NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
MASHINDANO ya mashairi yatakayofanyika Julai 30 na 31, mwaka huu katika viwanja vya Karimjee jijini hapa yamelenga kukumbuka historia ya Jiji la Dar es Salaam ambalo lilisifika kwa ushairi na tenzi nzuri.
Mwandaaji wa mashindano hayo, mstahiki Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita, alisema mashairi hayo yataghaniwa na wazee wa jiji hilo ambapo watawakilisha mada mbalimbali katika tenzi zao.
“Tungependa watukumbushe historia ya Mzizima ilikuwaje, Mwalimu Julius Nyerere alipoingia Dar es Salaam walimpokeaje na kwanini maadili ya vijana yanamomonyoka,” alisema Mwita.
Pia Meya huyo aliongeza kwamba Septemba 23 na 24, mwaka huu kutakuwa na maonyesho ya utalii wa ndani ambapo ngoma kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania zitaonyeshwa.