TUZO yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5, hutolewa kila mwaka kwa Rais wa nchi ya Afrika aliyeboresha usalama, afya, elimu, maendeleo ya kiuchumi na haki za kisiasa katika nchi yake na kukabidhi madaraka kwa misingi ya kidemokrasia kwa mrithi wake.
Kwa mara nyingine, wakfu wa Mo Ibrahim, Jumanne ya Machi 28, mwaka huu, ulitangaza kuwa hajapatikana kiongozi ambaye amekidhi sifa zote zinazohitajika katika mwaka 2016, ikiwa ni mara ya sita katika miaka kumi tangu kuanzishwa tuzo hiyo mwaka 2006.
Ni Marais wa zamani watano tu kutoka Afrika ndio walishapata tuzo hii, huku mara ya mwisho tuzo hiyo akiwa amepewa Rais wa zamani wa Namibia Hifikepunye Pohamba, mwaka 2014.
Wengine waliowahi kuipata ni Pedro Pires wa Cape Verde, Festus Mogae wa Botswana, Joachim Chissano wa Msumbiji na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tuzo hiyo, Dk. Salim Ahmed Salim wakati akitoa tangazo la kutompata mshindi alisema kuwa, tuzo hiyo ina vigezo vya juu kama vilivyoorodheshwa katika haya ya kwanza na vinawalenga viongozi ambao kabla ya kustaafu waliyaongoza mataifa yao vizuri, jambo ambalo si kawaida Afrika.
Hakika vigezo hivi vimeendelea kuwabwaga hata viongozi wetu wa Tanzania ambao kwa miaka mingi tangu kupata uhuru wamekuwa wakijinadi kuwa wanaongoza kwa kufuata misingi ya Sheria na Utawala Bora.
Rais John Magufuli unayo sababu ya kuibuka kidedea kwa kuitwaa tuzo hii kwa mara ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki, endapo utazingatia vigezo husika.
Kiusalama, majeshi yetu yamejitahidi kwani mipaka iko salama na vitendo vya ujambazi vimepungua. Lakini Je, vipi migogoro kati ya wakulima na wafugaji? Je, watu wanaojichukulia sheria mikononi? Je , ukatili dhidi ya watoto na wenye ulemavu wa ngozi?
Kwa upande wa afya Serikali inajitahidi lakini jambo la kujiuliza ni Je, watu wenye kipato duni hawawezi kupoteza maisha kwa kushindwa kugharimia matibabu? Je, hospitali za Serikali zina dawa za uhakika? Je, maeneo ya vijijini vituo vya afya vinatosha?
Elimu inapewa kipaumbele na Serikali kwani kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne hakuna kulipa ada. Lakini hizi shule za Serikali zina sifa ya kumfanya mhitimu kujitambua? Na kama ni ndiyo, mbona wananchi wengi wakiwamo watawala hupenda kupeleka watoto wao shule binafsi?
Maendeleo ya kiuchumi kwa mantiki ya viwanda kuna safari ya matumaini, lakini Je, vipi wakulima huko vijijini ambao wengi wao hutegemea matrekta ya kutumia damu tena bila msaada wa uhakika wa maafisa ugani, miundombinu ya umwagiliaji huku wakihimizwa kulima ili wasife njaa hata kama kuna ukame wa muda mrefu?
Je, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wafuasi wao wanapewa haki zao za kisiasa kama vile kukusanyika? Je, waandishi wa habari na vyombo vya habari ni sauti ya wasio na sauti?
Kwa muda mrefu Serikali yetu ya Muungano imekuwa na utamaduni mzuri wa viongozi kukabidhiana madaraka japo ni ndani ya CCM tu, lakini Je, kwa upande wa Zanzibar ambapo pameendelea kuwapo manung’uniko kwamba kuna hujuma za kisiasa haliwezi kuwa doa?
Wafaransa wana msemo usemao: ‘‘Vouloir c’est Pouvoir’’ tafsiri yake ikiwa ‘‘Kutaka ni Kuweza.’’ Naamini Rais wetu mpendwa Magufuli ukitaka utaweza na hatimaye baada ya kustaafu utaibeba tuzo ya MO IBRAHIM.