26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

RAIS MBABE WA MAREKANI NDIYE ANAYEHUSUDIWA DUNIANI

INAVYOELEKEA Rais wa Marekani akikosa hulka ya ubabe anapoteza mvuto duniani, kwani hata Rais anayeahidi wakati wa kampeni kutotumia ubabe kushambulia mataifa mengine, hubadilika na kufanya ubabe utakaoungwa mkono na wengi dhidi ya wachache miongoni mwa mataifa mengine.

Ndicho kilichotokea baada ya shambulizi la hivi karibuni la makombora 59 ya Tomahawk lililofanywa na Marekani dhidi ya kambi ya Shayrat ya jeshi la anga nchini Syria, iliyoko katika mji wa Homs.

Marekani iliyojivika upolisi wa dunia, ilipeleleza kwa muda mfupi kisha ikajigeuza jaji kuhukumu kuwa shambulizi la silaha za sumu katika mji wa Khan Sheikum lilifanywa na vikosi vya jeshi la Serikali ya Syria.

Raia tisa waliuawa katika shambulizi la Marekani, wakiwamo watoto wanne wasiohusika na vita, kimsingi Marekani imeua raia katika kutetea raia 87 waliouawa kwa kuunguzwa na silaha za sumu katika nchi ambayo haiko chini ya utawala wake.

Usingetarajia Syria inyamaze, licha ya kutoweza kutoshana ubavu na Marekani kwa kuwa wanaitegemea sana Urusi hata katika vita dhidi ya waasi wanaotaka kuipindua serikali.

Bashar al-Assad ambaye mataifa ya Magharibi yanatamani sana kumuona aking’oka madarakani, alitaharuki kwa shambulizi hilo, akadai kuwa Marekani inaugua ‘myopia’ ya kisiasa kwa kutouona ukweli, ikikabiliwa na upofu wa uhalisia kwamba shambulizi hilo linawachagiza kuwashambulia zaidi waasi.

Adui yako muombee njaa ili ashindwe kukabiliana nawe, kwani waasi wanaopambana na Serikali ya Syria wamefurahia shambulizi hilo wakitaka kambi nyingine 26 zinazotumika kupiga raia zibutuliwe ili kuzuia udhalimu wa Rais Assad.

Shambulizi hilo lililoidhinishwa na Rais Trump, lina matokeo kadhaa kutegemeana na kila upande utakavyochukua hatua, kwanza uhusiano baina ya Urusi na Marekani kwa dhana ambazo hazijaweza kuthibitishwa kwamba Putin aliagiza kudukuliwa uchaguzi wa Marekani ili kumfanikisha Trump kushinda, ili kusawazisha mbinyo iliyofanyiwa na Obama wa kuidhoofisha kiuchumi kupitia mafuta zimetatanika, hali inayoweza kutulia au kuelekea kubaya zaidi na kuiyumbisha dunia nzima.

Urusi imekasirishwa na ilichofanya Marekani na kuishutumu kwa kutafuta kisingizio cha kuishambulia nchi huru, kwamba uhusiano baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu za kijeshi utaharibika hata ushirikiano dhidi ya magaidi nchini Syria utakoma.

Lakini kinachotisha zaidi ni hulka mpya ya Rais Trump, ambaye ghafla amegeuka shujaa hata nchini mwake, ambako teuzi zake, amri zake na miswada yake kadhaa imekwamishwa.

Ikumbukwe chama anachotoka Trump cha Republican ndicho kinaongoza kwa marais wababe zaidi wa Marekani wanaohusudu vita bila ithibati endelevu, kama ilivyotokea katika mapigano yaliyomwondoa Rais Saddam Hussein madarakani nchini Iraq na kusababisha kuyumba kwa uchumi wa dunia kwa athari ya mafuta ghafi.

Madai ya Trump kuidhinisha shambulizi hilo baada ya kushuhudia athari za silaha za sumu za utawala wa Assad kwa raia wanaoishi katika mji wa Idlib, yamekuja mapema bila uthibitisho, kwani kuna madai mengine kuwa shambulizi hilo la silaha za sumu lilifanywa na waasi waliozinunua Iraq na Uturuki na kuzihifadhi miongoni mwa makazi ya raia na kulichongea Jeshi la Syria, ambalo hivi karibuni limefanikiwa kuwavurumisha wapinzani na kuurudisha mji wa Aleppo mikononi mwake.

Lakini mchezo mzima ni sawa na satarani (chess) inayochezwa na Marekani na Urusi, huku ubao wa kuchezea ikiwa nchi ya Syria na kete zenyewe ni raia, waasi na majeshi ya serikali.

Wakati Marekani ikidai kuwa matumizi ya silaha za sumu ni kushindwa kwa usimamizi wa uteketezaji wa silaha za sumu za Syria kwa makubaliano ya mwaka 2013 yaliyosimamiwa na Urusi, lakini hasimu wake, Urusi naye ametangaza kuisaidia Syria kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya anga.

Dunia ijiandae endapo mzozo huo utashindwa kudhibitiwa kwa kuwa maswahiba wa Marekani, zikiwamo Uingereza, Australia, Israel, Saudi Arabia, Italy, Japan, NATO, Jordan, Uturuki, Ujerumani, Ufaransa, Czech na Ufaransa zinaunga mkono kilichofanywa na Marekani.

Lakini kuna mataifa yasiyokubaliana na ilichofanya Marekani yanayopinga vikali, wakiwamo maswahiba wa Syria, wakiongozwa na Urusi, wakifuatiwa na Iran na China, lakini matamshi makali zaidi yametolewa na Korea Kaskazini, kwamba kama kuipiga Syria ni mkwara dhidi yake, haitishiki, iko tayari kukabili vitisho vya Marekani.

Lakini kama ni sinema ndiyo kwanza inaanza, kwani licha ya kambi hiyo kushambuliwa na ndege za vita 20 kuteketezwa, ilikarabatiwa kwa haraka na ndege vita nyingine ziliruka kutoka hapo kwenda kufanya mashambulizi dhidi ya waasi.

Marekani inadai haikuwa inatingisha kibiriti, kwamba ikiwezekana na ikibidi itafanya mashambulizi mengine, huku Trump akijinadi kwamba anaweza kubadili msimamo wake wakati wowote na kuishambulia Syria ili kuwalinda raia wasio na hatia. Kwamba yeye si Obama aliyedai awali kwamba Assad lazima ang’oke, lakini akamlegezea kamba, ingawa kumng’oa Rais huyo haielekei kuwa kazi rahisi kwa kuwa vita hiyo iliyoanza kwa vuguvugu la maandamano haielekei kwisha, licha ya kupiganwa kwa miaka sita.

Hali isipodhibitika, kuna hatari dunia ikashuhudia ubabe wa Rais wa Marekani ukiitumbukiza katika vita itakayovuruga utangamano itakayoathiri wote wanaohusika na wasiohusika nayo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles