DANI ALVES AFUNGA NDOA KIMYA KIMYA

0
687

IBIZA, HISPANIA


BEKI wa pembeni wa timu ya Taifa ya Brazil, Dani Alves, amefanikiwa kufunga ndoa kimya kimya na mpenzi wake wa muda mrefu kutoka nchini Hispania, Joana Sanz.

Harusi hiyo imefanyika kwenye visiwa vya Ibiza, ambapo Alves hakutaka kuiweka wazi kwenye mitandao ya kijamii hadi pale alipofanikiwa kukamilisha zoezi hilo.

Harusi hiyo ilikuwa ya aina yake, kwa kuwa ilitumia muda mfupi kumalizika, lakini rafiki zake wa karibu walikuwa wa kwanza kuposti picha kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilimuonesha Alves akifunga ndoa na mwanamitindo huyo.

Joana, mwenye umri wa miaka 23, ni miongoni mwa wanamitindo maarufu sana nchini Hispania, kutokana na kuwa na matangazo mengi kwenye majarida mbalimbali, kama vile Ella pamoja na Jimmy Choo.

Mwanamitindo huyo kwenye akaunti yake ya Instagram ina zaidi ya marafiki 345,000, hivyo baada ya kutupia picha zake za harusi zilisambaa kwa muda mfupi kwenye mitandao mingine ambazo zilisambazwa na marafiki hao.

Alves mara ya mwisho alikuwa anakipiga katika kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu nchini Italia, Juventus, kwa sasa amemalizana na klabu hiyo na yupo huru kujiunga na timu yoyote.

Hata hivyo, inasemekana kuwa, mchezaji huyo tayari amemalizana na uongozi wa klabu ya Manchester City kwa ajili ya kujiunga kwa mkataba wa miaka miwili na dili hilo linatarajiwa kukamilika mapema wiki hii.

Matajiri wa mjini Paris nchini Ufaransa, PSG, ni miongoni mwa klabu ambazo zinaingilia kati uhamisho wa mchezaji huyo kwenda Manchester City, hivyo matajiri hao wanataka kuwapiku Manchester City katika kuwania saini ya mchezaji huyo wakati huu wa usajili.

Lakini bado Manchester City wana nafasi kubwa ya kuinasa saini yake, kutokana na mchezaji huyo kudai kuwa anataka kufanya kazi kwa mara ya pili na kocha wa klabu, Pep Guardiola.

Awali mchezaji huyo aliwahi kufanya kazi na Guardiola katika klabu ya Barcelona tangu mwaka 2008 hadi 2012, ambapo Guardiola aliamua kuondoka na kujiunga na wababe wa nchini Ujerumani, Bayern Munich.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here