27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YATANGAZA MAJINA WABUNGE WAPYA CUF

  • Waliofukuzwa waenda mahakamani kupinga

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza majina manane ya watakaojaza nafasi nane za wabunge wa viti maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF), waliovuliwa uanachama.

Wakati NEC ikitangaza majina hayo, wabunge hao waliofukuzwa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, wamekwenda Mahakama Kuu kupinga hatua hiyo.

Walioteuliwa na NEC kujaza nafasi hizo ni Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Zainab Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.

Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima, alipoulizwa na MTANZANIA ni kwa nini suala hilo limepelekwa haraka kiasi hicho, alisema hakuna uharaka wowote uliofanyika, bali kila kitu kimefanyika kwa mujibu wa Katiba.

Alisema wametoa orodha hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343.

Mazungumzo ya MTANZANIA na Kailima yalikuwa kama ifuatavyo:

MTANZANIA: Tunaomba ufafanuzi wako kuhusu orodha ya majina mliyoitoa ya wabunge wanane. Je, ni kati ya majina ambayo yaliwasilishwa kwenu na CUF ndiyo yamepanda moja kwa moja au mliletewa mengine?

KAILIMA: Kama una Katiba hapo, ukisoma ibara ya 74, inaeleza bayana kwamba baada ya tume kupokea barua kutoka kwa Spika, inashauriana na chama cha siasa husika ili kujaza nafasi hizo.

MTANZANIA: Je, ni muda gani ambao mmeshauriana na chama hicho wakati Spika alitoa barua jana jioni (juzi)?

KAILIMA: Kwani ofisi za Serikali huwa zinaanza kufanya kazi saa ngapi?

MTANZANIA: Saa mbili asubuhi.

KAILIMA: Sawa sawa, na sasa hivi ni saa ngapi?

MTANZANIA: Saa kumi na moja kasoro.

KAILIMA: Sasa tatizo liko wapi? Iko hivi, asubuhi tuliwaandikia CUF barua na wao wakatuletea wenyewe hii orodha tuliyoitoa kwa sababu chama kilikuwa kimeshajiandaa.

MTANZANIA: Awali umesema kwamba tume baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika inashauriana na chama husika, sasa mmetumia muda gani kushauriana na CUF?

KAILIMA: Kwani tatizo liko wapi? Mbona maamuzi mengine tuliyoyafanya hata kwa haraka hivi hamkuhoji? Ngoja nikupe mfano mmoja, siku tulipopokea barua ya Spika kuhusu aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Simba, kesho yake tulitoa jina la anayejaza nafasi yake na hata kwa Chadema tulishapata kufanya hivyo.

 

WALIOFUKUZWA WAENDA MAHAKAMANI

Wabunge wanane na madiwani wawili waliovuliwa uanachama CUF, wamemfikisha mahakamani Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake, wakipinga hatua hiyo.

Wamekimbilia Mahakama Kuu kupinga hatua hiyo na kuiomba itamke kwamba uamuzi wa kuwavua uanachama haukuwa sahihi kisheria.

Wabunge hao waliwasilisha maombi namba 444 ya mwaka huu, jana chini ya hati ya dharura.
Maombi hayo yamefunguliwa na wabunge wote wanane na madiwani wawili dhidi ya Bodi ya Wadhamini CUF, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya.

Katika maombi yao, wanaiomba mahakama itamke kwamba wadaiwa waliwavua uanachama wadai Julai 24, mwaka huu bila kufuata misingi ya haki na Prof. Lipumba alitumia nguvu kuwanyima haki wadai ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Pia wanaomba mahakama itamke kwamba sababu za kuwavua uanachama hazina mashiko kisheria na itoe amri ya kuwazuia kwa namna yoyote kuingilia uanachama wao hadi kesi ya msingi ya kupinga uamuzi wa wadai itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Wabunge hao wanane waliofukuzwa ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed.

Madiwani ni Elizabeth Sakala na Layla Madiba.

 

MAALIM SEIF ATOA TAMKO

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema leo Baraza Kuu la Uongozi halali la chama litakutana katika kikao cha dharura na kutoa uamuzi.

“Tunawaomba na kuwasihi wanachama na wapenzi wote wa CUF waendelee kuwa watulivu na kufuata maelekezo wanayopewa na chama kupitia viongozi halali na vikao halali vya chama.

“CUF kimepita katika dhoruba na misukosuko mingi katika historia yake tokea kilipoasisiwa mwaka 1992. Tulishinda dhoruba na misukosuko hiyo na tutaushinda huu uliopo na hatimaye kuibuka tukiwa imara zaidi,” alisema Maalim Seif.

Juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliridhia kufukuzwa uanachama kwa wabunge hao baada ya Profesa Lipumba kumwandikia barua kiongozi huyo wa Bunge kuwafuta kutokana na alichodai kuwa wanakihujumu chama hicho.

Miongoni mwa makosa yaliyofanya wabunge hao kufukuzwa, ni pamoja na kukihujumu chama katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa Januari 22, mwaka huu na kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho (Lipumba).

Makosa mengine ni kumkashifu Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kaliua, Sakaya na wakurugenzi wa chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kaenichini kukijenga chama sio kurumbami na kupelekana mahakamani uchanhuzi haupo mbani WA 2020 utaporomoka halafu useme Fulani msaliti kura zimeibiwa na mambo mengine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles