25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aendelea kusota rumande

PATRICIA KIMELEMETA Na TUNU NASSOR


-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi limeendelea kumshikilia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe siku mbili mfululizo ambako jana walienda nyumbani kwake na kufanya upekuzi kuhusiana na tuhuma za uchochezi.

Zitto alikamatwa juzi nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam baada ya kudaiwa kutoa taarifa za uongo zinazohusiana na mauaji ya wananchi zaidi ya 100 katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Taarifa hizo anadaiwa kuzitoa alipozungumza  na waandishi wa habari   Oktoba 28, mwaka huu katika ofisi yake,  Kijitonyama,   Dar es Salaam.

Polisi walipomkamata juzi walimhoji kwa saa 8.00 kabla ya  kupelekwa kwenye Kituo cha Polisi   Mburahati na kumuweka mahabusu.

Ilipofika jana saa 2:30 asubuhi jana  polisi walifuatana  na mbunge huyo hadi nyumbani kwake Masaki ambako walifanya upekuzi kwenye nyumba hiyo huku wakiwa wameimarisha ulinzi ndani na nje ya nyumba anayoishi.

Ilipofika saa 5:30 walimchukua na kurudi naye Kituo cha Polisi Oysterbay kuendelea na mahojiano na ilipofika saa 7:00 walimchukua na kumpeleka Kituo cha Polisi Mburahati.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Wakili wa Zitto, Jebra Kambole alisema   wamewasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  mteja wao aweze kupewa dhamana.

“Kwa sasa tunahangaikia dhamana Kisutu, ikiwa tutafanikiwa tutaileta polisi mteja wetu aweze kupewa dhamana,” alisema Kambole.

Alisema Zitto amehojiwa mambo mbalimbali yaliyohusu mazungumzo yake  na waandishi wa habari   hivi karibuni.

Alisema miongoni mambo hayo ni mauaji katika  Kijiji cha Mpeta Uvinza, kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji (MO)  na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanaamini jeshi hilo linaweza kumuachia kwa dhamana  aweze kuendelea na majukumu mengine ya taifa kwa sababu mteja wao ni mbunge hivyo anapaswa kuwatumikia wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Kinondoni, Murilo Jumanne , alikataa  kulizungumzia suala hilo akidai aalikua nje ya ofisi na kwamba alikuwa hajatapa taarifa yoyote kutoka kwa watendaji wake.

“Nilikua kwenye msafara wa Rais. Dk John Magufuli alipoenda kwenye kongamano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).

“Mpaka sasa sijapata taarifa yoyote kutoka kwa watendaji wangu kwa sababu sikua ofisini muda mrefu.

“Hivyo basi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa mpaka watakaponieleza walipofikia,” alisema Kamanda Murilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas, alipoulizwa kuhusiana na kushikiliwa kwa mbunge huyo, alisema   wanaendelea na mahojiano na mbunge huyo licha ya yeye kutokuwapo ofisini.

“Nipo kwenye msafara wa Rais Magufuli, lakini askari bado wanaendelea na mahojiano ingawa sijajua wamefikia wapi kwa sababu nipo nje ya ofisi,” alisema Kamanda Sabas.

LOWASA AZUILIWA

Ilipofika saa 9.00 alasiri, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa alifika katika Kituo cha Polisi Mburahati aweze kumuona Zitto, lakini alizuiliwa kumuona kwa madai kuwa muda wa kumuona ulikuwa umekwisha kupita.

Msemaji wa Lowassa, Abuubakar Liongo, alisema   alifika Lowassa kituoni hapo na kuomba kibali cha kuonana na Zitto kwa sababu ni kiongozi mwenzao wa upinzani hivyo wameamua kushirikiana waweze kukabiliana na lolote linalowapata.

Kutokana na hali hiyo, Lowassa alisema katika kipindi hiki wapinzani wanahitaji kuwa kitu kimoja kuliko wakati mwingine wowote  kukabiliana na changamoto zinazowapata wapinzani.

“Nimeshangazwa kuona nazuiliwa kumuona Zitto wakati ni kiongozi mwenzetu wa upinzani kwa kunyimwa kibali na kuambiwa kuwa muda wa kumuona umekwisha,” alisema Lowassa.

Katika mkutano wake, Zitto aliwaambia waandishi wa habari kuwa; “Tulikua tukifuatilia kwa kina yanayojiri Uvinza tangu kuuawa kwa polisi wetu, tunasikitika kusema   taarifa tunazozipata kutoka Uvinza  zinaogofya mno.

“Tunaambiwa   wananchi zaidi ya 100 ambao ni  wanyantuzu,  wamefariki dunia  kwa kupigwa risasi na polisi na wengine wakielezwa  kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitali baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi.

“Nashangaa Jeshi la Polisi limekaa kimya pamoja na Mkuu wa Jeshi hilo(IGP), Simon Sirro kutembelea eneo la maafa.

“Haiwezekani kamwe  tukio kubwa kama hilo kutokea halafu serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yoyote kwa wananchi,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles