30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

EPUKA KUWAONESHA WATOTO HALI YA KUKATA TAMAA

Na Christian Bwaya


KUNA mtu aliwahi kusema, watoto ni watu maalumu wanaotoka mbinguni. Watoto wanakuja duniani na hali zao njema. Ndani yao kunakuwa na mbegu njema inayohitaji kukuzwa ili kuwafanya wawe watu wazima wenye wema ndani yao.

Mtu mwingine alimfananisha mtoto na mbegu ndogo yenye uwezo wa kuwa mti mkubwa ikipata mazingira sahihi. Hata hivyo, mbegu hii isipopata mazingira sahihi, haiwezi kufikia malengo yake. Inaweza isiote, au ikiota itazaa mti uliodumaa. Kuna ukweli wa kutosha katika mifano hii.

Tulizaliwa na mbegu njema iliyolenga kutufanya kuwa watu wema wenye upendo ndani yetu, watu wenye kiu ya kuhusiana na watu wengine bila kuwasababishia maumivu.

Bahati mbaya mazingira tunayoyakuta, hasa kwenye familia zetu, ndiyo yanayoamua aina ya tabia tutakazokuwa nazo. Familia zetu, kupitia kile kinachofanywa na wazazi, zinaweza kukuza au kuharibu mbegu njema tulizozaliwa nazo.

Katika vitu vya pekee ambavyo Mungu amewapa watoto ni uwezo wa asili wa kuchunguza yale yanayoendelea kwenye maisha ya wazazi wao. Wanafanya hivyo bila sisi wazazi kuelewa.

Tangu mtoto anapoanza kutambua nyuso za watu, anakuwa na uwezo wa ajabu wa kuzisoma nyuso za wale wanaomkaribia. Hamu yake ni kuona furaha kwenye nyuso za watu. Mama anapokuwa na huzuni, kwa mfano, mtoto ana uwezo wa kuelewa mabadiliko hayo.

Pia, kile anachokiona kwa mzazi ndicho kinachoamua yeye afanye nini. Kwa mfano, unapokasirika, kwake hiyo adhabu kwa sababu alitarajia kuona tabasamu. Ili kurudisha tabasamu kwenye uso wa mzazi, mtoto ataanza kujifunza kuelewa kitu gani amekifanya ambacho si sahihi.

Kwa sababu hapendi kumkosea mzazi wake ambaye kimsingi ndiye mtu muhimu zaidi kwenye maisha yake, mtoto atajifunza kuacha kufanya kitu fulani kwa lengo la kuepuka kumfanya mama yake au mtu wa karibu amnyime tabasamu. Hii ndiyo aina ya kwanza kabisa ya adhabu kwa watoto inayoweza kuleta matunda mazuri.

Hata hivyo, inapotokea kila jitihada anazozifanya hazileti tabasamu kwa mzazi, kitu kingine kinaanza kuota ndani yake. Mama anapokasirika muda mwingi, kwa mfano, mtoto hutafsiri yeye ndiye aliyesababisha hali hiyo. Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu, inaweza kuleta matatizo.

Kwa upande mwingine, watoto wana tabia ya kuiga kile tunachokifanya mara kwa mara. Unapokuwa na tabia ya kuwafokea watoto, unawafundisha kwamba hayo ndio maisha. Usishangae ukiwaona wakiwafokea wenzao kwenye michezo.

Kuyasema haya hatumaanishi watoto wanahitaji mzazi malaika asiyekosea. Hapana. Watoto hawahitaji mtu mkamilifu na wala kama mzazi huhitaji kupoteza muda mwingi kujaribu kuwa mzazi mkamilifu.  Jambo kubwa unaloweza kulifanya kwa mwanao, ni kumwonesha uso wa furaha bila kujali hali uliyonayo. Watoto, kama tulivyotangulia kusema, wanapenda kuona nyuso za furaha. Furaha yako haikusaidii wewe bali wao.

Nafahamu si mara zote unaweza kuwa na furaha. Maisha yenyewe hayatuhakikishii nyuso zilizochangamka muda wote. Pamoja na hayo, ni vyema kujitahidi kutunza uso wenye furaha. Unapokuwa mzazi mwenye utulivu bila kujali hali unayopitia, unawajenga watoto kutokuwa na wasiwasi na usalama wao. Utawafanya watoto wawe na amani na maisha. Kwa namna hiyo utawafanya wawe wachangamfu, wenye utulivu na tabia nyingine njema.

Kama si lazima, epuka kumfanya mtoto mdogo abebe mzigo ambao hajawa tayari kuubeba. Mzigo wenyewe ni kuonesha sura yenye masikitiko, huzuni na kukata tamaa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles