LONDON, ENGLAND
BAADA ya nyota wa klabu ya Arsenal, Olivier Giroud, kuonesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa Kombe la FA juzi dhidi ya Preston North End, kocha wa klabu hiyo, Arsene Wenger, amedai mchezaji huyo anastahili kuwa nahodha.
Katika mchezo huo, Giroud alipewa jukumu la kuwa nahodha, hivyo Wenger amedai ni wazi mchezaji huyo alistahili kupewa uongozi katika mchezo huo kutokana na yale aliyoyafanya kwa kuibeba timu yake.
Katika mchezo huo, Arsenal ilifanikiwa kushinda mabao 2-1, mabao ambayo yalionekana kuwa ya kusuasua huku wenyeji wa mchezo huo, Preston North End, wakiwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya saba lililofungwa na Callum Robinson, lakini Arsenal walifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 46 ambalo lilifungwa na Aaron Ramsey, kabla ya nahodha wao, Giroud kuongeza katika dakika ya 86.
Kocha huyo amedai kuwa aliamua kufanya maamuzi ya kumpa uongozi Giroud katika mchezo huo kutokana na jinsi anavyojituma katika michezo yake mbalimbali ya hivi karibuni.
“Nilimchagua mchezaji huyo kuwa nahodha wa mchezo kwa kuwa napenda jukumu hilo liwe linazunguka kwa wachezaji mbalimbali. Kuna kipindi Giroud alikuwa kwenye kipindi kigumu kwa kuwa alikuwa anakosa nafasi ya kucheza.
“Lakini kwa sasa amekuwa akijituma kwa kiasi kikubwa na kutoa mchango wa kutosha katika ushindi wa baadhi ya michezo yetu, ninadhani Giroud ameonesha jinsi uongozi unavyotakiwa kufanyika,” alisema Wenger.
Kocha huyo aliongeza kwa kusema kwamba, wachezaji wote wa klabu hiyo wamekuwa na umoja sasa ambao unaweza ukaleta mabadiliko makubwa kwenye michuano mbalimbali japokuwa ushindani ni mkubwa.
“Uwanjani wachezaji ni 11, hivyo ushindi ambao unapatikana ni kutokana na umoja wao na si kwa mchezaji mmoja, kila bao lazima liwe la mipango hivyo mipango hiyo haipangwi na mchezaji mmoja ni ushirikiano wa wachezaji wengi,” aliongeza Wenger.
Michezo mingine ambayo ilipigwa juzi ni pamoja na Leicester City ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Everton, Swansea City ikipokea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Hull City, Southampton ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Norwich, huku Stoke City ikipokea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers na Bournemouth wakichezea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Millwall.