23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BAA LA NJAA: UKO WAPI UMOJA WA AFRIKA?

KATIKA nusu ya kwanza ya miaka ya 1980, Ethiopia ilikumbwa na baa kubwa zaidi la njaa katika historia ya taifa hilo na pengine Afrika, ambalo liliteketeza mamia kwa maelfu ya watu.

Si serikali ya Ethiopia wala mataifa ya Afrika yaliyoitikia kwa nguvu suala hilo katika kuunganisha nguvu na mikakati ya kulitatua.

Bali historia inayakumbuka zaidi mataifa ya magharibi na mashariki pamoja na wanaharakati wengine akiwamo mwimbaji maarufu wa Uingereza Bob Geldof.

Geldof kwa mfano aliendesha matamasha mbalimbali ikiwamo kutunga nyimbo ambazo pato lililotokana nazo lilienda kusaidia waathirika wa baa hilo.

Aidha, mwaka 2005 yalikuwa mataifa tajiri yaliyoendelea kiviwanda yaiitwayo G 7 yaliyoanzisha kampeni ya ‘kuufanya umasikini barani Afrika kuwa historia’ zikiongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.

Katika harakati hizo, mwanamuziki Geldof pia alishiriki maandamano na matamasha makubwa yalifanyika katika majiji mbalimbali makubwa duniani katika mataifa kama vile Uingereza, Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Norway na kwingineko kuunga mkono kampeni hizo.

Harakati hizo pamoja na mambo mengine zililenga kuongeza misaada muhimu ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuyapunguzia madeni mataifa masikini duniani ili badala yake madeni hayo yasaidie huduma za afya, elimu katika nchi hizo daiwa.

Wakati hilo likiwa jambo zuri kwa kiasi chake kwa Afrika, mataifa ya Afrika yenyewe yalitia aibu kwa kushindwa kuwa mfano au mstari wa mbele kuitikia majanga hayo na kama mwitikio ulikuwapo basi mdogo.

Badala yake daima yamekuwa yakisubiri kubuniwa kampeni na mikakati kuhusu majanga yanayowahusu kutoka nje ya bara.

Tatizo hilo limejionesha katika changamoto kubwa zinazokabili baadhi ya nchi kipindi hiki hususani baa la njaa kiasi kwamba jumuiya ya kimataifa inazishangaa mamlaka za Afrika.

Hakika, ugaidi, vita, rushwa, ukame, mavuno hafifu, umasikini ni baadhi ya majanga yanayozidi kuyakabili nchi nyingi hususani za Afrika.

Umoja wa Mataifa unazizungumzia kama janga kubwa kabisa la kibinadamu tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia.

Kwa sasa mamilioni ya watu wanakabiliwa na kitisho cha njaa na hali ni mbaya hasa katika mataifa ya Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na kanda ya Ziwa Chad.

Mashirika ya misaada yanaomba ufadhili zaidi huku Jumuiya ya kimataifa ikiwa imeshtushwa, lakini imeweza kupata sehemu ndogo tu ya misaada iliyoahidiwa na mataifa yaliyostawi kiviwanda.

Lakini kama tulivyoona katika utangulizi hapo juu, si Afrika inayoonekana kugangamala katika kusaka suluhu ya dharura ya matatizo haya.

Mshikamano kati ya mataifa ya Afrika kuhusiana na janga hilo hauonekani, licha ya ukweli kwamba Umoja wa Afrika (AU) huitisha vikao vya kujadili na baadhi ya mataifa yakifanya kila liwezekanalo.

Mwakilishi wa Uingereza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), Matthew Rycroft ana picha kamili ya njaa baada ya kuzitembelea Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia na maeneo yanayozunguka Ziwa Chad.

Katika eneo la Ziwa Chad, kundi la kigaidi la Boko Haram limekuwa likiendesha harakati zake kwa miaka kadhaa kati ya mataifa ya Nigeria, Niger, Cameroon na Chad.

Maelfu ya watu wameuawa, kutekwa na vijiji vyao kuangamizwa huku ukame ukiongeza ukubwa wa matatizo katika maeneo hayo, kwa mujibu wa Rycroft.

"Kulikuwapo swali la iwapo mgogoro huu wa kibinadamu umetiwa chumvi. Mimi sidhani hivyo, tumejionea wenyewe hali inavyozidi kuwa mbaya huku mwitikio ukiwa si mzuri," anasema Rycroft.

Picha za wakimbizi waliokondeana tayari zinazunguka duniani, na Rycroft anafahamu kuwa anapaswa kufanya kila linalowezekana ili jumuiya ya kimataifa iguswe kwa uzito ule ule alioshuhudia kwa vile kuna kitisho kwa jumuiya hiyo kushindwa tena.

Lakini pia anapaswa kuzungumza kwa lugha bayana na washirika wake wa Kiafrika, hata kama matamshi yake yake atayavisha joho la kidiplomasia.

"Haihusu tu uitikiaji wa kimataifa, bali pia wa kitaifa, na ndiyo maana tumekuwa tukiihamasisha Serikali ya Nigeria, na serikali nyingine tulizozitembelea kuhakikisha hata wao wanaimarisha uitikiaji wao kama taifa moja moja na kwa pamoja pia.

“Tumesikia mambo mazuri na sasa tunataka kuona utekelezaji kamili wa ahadi hizo," anafafanua balozi huyo wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa.

Tafsiri ya hii ni kwamba: Ni zamu yenu sasa (Afrika). Hata hivyo Serikali ya taifa tajiri kwa mafuta la Nigeria imeahidi kutenga kiasi cha dola bilioni moja, hata kama hakuna pesa zilizoanza kutolewa mpaka sasa. Lakini madai ya ukosefu wa fedha si tatizo pekee katika mapambano dhidi ya njaa, anasema Omolola Adele-Oso kutoka shirika la Act4Accountability.

“Kwa sababu pia kuna rushwa. Nchini Nigeria kwa mfano, tumeona picha za mchele ukipakiwa tena katika magunia mapya na kuuzwa tena, kwa hiyo tuna chakula kinachopelekwa mahala kisipotakiwa kwenda.

Ni jambo la aibu na lisilokubalika,” anasema Waziri wa Maendeleo ya Ujerumani, Gerd Müller na kuongeza kwamba dunia inachukua hatua kwa kujikongoja.

Lakini jambo la kufedhehesha ni kukosekana kwa mshikamano miongoni mwa Waafrika wenyewe, anasema Moussa Faki Mahamat – mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika.

"Kitisho cha njaa kinachoikumba sehemu kubwa ya Afrika ni aibu kubwa kwetu. Uwezo mkubwa wa bara letu na ukuaji wa kiuchumi wa mataifa kadhaa wanachama wa Umoja wa Afrika vinatupokonya hoja za kuendelea kulitazama tu janga hili baya,” anasema.

Hali inazidi kuwa mbaya katika baadhi ya mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika kama vile Somalia ambako sehemu kubwa ya nchi hiyo inadhibitiwa na kundi la itikadi kali la Al-Shabaab, au Sudan Kusini, ambako serikali na waasi wanashiriki mapigano yanayowagharimu zaidi raia.

Ni nchi chache tu za Afrika zinazowajibika. Uganda inachukua wakimbizi kutoka Sudan Kusini, na Ethiopia inafanya kila iwezalo kuwasaidia waathirika wa njaa kutoka nchi jirani ya Somalia.

Ethiopia na Uganda zinategemea misaada ili kuendelea kutoa msaada huo. Lakini maombi ya ndani kwa ndani barani Afrika husikika kwa nadra.

Umoja wa Afrika unashughulikia tu migogoro midogo midogo na umetenga mfuko wa dola 200,000  tu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaokabiliwa na utapiamlo, na umeitaka jumuiya ya kimataifa kuendeleza utoaji wa misaada.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa mtandao hasa DW.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles