23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CCM IMEPOTEZA UWEZO WA KUONA PICHA KUBWA YA MUSTAKABALI WA TAIFA

TAIFA letu lilipopata uhuru takribani miaka 55 iliyopita, viongozi wetu walioongoza mapambano ya kudai uhuru wakiongozwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, walionyesha dira ya uongozi na matarajio yao kuwa Tanganyika na baadaye Tanzania liwe taifa la namna gani.

Waasisi wetu hao walitamani taifa letu liwe la kijamaa ambapo njia kuu za uchumi zinamilikiwa na dola kwa manufaa ya watu wote.

Ili kufikia ndoto ya taifa la ujamaa ilibidi viongozi wetu waweke nguzo za kuligeuza taifa letu kuwa la kijamaa na moja ya nguzo hizo ni pamoja na uongozi bora, siasa safi, watu na ardhi. 

Kwa sababu viongozi wetu waliamini kuwa taifa la ujamaa haliwezekani kama dola haitajishughulisha na ustawi wa watu ipasavyo. Hii ndiyo sababu mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu maendeleo, haukuwa juu ya maendeleo ya vitu bali ni maendeleo ya watu. 

Hivyo basi, ili kuwaletea watu maendeleo sharti kuwepo na viongozi bora. Hapa ndipo ambapo vyeo vya hawa viongozi ndani ya dola vinageuka kuwa ni dhamana tu ya kuwaletea watu maendeleo na vyeo hivyo si zawadi kwa viongozi.

Kiongozi anayetambua kuwa cheo chake si mali yake binafsi isipokuwa ni nafasi ya yeye kuwajibika, katu kiongozi huyo hawezi kuiacha misingi ya ujenzi wa taifa.

Miaka 55 iliyopita imekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuongozi na kisiasa kwa maana ya namna ya kuendesha serikali ili dhima ya dola kustawisha maisha ya watu itimie.

Mabadiliko hayo yamepelekea dira ya taifa kuyumba na taifa kukosa mwelekeo wa kifalsafa, jambo lililosababisha misingi ya ujamaa ambayo ni udugu, umoja na uhuru kuingiliwa na virusi vya itikadi za kisiasa. 

Ujamaa ungefanikiwa endapo taifa lingeendelea na mfumo wa siasa za chama dola chama kimoja cha siasa, lakini baada ya kuwa na mfumo wa vyama vingi mashindano yamekuwa si tena kujenga fikra kubwa juu ya wapi na nini ndiyo iwe falsafa ya kiuongozi kwa taifa letu, bali mashindano yamekuwa ni kuzuia kwa udi na uvumba dola isikamatwe na Watanzania wenye itikadi tofauti na ile ya waasisi wa taifa.

Mashindano kati ya CCM na vyama vya upinzani juu ya kuishika na kuongoza dola yamepofusha kabisa fikra kubwa juu ya picha kubwa ya tunataka taifa la namna gani.

Kumekosekana mwafaka wa kitaifa juu ya aina ya Taifa tunalolijenga, ndiyo sababu kiongozi asiyejua cheo ni dhamana anaweza kudiriki kutumia cheo chake kuwanyanyasa wapinzani wasiokuwa na itikadi moja naye.

CCM ni chama kikongwe na kwa uzee wake bila shaka kimechoka kuiongoza dola, hivyo kinatumia kila juhudi kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kuishika dola.

Juhudi hizi za CCM kutamani kuendelea kuishika dola kunaifanya ikose muda maridhawa wa kuiona ‘picha kubwa’ ya mustakabali wa taifa, badala yake inamwona kila mtu anayetaka kuishika dola ili kufafanua ‘picha kubwa’ ya mustakabali wa taifa kuwa adui yake anayestahili kudidimizwa. 

Kwa kawaida ni kazi ngumu kuiona picha kubwa ya ujenzi wa taifa ukiwa ndani ya CCM, kwa sababu utashiriki juhudi za CCM kuendelea kuishikilia dola. Wanasiasa waliowahi kuwa CCM na wakatoka nje wao hufanikiwa kuiona picha kubwa ya mustakabali wa taifa letu kulikoni wale waliopo ndani. 

Hii ndiyo sababu iliyomfanya Mwalimu Nyerere alipokuwa nje ya uongozi kusema anaweza kutoka nje ya CCM kwa kuwa CCM si mama yake wala  baba yake, kauli ambayo Waziri wa zamani, Edward Lowassa, aliirudia mwaka 2015 alipotoka nje ya CCM.

Sasa kama taifa tunatokaje kwenye mkwamo unaosababishwa na CCM wa kutoiona picha kubwa ya mustakabali wa taifa? Njia salama ni ile ya Watanzania kuamua kuwa tunataka sasa kuondokana na mkwamo huo na kuiangusha ngome inayozuia picha kubwa isionekane kwa ajili ya taifa. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles