25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA JAY KUFANYA UPYA SHEREHE YA NDOA YAKE MIKUMI

Na MWANDISHI WETU



HISTORIA iliyowekwa Julai 8, mwaka 2017 ya kufunga ndoa kati ya Mbunge wa Jimbo la Mikumi kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia ni rapa mkongwe kwenye muziki wa Bongo Fleva, Joseph Haule (Profesa Jay) na Grace Mgonjo (Mama Lisa) haitafutika tena.

Ndoa hiyo imefanyika baada ya miaka zaidi ya 13 ya uchumba wa wawili hao.
Kwa mujibu wa wawili hao, hadi kufikia mafanikio ya ndoa hiyo wamepitia mambo mengi, ambayo kama wasingekuwa na uvumilivu wasingefikia hatua hiyo njema kwa Mungu.

Profesa Jay, anayetamba na wimbo wa ‘Kibabe’, alifunga ndoa hiyo Kanisa la St. Peter, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, kisha sherehe ya harusi hiyo ikafanyika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambako wabunge na viongozi mbalimbali wa chama na serikali walihudhuria, bila kujali tofauti zao za kisiasa.

Ujumbe muhimu kwa Profesa Jay kwa wasanii wenzake ni kwamba, umefika wakati wa wasanii kuachana na maisha ya ubachela, waingie kwenye maisha ya ndoa kwa kuwa ni hatua nzuri na kumpendeza Mungu na faida nyingine nyingi.

Wahudhuriaji wengine waliojitokeza kwenye sherehe ya harusi hiyo ni wanamuziki mashuhuri nchini, akiwamo Ambwene Yessaya (AY), Joseph Mbilinyi (Sugu), Black Ryhno ambaye ni mdogo wa kuzaliwa wa Profesa Jay, Abdul Nassib (Diamond Platnumz), Harmonize na wengine wengi.

Wasanii hao kila mmoja alipata fursa ya kuburudisha wanandoa na watu waliojumuika katika Ukumbi huo wa Mlimani City na shoo zao ziliburudisha vya kutosha.

Hard Blasters wakutana
Profesa Jay, aliyezaliwa Desemba 29, 1975 huko Songea, alitumia nafasi hiyo kukumbushia kundi lao la Hard Blasters (HBC) kwa kuwakutanisha wasanii wenzake waliokuwa wakiunda kundi hilo, ambao ni Willy Terry (Fanani), Big Willy na Nigga J, ambaye sasa ndiye Profesa Jay.

 

Zawadi/Ofa

Licha ya kupewa zawadi nyingi, lakini wasanii waliofurahisha na kuonekana kama kichekesho ni zawadi ya karanga za msanii Nassib Abdul (Diamond), baada ya kuelezwa na meneja wake, Babu Tale, nyingine ni ofa aliyoitoa Mbunge wa Mbeya Mjini, ambaye pia ni rapa, Joseph Mbilinyi (Sugu), aliyewataka wanandoa hao kwenda kupumzika jimboni kwake kwa muda wa wiki nzima, baada ya kumaliza safari za honeymoon zao wanazotarajia kufanya nje ya nchi.

Sherehe kubwa Mikumi

Wengi wamehudhuria kwenye sherehe yake hiyo iliyokuwa na mialiko, lakini anaamini kwamba wengi wa wapigakura wa jimboni kwake hawakupata nafasi ya kuhudhuria sherehe za ndoa yake hiyo, hivyo ameamua kwenda kufanya sherehe nyingine kwa ajili yao.

“Nimepanga Jumapili ijayo kwenda kufurahi na wapigakura wangu wa Mikumi, kutakuwa na sherehe kubwa kwenye uwanja wa mpira wa Mikumi, mkoani Morogoro, uwanja wa wazi, hakutakuwa na kiingilio chochote, kila atakayeweza kufika anakaribishwa, kula kunywa, kucheza na kupongeza mafanikio yetu.

“Naamini wengi wa wapiga kura wangu walipenda kuhudhuria kwenye harusi yangu, lakini wameshindwa kutokana na sababu mbalimbali, hivyo nimeamua kwenda kujumuika nao kwenye uwanja wa wazi ili tule na tufurahi pamoja,’’ anaeleza Profesa Jay.

Alipotokea

Profesa Jay aliingia kwenye muziki mwaka 1994, akijiita Nigga J, kipindi hicho alikuwa kwenye kundi la Hard Blasters pamoja na wasanii wengine wawili, Willy Terry (Fanani) na Big Willy na wakafanikiwa kuachia albamu yao ya kwanza ya ‘Funga Kazi’ na baada ya mwaka mmoja walikuwa kundi bora la hip-hop nchini Tanzania.

Mwaka 2001 alijiondoa kwenye kundi hilo akawa akifanya kazi zake binafsi, hapo akaachia nyimbo mbalimbali, zikiwamo ‘Nikusaidiaje’ na ‘Zali la Mentali’, aliomshirikisha Juma Nature.

Nyimbo nyingine ni ‘Piga Makofi’, ‘Yataka Moyo’, ‘Ndiyo Mzee’, kisha akatoa albamu yake ya kwanza akiwa msanii anayejitegemea akaiita ‘Machozi, Jasho na Damu’ na ameshinda tuzo mbalimbali za muziki, ikiwamo albamu bora ya hip-hop ‘Mapinduzi halisi’.

Ameshirikiana na wasanii mbalimbali wa ndani na nje, ukiwemo ‘Nikusaidiaje’ na ‘Vuta raha’ aliomshirikisha Ferooz, ‘Nimeamini’ aliomshirikisha Lady Jaydee, ‘Inatosha’ aliomshirikisha Sugu, ‘Border kwa border’ aliomshirikisha Nazizi, ‘Heka heka za star’ na ‘J.O.S.E.P.H.’.

‘Nisamehe’ aliomshirikisha Banana, ‘Wapi nimekosea’, ‘Hakuna Noma,’ ‘Jina Langu’, ‘Bongo Dar es Salaam’, ‘Piga Makofi’, ‘Msinitenge’, ‘Kikao cha Dharura’, ‘Zali la Mentali’, ‘Ndivyo Sivyo’, ‘Mtazamo’, alioshirikishwa na Afande Sele, ‘Hapo Sawa’ na ‘Kumekucha’ alioshirikishwa na Nonini.

Albamu yake ya kwanza ni ‘Machozi, Jasho na Damu’ iliyotoka mwaka 2001,’ ‘Mapinduzi Halisi’ uliotoka mwaka 2003, ‘J.O.S.E.P.H’ iliyotoka mwaka 2006, ‘Aluta Continua’ ya mwaka 2007, ‘Izack mangesho’ iliyotoka mwaka 2014 na ‘Kazi Kazi’ ya mwaka 2016.

Alishinda tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2004 albamu yake ya ‘Mapinduzi Halisi’ ilikuwa albamu bora ya mwaka, mwaka 2006 wimbo wake wa ‘Nikusaidiaje’ uliibuka wimbo bora.

Kupitia tuzo ya Kisima Music na wimbo wake wa ‘Ndivyo sivyo’ alioshirikiana na msanii wa Uganda, Chameleone, ukawa wimbo bora kwa Uganda na tuzo nyingine nyingi, ikiwemo ya mwandishi bora wa muziki aliyoipata mwaka 2009 na mwaka 2007 alishinda tuzo ya ‘Pearl of Africa Music Awards’ (PAM Awards)kama msanii bora wa kiume.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles