Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KOCHA msaidizi wa Azam FC, Iddy Cheche, amesema mipango waliyosuka kabla ya kukutana na Yanga juzi katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ndio imewasaidia kupata ushindi mnono dhidi ya wapinzani wao.
Katika mchezo uliochezwa juzi usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Azam walicharuka na kufanikiwa kuwanyamazisha Yanga kwa kuwafunga mabao 4-0 na kukamata usukani wa Kundi A.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Cheche alisema awali kikosi hicho kilikuwa kinapata matokeo yasiyoridhisha lakini baada ya kufanyia kazi makosa yaliyokuwa yakijitokeza wachezaji walibadilika na kuanza kuonyesha soka safi.
“Tunashukuru tumefanikiwa kupata ushindi mnono dhidi ya Yanga, mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa lakini wachezaji walipambana na kucheza kwa mipango ambayo ilisaidia kuondoka na pointi tatu muhimu,” alisema.
Alisema wamejiweka malengo ya kunyakua Kombe la Mapinduzi hivyo watacheza kwa makini katika michezo inayofuata ili kuhakikisha wanarudi na kombe hilo ambalo linashikiliwa na URA ya Uganda.
Cheche alidai kuwa mashabiki wa Azam wamekosa furaha kwa muda mrefu kutokana na timu hiyo kufanya vibaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, lakini sasa atawafurahisha kwa kupata matokeo mazuri.
Azam inaongoza katika Kundi B ikiwa imejikusanyia pointi saba baada ya kushuka dimbani mara tatu, huku Yanga ikishika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi sita.