25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CHOZI LA PLUIJM LINAVYOMTAFUNA LWANDAMINA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SLAAM


PENGINE yule  aliyesema uwezo wa kufundisha wa aliyekuwa kocha na Mkurugenzi wa benchi la ufundi  la timu ya Yanga, Han van Pluijm, ni mkubwa kulinganisha na kocha wa sasa wa timu hiyo, George Lwandamina, hakukosea na  labda angesikilizwa kabla ya kupuuzwa.

Kuna udhaifu mkubwa katika kikosi cha Yanga hasa viwango vya wachezaji tangu Lwandamina achukue kijiti cha kocha Pluijm, ambaye hivi karibuni klabu hiyo ilimtimua rasmi akiwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi.

Matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Zanaco  katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa juzi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam yalikuwa ni mwendelezo wa  matokeo ya ovyo ya michezo iliyopita, ikiwamo ule dhidi ya Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC na michezo mingine.

Hakukua na sababu yoyote ya Yanga kupata sare dhidi ya Zanaco ambayo itaifanya timu hiyo ilazimike kutafuta ushindi katika uwanja wa ugenini kama inataka kufuzu hatua ya makundi.

Makosa yaliyofanywa katika mchezo huo ni yale yaliyoitokea Yanga katika michezo iliyopita, hasa mabadiliko ya Thaban Kamusoko, makosa ya kizembe ya Justine Zulu, udhaifu wa namba sita anayocheza sasa Kelvin Yondan ambayo wakati mwingine humzidi uwezo.

Watu hao watatu hata kabla ya kutolewa, walisababisha katikati kukosa mgawanyo wa majukumu, nani mwenye majukumu gani kwa wakati upi na mwingine afanye nini, mwisho wa siku wakajikuta wakifanya majukumu yanayofanana kwa wakati mmoja.

Yondani na wenzake walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kujikuta wakishindwa kumpata mtu sahihi mwenye kazi ya kupokonya mipira na kufanya vurugu ili kuwafanya Zanaco wasicheze kwa uhuru, mwingine kuchukua mipira iliyopokonywa na kupiga pasi nzuri kwa wachezaji wa mbele.

Matokeo yake wakatoa mwanya kwa Zanaco kutawala mchezo na kuwashambulia sana Yanga, ambao mara nyingi walikuwa wakiwazuia Zanaco ambao walikuwa ugenini.

Ukiachilia mbali uzembe huo na ule uliofanywa na Emmanuel Martin wa kukosa mabao ya wazi ndani ya 18 kutokana na uwezo wa chini wa kufunga mabao, umakini wa safu ya ushambuliaji wa Yanga ni tatizo kubwa kwa sasa.

 

Mbali na mambo mengine, Yanga kwa sasa ina tatizo la kiufundi ndani ya uwanja ambalo linafanya kuwa tofauti na ile iliyokuwa chini ya Pluijm.

Tatizo kubwa ni uwezo wa kocha kuusoma mchezo na kufanya mabadiliko, pia kuwaamini baadhi ya wachezaji katika michezo iliyowazidi uwezo wao.

Kushindwa kutambua umuhimu wa mchezo na namna ya kujipanga kupambana na adui, kushuka ari na hamasa ya wachezaji wenyewe pia lilikuwa tatizo.

Kwa ujumla hilo ndilo lililojitokeza katika michezo yote ambayo Yanga imeshindwa kupata matokeo, tukianzia Kombe la Mapinduzi Zanzibar ambapo walishuhudiwa Wanajangwani hao wakipoteza katika michezo yote waliyocheza na timu kubwa za Simba na Azam FC.

Mwelekeo wa Lwandamina kwa sasa ni dhahiri ameshindwa kuvaa viatu vya mtangulizi wake Pluijm, kutokana na ukubwa wake na endapo hali hiyo itaendelea kuwa hivi kama asipokifanyia marekebisho kikosi chake, huenda Yanga ikawa mbaya zaidi  msimu ujao.

Mchambuzi wa soka, Kenned Mwaisabula, alizungumza na MTANZANIA juu ya mchezo huo ambapo alisema baadhi ya viungo wa katikati wa Yanga hawana sifa ya kucheza eneo hilo.

“Ukimwondoa Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko, Yanga hawana viungo wengine wenye sifa ya kuitwa viungo eneo  la katikati.

“Siku hizi mpira unachezwa eneo la kati, kukosekana kwa  Niyonzima na Kamusoko aliyetolewa kabla ya kumalizika mchezo, kulisababisha eneo hilo kushindwa kucheza kwa nidhamu kwa kusababisha faulo na makosa ya kizembe,” alisema Mwaisabula.

Mchambuzi huyo alisema endapo Yanga watafanya maboresho katika eneo hilo, wanaweza kufanya vizuri katika mchezo wao wa marudiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles