaha.”

 

WIZI WA SILAHA, MAUAJI

Habari nyingine zinadai kuwa huenda uteuzi wa IGP mpya umesukumwa zaidi na mauaji ya raia na askari polisi, wanaouawa kwa kupigwa risasi katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.

Hadi sasa watu 31 wakiwamo askari polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wameuawa mkoani humo huku chanzo cha mauaji hayo kikiwa hakijulikani.

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonyesha kati ya mwaka 2014 hadi sasa askari polisi 36 wameuawa.

Pia zaidi ya silaha 60 ziliibwa katika vituo vya polisi vya Newala, Ikwiriri, Kimanzichana, Ushirombo, Tanga, Mgeta, Pugu na Stakishari.

 

KAULI YA CCM

Wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilitoa tamko kuhusu mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, huku kikiwataka viongozi wenye dhamana na usalama wa wananchi kujitafakari.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ikiwa mauaji hayo yataendelea, chama hicho kitaielekeza Serikali kuchukua hatua kwa walio na dhamana kwa kutowajibika katika majukumu yao.

 

WATEULE WA JK

Kwa hatua ya kutengua uteuzi wa Mangu, ni wazi sasa Rais Magufuli amekamilisha kufanya mabadiliko ndani ya vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuweka wateule wake, huku wale waliokuwapo tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya nne chini Jakaya Kikwete, wengi wao wakiwekwa kando.

Aprili mwaka jana, alimteua Kamishna wa Polisi, Thobias Andengenye kuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Desemba 2 mwaka jana, alimteua Kamishna wa Magereza, Dk. Juma Malewa kuwa Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza baada ya kuridhia ombi la kusitisha mkataba na kustaafu kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), John Minja.  

Februari 2 mwaka huu, alimteua Luteni Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi baada ya Jenerali Davis Mwamunyange kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Februari 10 mwaka huu, alimteua Dk. Anna Makakala kuwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji.

 

VIONGOZI WA DINI

Wakizungumza baada ya kuapishwa kwa IGP Sirro, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga, alisema kiongozi huyo watashirikiana naye katika kazi zake.

 “IGP Sirro ni mtulivu na ni mtu anayetafakari maamuzi yake bila kujali presha au maagizo ya kisiasa,” alisema Askofu Mwamalanga.

Alimwelezea IGP Sirro kuwa ni kiongozi ambaye anawashirikisha wafanyakazi wenzake na wananchi kwa ujumla ili kuleta amani, kazi ambayo huifanya kwa weledi.

Ameongeza kuwa kiongozi huyo wa juu katika Jeshi la Polisi ni mtu mwenye kuthubutu, hasa katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na ujambazi.

“Nakumbuka Sirro ni polisi wa kwanza kupata tuzo katika kufanikiwa kudhibiti majambazi,” alisema Askofu Mwamalanga.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa, alimpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi wa Sirro akisema ni mtu makini na mwenye kuheshimika kutokana na utendaji wake.

“Tumeona weledi wake, utendaji wake ndani ya Jeshi la Polisi, hivyo Kamishna Sirro anatosha na tunamwamini,” alisema Sheikh Alhad.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here