NKARA,Uturuki
RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana kibiashara na nchi washirika wake kwa kutumia sarafu moja ikiwamo Urusi, ili kukabiliana na nguvu ya Dola ya Marekani.
Kiongozi huyo aliyasema hayo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Rize akisema Uturuki imeamua kufanya hivyo ili kuendeleza uhusiano kibiashara na mataifa hayo ambayo ni washirika wake.
Alisema, katika mkakati huo atashirikiana na nchi za Urusi, China, Iran na Ukraine ili waweze kupanua wigo wa kibiashara na kasema kuwa na kama mataifa ya Ulaya yatang’ang’ania matumizi ya dola watakuwa wameshajipanga kukabiliana na suala hilo.
“Tunajiunga kibiashara katika sarafu moja ya mataifa ya China, Urusi, Iran, Ukraine, ambayo ina fursa kubwa zaidi ya biashara baina ya nchi hizi.Kama nchi za Ulaya zinataka kuondokana na shinikizo la dola, tuko tayari kujenga mfumo sawa na wao ,” alisema.
Katika hotuba hiyo Rais Erdogan alibainisha kuwa Serikali yake ya Ankara haiwezi kuvumilia hali ngumu ya vikwazo vya kiuchumi vilitangazwa dhidi ya dunia nzima na mashinikizo wanayowekewa nchi nyingine, ambazo zinatishiwa na vikwazo.
Alitamba akisema kwamba hakuna wanasiasa au nchi yoyote duniani kote ambayo itafanikiwa kwa kufuata sera ya uadui zinazoelekezwa dhidi ya Uturuki.
Awali msemaji wa Rais huyo, Ibrahim Kalin, hivi karibuni alieleza katika mahojiano na Gazeti la Daily Sabah kwamba Marekani ina hatari ya kupoteza Uturuki kama mshirika wake.
Gazeti jingine la New York Times lilichapisha makala ya Rais Erdogan, akieleza kuwa vitendo vya Marekani inavyovifanya dhidi ya nchi hii ndivyo vilivyochangia serikali yake kutafuta washirika wapya.
Uhusiano baina ya mataifa haya mawili, ulianza kuzorota, baada ya Rais Donald Trump wa Marekani, kuongeza ushuru kwa bidhaa alminium na chuma kwa asilimia 20 hadi 50 zinazotoka nchini hapa.