25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

ATE yatakiwa kuandaa tuzo mwajiri bora mapambano dhidi ya VVU

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imekitaka Chama cha Waajiri (ATE) kuongeza tuzo ya mwajiri bora katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi ili kufanikisha malengo ya kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo Desemba 4,2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako, wakati wa utoaji tuzo ya mwajiri bora wa mwaka zinazoandaliwa na ATE.

“Endeleeni kutokomeza unyanyapaa mahali pa kazi, ongezeni hamasa kwa wafanyakazi ili wapime kwa hiyari,” amesema Majaliwa.

Aidha amesema Serikali itaendelea kupunguza tozo mbalimbali na gharama za uwekezaji nchini ili kulinda mitaji ya wawekezaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako, akimkabidhi kikombe Ofisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonnay, baada ya benki hiyo kuibuka washindi wa pili wa jumla wakati wa sherehe za utoaji tuzo ya nwajiri bora wa mwaka 2023 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Pia amewataka waajiri kutoa ushirikiano kwa ATE kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kuja kujifunza kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi.

“Suala la kukuza ujuzi ni letu sote yaani sekta binafsi na serikali, ushirikiano katika hili utaleta mabadiliko ya haraka katika kutekeleza azma ya kujenga rasilimali watu yenye ujuzi wa stadi mbalimbali,” amesema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzzane Ndomba, amesema tuzo hizo zimelenga kutambua waajiri wenye misingi bora ya usimamizi wa nguvu kazi na rasilimali watu ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara.

“Tangu kuanzishwa kwa tuzo ya mwajiri bora wa mwaka imeendelea kuwa tukio muhimu kwa waajiri wote nchini linalotambulika katika ngazi ya kitaifa na kuhamasisha kampuni wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu,” amesema Ndomba.

Amevitaja vipengele 14 vilivyoshindaniwa kuwa ni ubora katika usimamizi wa rasilimali watu, utofautishwaji na ushirikishwaji, masuala ya utawala na uongozi, ukuzaji wa vipaji, kusaidia jamii, ushirikishwaji wa mwajiriwa na uwajibikaji katika mwenendo wa biashara na utendaji unaokidhi.

Vipengele vingine ni uwajibikaji katika mwenendo wa biashara na utendaji unaokidhi, mafuzo ya ujuzi wa kazi na uanagenzi, maudhui ya ndani, ubora, uzalishaji na ubunifu, mabadiliko ya tabia nchi, namna ambavyo makampuni yanakabiliana na majanga yanayotokea katika maeneo ya kazi, usawa wa kijinsia na usawa katika maeneo ya kazi na kampuni inayofuata miongozo na matakwa ya kisheria.

Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2005 na tangu wakati huo zimekuwa zikiwatambua wanachama waliofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kuthamini usimamizi wa rasilimali watu na shughuli za kibiashara.

Katika hafla hiyo Kampuni ya Barrick NorthMara iliibuka mshindi wa jumla wakati Benki ya NMB iliibuka mshindi kwa upande wa sekta ya umma na Kampuni ya Serengeti Breweries ikiibuka mshindi wa pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles