22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 29, 2022

WANANCHI WATAMHUKUMU MTATIRO – CUF

 

  • Wamtaka aonyeshe barua aliyomwandikia Maalim Seif

Na NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na upande wa Profesa Ibrahim Lipumba vimemjia juu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa chama hicho, Julius Mtatiro kwa kusema kuwa ni mdhaifu.

CUF – Maalim wamesema hakikutarajia kama Mtatiro angeondoka na kujiunga na upande aliokuwa akiupinga kwamba hauna demokrasia huku CUF – Lipumba wakisema mwanasiasa makini hakimbii migogoro.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim, Salim Bimani, alisema wataendelea na mapambano na kushirikiana na wapinzani wa kweli.

“Hatukutegemea kama angeondoka kwenye upande wa kuikosoa Serikali na kwenda mahali ambako aliona hakuna demokrasia…wananchi ndio watakaomuhukumu,” alisema Bimani.

Hata hivyo alisema hawatatetereka kwani Mtatiro si wa kwanza kuondoka CUF na kwamba wataendelea na mapambano.

“Aliondoka Lipumba, Mapalala na bado CUF iliendelea kusimama kwa sababu misingi yake ni kupigania haki sawa kwa wote.

“Tutaendelea na mapambano na kushirikiana na wapinzani wa kweli, hatutarudi nyuma na anayeshuka safari yake imefika mwisho,” alisema.

Bimani pia alikifananisha kitendo cha wapinzani kuhamia CCM sawa na biashara aliyodai kuwa inapoteza fedha za wananchi.

“Biashara hii ni aibu haijapata kutokea, tunapoteza fedha za wananchi na kuichezea demokrasia, tuikatae kwa nguvu zote,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Profesa Lipumba, Abdul Kambaya, alisema Mtatiro hana ukomavu wa kidemokrasia.

“Alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi, ndiye kamanda halafu anaondoka, huu ni udhaifu wa kisiasa. Wanasiasa ‘strong’ hawakimbii migogoro na hakuna taasisi isiyokuwa na migogoro,” alisema Kambaya.

Alisema pia hakuna ambacho CUF imenufaika naye zaidi ya kuwaingiza kwenye mgogoro na Maalim Seif na kwamba yote aliyosema ni uongo mtupu.

“Amechangia kwa asilimia 70 migogoro iliyoko ndani ya chama na mpaka sasa kuna kesi 38 ziko mahakamani na vikao vya Baraza Kuu yeye ndiye alikuwa anaviongoza.

“Hata mgogoro unaoendelea sasa anapaswa kulaumiwa, alikuwa mshauri wa karibu wa Katibu Mkuu (Maalim Seif) na misimamo aliyokuwa nayo katibu mkuu kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na Mtatiro,” alisema Kambaya.

Alisema pia mitazamo ya kulitumikia taifa si lazima mtu awe CCM kwani anaweza kuwa upande wowote na bado akalitumikia taifa.

“Kuna tofauti ya kufanya siasa kwa masilahi ya Watanzania na kulitumikia taifa kwa maana ya kupata uteuzi. CCM kwenyewe kuna watu wenye ‘potential’ wanakosa nafasi sembuse akienda yeye…Rais amtazame akikosa anachotarajia atapata wakati mgumu sana na utatokea mgogoro mwingine CCM kuliko uliotokea CUF,” alisema.

Akizungumzia chaguzi za marudio alisema; “Rais na chama chake kama wanaona ndio njia za kuwavutia watu watoke upinzani huku ni kubariki matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kuhusu Mtatiro kumwandikia barua Maalim Seif, pande hizo zilisema si kweli kwani Maalim hawezi kubariki uamuzi huo.

Kambaya alisema; “Tuko tofauti na Maalim takribani mwaka mmoja sasa na kutokana na misimamo ya Maalim siamini kama ni kweli amempa baraka. Na katika hili Maalim analo la kujifunza.

Naye Bimani alisema; “Si kweli kwamba Mtatiro alimwandikia barua Maalim…angeionyesha hadharani,” alisema Bimani.

Mtatiro alijiuzulu juzi na kujiunga na CCM kwa madai ya kuchoshwa na migogoro iliyomo ndani ya CUF.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,204FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles