29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

JAFO AAHIDI MAKUBWA KISARAWE

Na GUSTAPHU HAULE


NAIBU Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, ameahidi kuendelea kuiboresha Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ili itoe huduma bora kwa wananchi.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe (CCM), alisema tayari amekamilisha jengo la kisasa la upasuaji pamoja na wodi ya watoto na wajawazito yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Baps Charities ya jijini Dar es Salaam.

Jafo alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa majengo hayo iliyohudhuriwa na  wananchi wa Jimbo la Kisarawe wakiwamo madiwani na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Alisema awali hali ya chumba cha upasuaji, wodi za watoto na wajawazito katika hospitali ya wilaya hiyo, ilikuwa mbaya kiasi cha kukatisha tamaa wananchi.

“Hali hiyo ilikuwa ikiwakatisha tamaa wananchi na wengine kulazimika kufuata huduma za matibabu na upasuaji katika hospitali nyingine za jijini Dar es Salaam.

“Baada ya kuona hali hiyo, niliwatafuta wafadhili na kufanikiwa kuwapata Baps Charities ambao walikubali kuaja kufanya ukarabati ambao kwa sasa umeleta sura mpya katika hospitali yetu.

 

“Kwa hiyo, nawaomba wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa sababu kina nia ya dhati ya kuleta maendeleo hapa nchini,” alisema Jafo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda, alisema hospitali hiyo ya Kisarawe ilikuwa na hali mbaya kwa kuwa ilijengwa miaka mingi iliyopita na haijawahi kufanyiwa ukarabati.

“Lakini kutokana na juhudi zinazofanywa na Mbunge Jafo na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla, hivi sasa hospitali iko katika hali nzuri kimajengo na katika utoaji wa huduma pia.

“Kutokana na hiki nilichokiona, nampongeza Waziri Jafo kwa juhudi zake za kuwasaidia wananchi wa Kisarawe hasa katika kuwatatulia kero zao.

“Naamini ukarabati huu uliofanyika hospitalini hapa, utawanufaisha wananchi wa Dar es Salaam na Pwani ambao wamekuwa wakitibiwa hospitalini hapo,” alisema.

Naye Katibu wa Baps Charities, Paresh Chollera, alisema wataendelea kushirikiana na mbunge huyo katika kuhakikisha wanakamilisha ukarabati wa hospitali hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles