24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CUF WANA NIA YA KULETA MAGEUZI YA KWELI?

WIKI iliyopita tumesikia Mahakama Kuu ikitoa uamuzi wa kumuachia huru Mbunge wa Chadema aliyekuwa amefungwa kwa miezi sita pia uamuzi  kuwa Chama Cha Wananchi (CUF) chini ya uongozi wa Prof. Lipumba kisipatiwe ruzuku hadi shauri lililopo mahakamani litakapokwisha.

Pia wiki hiyo hiyo tumeona kwenye mitandao ya kijamii  kulikuwa Dk. Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema ikisemekana amedai kuwa anarejea nchini. Kurejea nchini si hoja ila akirejea naye atakuja na yapi?. Tunakumbuka yeye na  Prof. Lipumba  waliondoka kwenye vyama vyao karibu wakati mmoja na Prof. huyu  aliporejea ndio unaonekana mgogoro unaofukuta hadi kutishia uhai wa chama hicho.

Katika kuangalia hali inayoendelea ya vyama vya siasa tangu mfumo huu wa vyama vingi vya siasa uanze ninadhani ipo  sababu ya kujiuliza iwapo kweli dhamira ya uwepo wa vyama hivyo au la?

Kurejea kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini haikuwa kazi rahisi,wapo watu waliofanya utetezi na kwa wakati ule hawakueleweka kabisa lakini walikuwa  wanaelewa umuhimu wa uwepo wa vyama hivyo vingi vya siasa. Kama mnavyofahamu nchi yetu wakati tunapata uhuru vyama vya siasa vilikuwa zaidi ya kimoja ila viliondolewa na tukabaki na mfumo wa chama kimoja na chama hicho kilikuwa ni chama kilichopigania uhuru chama cha TANU  na kwa upande wa Zanzibar Afro Shirazi Party (ASP).Vyama hivi vliliendelea hata baada ya nchi mbili kuungana mwaka 1964  kila kimoja kikifanya kazi upande mmoja wa Muungano.

Mwaka 1977 ndipo vilipounganishwa na kuwa chama kimoja cha CCM. Chama hiki kilishika hatamu za uongozi wa Serikali kwa kipindi chote hicho. Hata hivyo wimbi la mageuzi lilianza kutanda na miaka ya mwanzoni mwa tisini vuguvugu liliongezeka. Ilikuwa si rahisi kuona mabadiliko hayo ndio maana shirika la TANLET lililoratibu kongamano kubwa la kuzungumzia uwezekano wa uwepo wa mfumo wa vyama vingi lilitaka kufutwa.

Mabadiliko hata hivyo  ilibidi yatokee hata baada ya Tume ya Jaji Nyalali kuonyesha kuwa asilimia themanini ya Watanzania hawaoni sababu ya kuwa na mfumo wa vyama vingi. Hawa Watanzania walihojiwa wakati  wakiwa hawauelewi mfumo huo na maana yake kwao ni nini? Baada ya mfumo kuanza hata hivyo palikuwa na wimbi kubwa sana la mageuzi watu wengi hasa wa mijini wakijiunga na vyama hivi vya siasa vinavyoitwa vyama vya upinzani. Jambo ambalo limekuwa dhahiri tangu mfumo huu uanze ni kuwa vyama hivyo vikipata nguvu tu migogoro inaanza au inaanzishwa na inafukuta hadi ama  chama kinapoteza mwelekeo au kinakosa nguvu kabisa.

Vyama ambavyo vinapata migogoro ni vile ama vyenye nguvu na ushindani mkubwa au vile vyenye watu ndani yake wanaoonekana kuwa na ushawishi mkubwa. Nikitoa mifano michache kuanzia mwaka 1992 mfumo huu ulipoanza aliyekuwa anazungumza kwa ushawishi mkubwa sana wakati huo kabla hata ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi alikuwa Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila.

Huyu alipata hekaheka na akawa mara nyingi ana kesi na hata aliwahi kutiwa hatiani na kufungwa. Mwaka1995 Chama cha NCCR- Mageuzi kilipata nguvu kubwa na kikaonekana ni chama  chenye wanachama wengi na kikaweza kugombea nafasi ya urais na mgombea wao alipata karibu theluthi ya kura.

Mara baada ya uchaguzi huo mkuu na chama hicho kupata wanachama wengi sana mgogoro ulifukuta na nakumbuka waliweza kupigana kabisa kule Tanga  na ndio ukawa mwanzo wa mwisho wa umaarufu wa chama hicho kilichokuwa kimepata wanachama na nguvu kubwa sana ya upinzani nchini.

Chama Cha Wananchi (CUF) kilionekana kuwa ndicho kinafuatia kwa umaarufu na hasa huko Zanzibar na pia kilipata sifa ya kuwa na nguvu ya ndani yankuweza kuwagundua watu wanaotaka kukiharibu chama chao na hivyo kwa muda mrefu sana kiliendelea vizuri. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nacho kimeendelea kukua taratibu huku kikijipatia nguvu taratibu.

Wakati wa Bunge Maalumu la Katiba jambo jipya lilijengeka pale  vyama vya upinzani vilivyoamua kususia Bunge lile na kwa pamoja wakajitambua kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Umoja huu uliachana na suala la mchakato wa Katiba Uchaguzi Mkuu ulipofika na wakaunganisha nguvu  kukikabili chama tawala.

Hapa nguvu yao pia ilionekana na hasa mwanaCCM maarufu alipokihama chama hicho tawala na kujiunga katika chama kimojawapo na kupewa  fursa ya kugombea urais. Uchaguzi huo wa Mwaka 2015 ulionekana wa tofauti sana  kwa vyama hivyo vya upinzani kupata wafuasi na kuwa na kampeni zilizoonekana kuwa na mvuto sana .

Jambo la kushangaza sana ni kuwa iwapo vyama hivi vya siasa vya upinzani nia yao kweli ni kuleta mageuzi nchini na kukipa chama tawala upinzani au kukifanya kifanye kazi yake vyema na hata wakiweza wakiondoe iweje basi waruhusu migogoro ya aina tunayoiona?

Kuna wakati chama kinamfukuza mbunge ambaye tayari wameshampata. Hata kama kuna matatizo kwa watu wanaotazama lengo kuu mbele yao wasingeshindwa kumaliza matatizo yao ya ndani kwa kukinusuru chama. Kilichokuja kushangaza zaidi ni huu mgogoro ambao naweza kusema ni wa kwanza kwa ukubwa na wa aina yake kwa Chama Cha Wananchi (CUF). Hivi kweli wanaCUF wana nia ya kuleta mageuzi ya kweli nchini?

Kitu gani kinachowafanya washindwe kuafikiana kwa ajili tu ya kukinusuru chama chao na kusimamia ajenda kuu ya  kuleta mageuzi na ushindani wa kisiasa dhidi ya chama kilichoko madarakani? Wote wanaoonekana kuleta shida wapo kwenye hicho chama kwa muda mrefu sasa na wanakijua chama hicho fika, kwanini wasiamue kuachana na hayo malumbano ili tu chama chao kipone? Na hao wanachama wa chama hicho wanashindwa nini kuwaondoa wote wanaoonekana kuwarudisha nyuma? Kwani chama hicho ni cha viongozi  tu wanachama wako wapi?

Mara nyingi pia tunaona vyama hivi huwa vinaanza mizozo wakati uchaguzi unapokaribia sasa tujiulize huwa wanakuwapo watu wanaotumwa kukivuruga chama ili kipoteze mwelekeo? Na kama wapo wanaotumwa wale ambao ndio wenye chama wanakuwa wapi hadi chama kiingiliwe kiasi hicho? Ukitafakari sana unaona kuwa uwepo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini ni kama kuchezeshwa shere tu si kitu kilichokuwa kimemaanishwa bali ili kudhihaki dunia kuwa tuna mfumo huo.

Tunaona wale wanaoonekana kumaanisha kusimamia upinzani halisi ndio huwakuta katika  matatizo makubwa kama vile kupata kesi za mara kwa mara , kuwekwa ndani na hata imefikia kiongozi wa upinzani mbunge kufungwa jela kwa njia inayoonekana ni ya uonevu.

Hoja ni kuwa iwapo hatuutaki mfumo huu wa vyama vingi sidhani tunalazimishwa, lakini kwa vile tuliukubali na kuingiza kwenye Katiba kama mfumo tunaotaka uongoze siasa zetu basi tuuheshimu. Kama mfumo umetushinda tuko kwenye mchakato wa Katiba hebu tujitafakarishe. Si haki kuona watu wanaonewa kwa vile tu wanasema kweli na kusimamia yale wanayoyaamini katika  mfumo huu.

Na si sawa kwa Watanzania kuangalia jinsi watu wanavyotenda vitendo ya kuharibu kwa makusudi mfumo huu na  wakanyamaza tu. Kujiunga na vyama vya siasa ni hiyari lakini kuwapo kwenye vyama hivyo si kosa kwani vipo kisheria na ni haki. Pamoja na kuwa migogoro huweza kuwa njia nzuri ya kuleta maendeleo lakini migogoro ya kutengeneza si afya kwa vyama hivyo.

Ipo migogoro inayoibuka  kama sehemu ya kukua kwa vyama lakini mingi tunayoiona ni ya kutengeneza na ina madhara si kwa chama husika tu bali ni kwa mfumo mzima wa vyama vingi vya siasa. Tujitazamishe.

Imeandaliwa na

DKT.Helen KijoBisimba

Mkurugenzi Mtendaji -LHRC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles