27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge ataka Burundi isibembelezwe

Peter Mathuki
Peter Mathuki

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

WAKUU wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wametakiwa kuacha kuibembeleza Burundi inayotakiwa kusimamia mkataba wa makubaliano ya uanzishwaji wa jumuiya hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana kwenye kikao cha siku moja cha Bunge hilo kilichoitishwa kupitisha azimio la kupinga mauaji ya aliyekuwa Mbunge wa Bunge hilo, Raia wa Burundi, Hafsa Mossi aliyeuawa Julai 13, mwaka huu kwa kupigwa risasi jijini Bujumbura.

Akizungumza kwenye majadiliano hayo Mbunge kutoka Kenya na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Peter Mathuki, alisema umefika wakati kwa wakuu wa nchi za EAC, kuacha kuendelea kuibembeleza Burundi katika suala la amani.

Mathuki aliyewasilisha hoja hiyo iliyojadili hali ya amani na demokrasia nchini Burundi, alisema Mossi aliuawa kutokana na mgogoro wa kisiasa nchini humo.

“Wakuu wa nchi waache kuibembeleza Burundi katika suala la amani. Huyu ni mwanachama wa EAC na alisaini mkataba wa kuanzishwa jumuiya unaotaka kila nchi kusimamia amani na demokrasia.

“Serikali ya Burundi lazima ijitokeze na kuhakikisha amani inarejea na sisi wabunge tunatakiwa kusema sasa inatosha kwa viongozi kuendelea kuuawa nchini humo.

“Katika suala hili hatuombi, tunawaagiza viongozi wa Burundi warekebishe haraka tofauti zao kwa maslahi ya taifa na raia wake.

“Jumuiya haiwezi kurudishwa nyuma na watu wachache, kama hawataki watuambie wanataka nini,” alihoji Mathuki.

Kwa upande wake, Mbunge kutoka Tanzania Shyrose Bhanji, alilaani vikali tukio hilo huku akisisitiza kuwa suala la amani nchini humo linatakiwa kupewa kipaumbele kuliko vitu vingine vyote.

Shyrose aliyebubujikwa machozi wakati akichangia bungeni humo, alisema bila kuwa na usalama nchini Burundi, vitendo vya mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia na viongozi vinaweza kuendelea.

“Pamoja na kwamba bado uchunguzi wa  mauaji haya haujakamilika na hakuna taarifa zozote, tunaziomba pande zinazovutana zihakikishe amani inarejea haraka,” alisema Shyrose na kuongeza.

“Niwaombe pia viongozi wanaohusika na mazungumzo ya kutafuta amani Burundi, waongeze kasi ili amani iweze kurejea.

Naye Mbunge kutoka Uganda, Dorah Byamukama akichangia katika kikao hicho, aliomba uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na vyombo binafsi kutoka nje ya Burundi.

Dorah aliyebubujikwa machozi kila alipozugumza bungeni humo, alimwelezea marehemu Mossi kuwa alikuwa kiongozi wa kipekee na aliyependa amani ya nchi yake.

Kikao hicho kiliongozwa na Spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega na kuhuduriwa na wabunge mbalimbali waliokuwa wamejawa na huzuni kila walipokuwa wakichangia.

Hivi karibuni mjini Arusha, kulifanyika mazungumzo ya awamu ya pili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendeea nchini Burundi yakiongozwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, mazunguzo hayo hayakufikia mwisho baada ya kuibuka kwa hali ya kutoelewana miongoni mwa wajumbe waliokuwa wakishiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles