27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

KARIBU DK. MWAKYEMBE, LAKINI TUMEJERUHIWA!

KWAKO Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Salaam!

Sina hakika kama natakiwa kuanza kukupongeza kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ama kama natakiwa kukupa pole.  Pengine nivifanye vyote viwili:

Naomba nianze kukupongeza sana kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kuendelea kuwapo kwenye baraza lake la mawaziri. Mpo wateule wachache ambao mnaitwa mawaziri na kuona kwamba umeendelea kuwapo kwa zaidi ya mwaka mmoja, ni jambo ambalo pengine unahitaji pongezi.

Nakupongeza pia kutokana na ukweli kwamba kabla ya uteuzi huo, ulianguka kidogo katika wizara uliyokuwa ukiiongoza awali, Wizara ya Sheria na Katiba.  Wiki chache tu zilizopita ulitoa amri ambayo iliibua maswali mengi, baada ya kusema kwamba wale wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa, hawataruhusiwa kufunga ndoa.

Ulianguka kidogo kwa sababu siku iliyofuata, Rais wako, bosi wako, aliitengua amri yako hiyo na kueleza “kushangazwa” na kauli uliyokuwa umeitoa.  Alieleza kwamba amri yako inawanyima Watanzania haki yao ya msingi ya kufunga ndoa, kutokana na ukweli kwamba suala la vyeti vya kuzaliwa bado ni changamoto.

Ulianguka pia baada ya kuweka wazi msimamo wako kupinga kitendo cha Mwanasheria Tundu Lissu kugombea kiti cha urais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS).  Msimamo wako ulishangaza pia, kwani ulifikia hatua ya kutishia kuifuta TLS endapo ingechagua “mwanasiasa” hasa ikifahamika kwamba licha ya Tundu Lissu kuwa mwanasheria machachari ambaye huwapa mawakili wa Serikali wakati mgumu kwenye kesi zilizo dhidi yake, bado pia ni mwanasiasa machachari sana kutoka kambi ya upinzani.

Bila kujua, Mheshimiwa Mwakyembe, ulimpigia Mheshimiwa Lissu kampeni kubwa sana iliyofanikisha kuchaguliwa kwake kwa kishindo.  Kutokana na kuandamwa kwake, kufunguliwa kesi zingine za ghafla, kujaribu kuzuiwa kwenda kwenye uchaguzi Arusha na kutishia kuifuta TLS endapo ingemchagua, ilikuwa ni kampeni moja kubwa sana ambayo ilisababisha wanasheria, kwa umoja wao, kuamua kumpa kura ili kuonyesha kwamba hawaendeshwi kwa matakwa ya Serikali.

Kutokana na tunavyofahamu Rais wetu Mheshimiwa John Magufuli asivyopenda kushindwa namna hiyo, tulikuwa tukisubiri kuona kama utaendelea kuwapo kwenye baraza lake la mawaziri.  Alifanya mabadiliko na akakuhamishia Wizara ya Habari, unastahili pongezi.

Mheshimiwa Mwakyembe, unafahamu kwamba umeletwa kwenye wizara iliyokuwa ikiongozwa na Waziri kijana Nape Nnauye.  Huyu bwana hayumo tena kwenye baraza la Mheshimiwa Rais na kuondoka kwake kunahusishwa na msimamo wake wa kutetea uhuru wa habari.  Alipoondoka, asilimia kubwa ya watu tulisikitika na kumuona kuwa shujaa.  Alipoondoka, si kila mtu alifurahia uteuzi wako, kutokana na ukweli kwamba ghafla Nape alijizolea sifa.  Hii ndio sababu inayonifanya pia nikupe pole.

Nalazimika kukupa pole, Mheshimiwa Mwakyembe, kutokana na uteuzi wako katika wizara hii kuwa wa “masharti”.  Wakati akikuapisha, Rais alikuagiza kwenda kudhibiti wamiliki wa vyombo vya habari kutokana na aliyetoka kutokuwa mkali sana kwao.  Wakati akikuapisha, Rais aliagiza ukafanye kazi na alifikia hata hatua ya kuwaonya wamiliki wa vyombo vya habari kutokana na aina ya habari na picha zilizokuwa zinawekwa kwenye kurasa za mbele za magazeti.  Aliwatishia na kuwaambia wajiangalie.

Mheshimiwa Mwakyembe, wewe ni Mwanahabari.  Hata hivyo, unafahamu fika, kama tunavyofahamu sisi, kwamba umeletwa kwenye wizara hiyo kwa ajili ya ‘kutunyoosha’.  Sina hakika mpango mkakati wako ni upi, lakini naona kama umewekwa mahala pagumu sana, wazungu wanapopaita ‘between a rock and a hard place’.

Kama Mwanataaluma wa tasnia ya habari na mwanasheria nguli, nina imani kwamba shabaha yako ni kuona Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafuatwa, hasa tukizingatia Ibara ya 18 (1) na (2) ambazo zinatoa haki ya mtu kutoa taarifa, na pia haki ya watu kupata taarifa. 

Kwa upande mwingine, wewe ni waziri na mwanasiasa.  Rais wa nchi ni bosi wako na analoagiza linatakiwa kutekelezwa.  Unatakiwa umfurahishe kwa kuonyesha matokeo kwa yale yote anayoyatolea amri, kwani pasina kufanya hivyo, utakuwa umekiuka maagizo na kustahili kutumbuliwa.

Mheshimiwa Mwakyembe, nadhani hadi hapo umenielewa.  Karibu sana kwenye wizara yetu, lakini ujue kwamba tumejeruhiwa na tunahitaji faraja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles