27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

LWANDAMINA: HATUJAKATA TAMAA TUNAJIPANGA UPYA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


george-lwandaminaKOCHA mkuu wa timu ya Yanga, George Lwandamina, amesema licha ya kupokea kipigo kikali kutoka kwa wapinzani wao Azam FC, bado hawajakata tamaa bali wanaendelea kupambana ili kuhakikisha wananyakua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi msimu huu.

Baada ya kupata kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Azam juzi katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar, Yanga iliyopangwa Kundi A inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita huku Azam ikiongoza kwa pointi saba.

Kocha huyo raia wa Zambia aliliambia MTANZANIA jana kuwa bao la mapema lililofungwa na Azam katika mchezo huo liliwachanganya wachezaji na kubadili kabisa hali ya mchezo.

Lwandamina ambaye alianza kukinoa kikosi cha Yanga katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, alisema ni vigumu kusahau kilichotokea juzi huku akisisitiza kwamba bado wapo imara na watazidi kupambana kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo inayofuata.

“Kipigo tulichopata kimetufundisha mambo mengi lakini zaidi tunatakiwa kuongeza hamasa katika kila mchezo kwa kuwa sababu kubwa iliyochangia kufungwa na Azam juzi ni wachezaji kukosa ari na morali ya ushindi,” alisema Lwandamina.

Hicho ni kipigo cha kwanza kwa Lwandamina ambaye alitua Yanga akitokea katika klabu ya Zesco United ya Zambia.

Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema umoja na mshikamano ndiyo njia pekee itakayoweza kurejesha hamasa kwa mashabiki na wachezaji wa timu hiyo.

“Klabu imekosa umoja na mshikamano kama zamani na hali hiyo imechangia wachezaji na mashabiki kupoteza hamasa uwanjani,” alisema Muro.

Kipigo hicho kinaifanya Yanga kuwasubiri Simba katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa Januari 10 mwaka huu iwapo Wanamsimbazi hao wataibuka na ushindi dhidi ya  Jang’ombe Boys katika mchezo uliotarajia kuchezwa jana katika uwanja huo huo.

Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Simon Msuva, amewaomba mashabiki wasikate tamaa kwa kipigo walichopata bali waendelee kuwaunga pamoja na kocha wao, Lwandamina, ili waweze kufanya vizuri katika hatua inayofuata.

Msuva alisema anaamini kocha atafanya maboresho kwa kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza wafanye vizuri katika michezo mingine inayowakabili kwenye mashindano hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles