Na IBRAHIM YASSIN- SONGWE
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe, linawashikilia watu wanne, wakazi wa Kijiji cha Malezi wilayani Songwe, kwa kujihusisha na uvuvi haramu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Ambwene Mwanyasi, alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 28, mwaka huu kutokana na msako uliofanywa na jeshi hilo katika Ziwa Rukwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwanyasi, watuhumiwa hao walikamatwa na nyavu kumi aina ya makokoro pamoja na vyandarua walivyokuwa wakivitumia katika uvuvi.
“Kuna wanaume wanne tunawashikilia baada ya kuwakuta wakivua samaki katika Ziwa Rukwa kwa kutumia nyavu haramu.
“Watu hao walikuwa wakijihusisha na uvuvi huo wakati wakijua ni kinyume cha sheria. Kwa hiyo, tutawafikisha mahakamani baada ya taratibu zote kukamilika,” alisema Kamanda Mwanyasi.
Pamoja na hayo, aliwataka wananchi kutoendelea na uvuvi haramu ili kuepuka kukamatwa na akawataka wavue samaki kwa kutumia nyavu zilizoruhusiwa kisheria.
Wakati huo huo, kamanda huyo wa polisi alisema operesheni ya kuwakamata wavuvi haramu ni endelevu na kwamba hawatakuwa tayari kuwaacha wananchi waendelee na uvuvi kinyume cha sheria.