30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAUZA UNGA NI WATU WEMA KWENYE JAMII ZAO

Luqman Maloto


WAUZA unga wana mbinu nyingi za kufukia alama (footage) ili wasibainike katika mizunguko yao ya kibiashara. Wanajua jinsi ya kucheza na akili za wapelelezi wa serikali mbalimbali. Inawezekana kuwa na taarifa nyingi kumhusu lakini kumtia hatiani ni shughuli pevu.

Hii ndiyo sababu wauza unga wengi wakubwa hawakamatwi na wanakuwa mpaka walezi wa serikali na hata viongozi. Wanatoa misaada mno. Ni watu wema kweli kwenye jamii zao kwa kuwaangalia kwa macho ya kawaida ila ni katili mno ukiwaingilia kwenye anga zao.

Christopher Coke ‘Dudus’ raia wa Jamaica na kiongozi wa genge la Shower Posse, alionekana mtu mwema kwa watu kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumgusa. Polisi wa Jamaica walishindwa kumfanya chochote maana haikuwa rahisi kumbaini, ilibidi Marekani watumie nguvu kuingia Jamaica na kumkamata wenyewe.

Dudus alilindwa mno na Serikali ya Jamaica. Haikuwa rahisi kuingia ndani ya nchi hiyo kumkamata, maana kwa macho ya wengi, Dudus alikuwa raia mwema na mfadhili mkubwa wa jamii na wanasiasa. Tuhuma zote za kuhusika na dawa za kulevya zilionekana za kutunga.

Alipokuwa na umri wa miaka 23 tu, tayari Dudus kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha aliokuwa nao, aliweza kuwa kiongozi wa kijamii katika Mji wa Tivoli Gardens, uliopo Magharibi ya Kingston, Jamaica.

Ndani ya Mji wa Tivoli Gardens, Dudus alisifika kwa kugawa fedha kwa watu maskini. Kila familia maskini aliifikia na kuipa msaada. Dudus alitengeneza ajira nyingi kwa jamii ya watu wa Tivoli Gardens na Kingston kwa jumla. Hiyo ndiyo sababu alipendwa mno na watu.

Dudus aliweza vipi kupata utajiri mkubwa katika umri mdogo? Jawabu la swali hilo limenyooka kabisa. Ni kwamba Dudus alirithi utajiri kutoka kwa baba yake, Lester Coke ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Jim Brown, aliyetengeneza ngome kubwa ya kusafirisha bangi kutoka Jamaica kwenda Marekani. Jim Brown ndiye mwasisi wa Shower Posse.

Akiwa mdogo, Dudus na ndugu zake, walisoma shule za kitajiri kwa sababu ya jeuri ya fedha aliyokuwa nayo baba yao. Walipokua, waliingia kwenye genge la baba yao, hivyo kusababisha kifo cha dada yake, mwaka 1987. Dada yake Dudus aliuawa katika fujo za makundi ya wauza dawa za kulevya.

Mwaka 1992, baada ya baba yake Dudus kufariki dunia, Dudus alichukua uongozi wa genge la Shower Posse ambalo liliasisiwa na baba yake. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 23 tu, alikuwa kijana mdogo lakini mwenye fedha nyingi na nguvu kubwa.

Kila alipotembea alilindwa na kikosi cha usalama cha Shower Posse. Alikuwa na mashushushu ambao walifanya kazi ya kuchunguza na kumpa taarifa zote kuhusu yeye binafsi, genge lake na biashara ya unga kwa jumla.

Mdogo wake Dudus (wa kiume), alifariki dunia mwaka 2004 katika vurugu nyingine za mapambano kwenye magenge ya mihadarati, hivyo kumfanya Dudus abaki peke yake katika familia yao.   

Mwaka 2009, Marekani waliiarifu Jamaica kuwa wanamhitaji Dudus kwa kuhusika kwake kusafirisha bangi na cocaine kuingia Marekani. Hata hivyo, Serikali ya Jamaica iligoma kabisa kumruhusu Dudus kutoka.

Sababu ni kuwa Dudus alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye Bunge, vilevile chama tawala na Serikali kwa jumla. Dudus anatajwa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na chama cha siasa cha Jamaica Labour Party (JLP), ambacho hivi sasa ndiyo kinachoongoza Serikali ya Jamaica.

Waziri Mkuu wa Jamaica, Bruce Golding, ambaye alikuwa Waziri wa Bunge, akitokea Wilaya ya Tivoli Gardens, alihoji uhalali wa kisheria wa Marekani kumtaka Dudus, bila kuwa na hati ya kimataifa.

Golding alisema pia kuwa Marekani wamekuwa wakiingia Jamaica bila idhini na kufanya upelelezi, hivyo akataka Serikali ihakikishe inazuia jitihada zozote za Marekani kutaka kumkamata Dudus ili kuifundisha wakati mwingine kuheshimu mataifa mengine.

MVUTANO WA KISIASA

Ulitokea mvutano mkubwa katika suala la Marekani kumchukua Dudus, wanasiasa wa chama hasimu na JLP cha People's National Party (PNP), walipaza sauti kuwa JLP ni chama kinachoendeshwa na genge la Shower Posse, ndiyo maana Golding na wenzake waliapa kumlinda Dudus.

Baada ya mzozo mkubwa, Mei 17, 2010, Serikali ya Jamaica ilikubali kumkamata Dudus na kumkabidhi kwa Marekani ili akayakabili mashtaka ya kuingiza bangi na cocaine kwa zaidi ya miongo miwili nchini humo.

Hata hivyo, hati ya kumkamata ilitolewa lakini kumkamata ilikuwa vigumu. Maofisa wa Marekani hawakuweza kupenya ndani ya Wilaya ya Tivoli Garden na kumkamata kwa sababu ulinzi ulikuwa mkubwa na jamii yote iliyomzunguka ilimwamini na kujitolea kumlinda.

Baadaye Marekani waliona kuwa Serikali ya Jamaica haikuwa tayari kumtoa Dudus, kwani pamoja na ugumu wa kumfikia Tivoli Gardens, pia alikuwa na uwezo wa kusafiri maeneo mengine hata nje ya Jiji la Kingston na kufanya shughuli zake kisha kurejea Tivoli Gardens salama, tena akilindwa.

Marekani ilipojiridhisha kuwa Serikali ya Jamaica ilikuwa haina dhamira ya kumtoa Dudus, ilibidi makachero wake wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DEA), waanze kumfuatilia wenyewe na kumtega akiwa nje ya Tivoli Gardens, maana ndani ya Tivoli Gardens yote na Kingston kwa jumla, ilikuwa ngumu kumkamata.

Juni 22, 2010, Dudus akijua askari wa Jamaica hawawezi kumkamata kutokana na mkono mrefu aliokuwa nao serikalini, alifanya mizunguko yake nje ya Kingston, bila kujua kuwa intelijensia ya Marekani, kupitia kikosi cha DEA, walikuwa wanamfuatilia.

DEA walikuwa wametega ushushushu wao nje ya Kingston, hivyo ilikuwa rahisi kwao kutambua kuwa Dudus alikuwa nje ya Kingston. Baada ya hapo walimfuatilia na kumzunguka kabla ya kumkamata na kumsafirisha mpaka Marekani bila kuishirikisha Serikali ya Jamaica.

 

MAANDAMANO YA WANANCHI

Kitendo cha Dudus kukamatwa, kiliamsha hisia na hasira kwa wananchi wa Jamaica, hususan wakazi wa Tivoli Gardens, ambao waliingia mitaani na kuandamana, wakitaka Dudus aachiwe huru.

Wananchi walikuwa na mabango yaliyoandikwa kuwa Dudus ni mlinzi wa amani ndani ya Tivoli Gardens, hivyo aachiwe. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kuandika kwamba kumkamata Dudus ni sawa na alivyokamatwa Yesu kwa sababu ni mtu safi na mwenye heshima.

Hiyo ni kuonesha kuwa wananchi wa Jamaica, hasa wa wakazi wa Tivoli Gardens, walikuwa hawaambiwi kitu kuhusu Dudus. Tuhuma zote za kuhusika na dawa za kulevya, waliona ni uzushi na alikuwa anaonewa kwa wivu wa Wamarekani na Serikali yao.

Ijumaa ya Juni 15, 2012, Mahakama ya Kuu ya New York, ilimhukumu Dudus kifungo cha miaka 23 jela. Miaka 20 ikiwa kwa kosa la kupanga njama na kufanya biashara haramu na miaka mitatu ya kula njama za kufanya mashambulizi.

Sababu nyingine iliyofanya Dudus asakwe sana na Marekani ni kwamba pamoja na kuingiza bangi na cocaine nchini humo, vilevile alikuwa akiingiza na kuuza bunduki kinyume cha sheria, hivyo kusababisha matumizi mabaya ya silaha mitaani.

Hiyo ndiyo sababu ya kifungo cha miaka mitatu jela ya kula njama za kufanya shambulio, hivyo kutimiza jumla ya miaka 23 jela. Alianza kutumikia kifungo akiwa na umri wa miaka 43, bila shaka atatoka umri ukiwa umeyoyoma.

Sheria ya Marekani ni kufilisi mali zote za wauza dawa za kulevya pindi wanapokutwa na hatia, lakini imekuwa vigumu kumfilisi Dudus, maana uwekezaji wake wote ameufanya Jamaica ambako Serikali inamlinda.

Hata sasa, genge la Shower Posse linaendelea na kazi ya usafirishaji wa bangi, cocaine na sialaha kwenda Marekani, japokuwa bosi wao yupo jela, akitumikia adhabu yake.

Ipo hofu kuwa hata baada ya Dudus kumaliza kifungo jela, huenda Serikali ya Marekani isimwachie huru kwa sababu ya hofu kwamba atarudi kazini kwake na kuzidi kuwaangamiza Wamarekani kwa kuwauzia dawa za kulevya na silaha haramu.

 

NGUVU YA SHOWER POSSE

JLP na PNP ndiyo vyama viwili hasimu nchini Jamaica. Vyenyewe ndiyo hupishana kuongoza Serikali kutokana na matokeo ya uchaguzi yanavyokuwa. Vyote ni vyama vikubwa na vina ushindani.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamaica na kiongozi wa PNP, Michael Manley, aliibuka na kauli mbiu ya Power, kwa maana ya Nguvu, maana yake ikiwa ni Nguvu ya Watu au Nguvu ya Umma.

Hiyo kauli mbiu ya Power iliyotumiwa na Manley pamoja na PNP, ilijibiwa na JLP ambao ya kwao waliita Shower, kwa maana ya manyunyu au mvua za rasharasha. Huku Power, kule Shower. Hapa Nguvu, pale Manyunyu. Mchuano ulikuwa mkubwa kweli.

Mwasisi wa Genge la Shower Posse, Lester Coke (baba yake Dudus), kwa kuwa alikuwa mtu nyeti kwenye Chama cha JPL, aliamua kuichukua kauli mbiu ya Shower, akaongezea neno Posse, hivyo genge hilo likawa linafahamika rasmi kama Shower Posse.

Tuendelee Alhamisi ijayo, kuona nguvu ya Shower Posse iliyoitikisa Marekani na jinsi baba yake Dudus alivyouawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles