26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanazuoni wamchambua Magufuli

NA ANDREW MSECHU – dar es salaam


WANAZUONI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na watu wengine, jana walipata wasaa wa kuchambua miaka mitatu ya Rais Dk. John Magufuli juu ya hali ya siasa na uchumi nchini.

Katika mdahalo uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo, wanazuoni hao walijadili mada mbalimbali, huku wengi walijaribu kulinganisha hali ilivyo sasa na ilivyokuwa katika awamu zilizopita.

Kimsingi wanazuoni hao waligawanyika sehemu mbili, wakiwamo ambao wapo serikalini baada ya kuteuliwa kwenye nafasi mbalimbali na Rais Magufuli, huku wengine wakiwa ni walimu tu kwenye chuo hicho.

Katika kongamano hilo lililochukua takribani saa tano, baada ya watoa mada kuwasilisha maoni yao na mapendekezo yao, Rais Magufuli ambaye alikuwa mshiriki maalumu, pia alipata fursa ya kuzungumza juu ya aliyotenda na anakotaka kufika.

 

PROF. MUKANDALA ATOA MASWALI MATANO YA KUPIMA KAMA JPM KAFANIKIWA

Msomi wa sayansi ya siasa, Profesa Rwekaza Mukandala, aliwasilisha mada juu ya siasa na utawala.

Katika uwasilishaji wake, alisema atatoa maswali matano ambayo watu watajibu wenyewe na kuona watampa alama ngapi Rais Magufuli juu ya alivyofanya kwenye maeneo hayo.

Alisema; “Swali la kwanza na la pili ni la nadharia na kiitikadi. Je, kumekuwa na uelewa wa ulimwengu na changamoto zake pamoja na kuainisha matatizo ya mfumo huu wa kimataifa?

“Je, kumekuwa na uelewa na uchambuzi wa hali ya nchi yetu, changamoto zake na namna ya kuzitatua?

“Swali la tatu litahusu kazi ya Rais, kiongozi na mwanasiasa mkuu wa nchi. Je, ameweza kuongoza kuwa mstari wa mbele kwa mawazo na vitendo? Je, ameweza kuhamasisha wananchi wamfuate? Je, ameweza kubuni lugha mahususi na mwafaka inayochangamsha na kujenga upendo, utashi na utii kwake?

“Swali la nne linahusu chama. Je, ameweza kuimarisha na kuongoza chama ili kiwe kitiifu kwake na kiweze kuunga mkono juhudi zake?

“Swali la tano na la mwisho linahusu dola. Je, Serikali na taasisi zake zimeimarishwa? Mfumo na mchakato wa utendaji kazi umeboreshwa? Utawala wa sheria unazingatiwa? Haki za kijinsia, haki za binadamu na watu wenye ulemavu na haki za kukusanyika na kujieleza zinazingatiwa?”

Profesa Mukandala alisema katika mtanziko wa kisiasa, siasa ni mchezo mgumu wa hesabu za kimkakati, hivyo kiongozi yeyote wa kisiasa huwa na malengo yake.

Alisema lengo la kwanza kwa mwanasiasa huwa ni kupata madaraka, lengo la pili huwa ni kuhakikisha anadumu kwenye madaraka na lengo la tatu huwa ni kujenga chama cha siasa kilicho na uaminifu na tiifu kwake.

“Katika kufanya tathmini ya utendaji wa Rais Magufuli, wapo watu wanaoshabikia matokeo kwa sababu tu wameona jambo fulani limefanyika bila kujua lolote kuhusu kufanyika kwake,” alisema.

Profesa Mukandala alisema tathmini ya utendaji pia inafanyika kwa kuangalia kigezo cha hali ya watu na namna wanavyojisikia kutokana na matendo ya Serikali yao.

Alisema wapo wanaopenda kuona amani na usalama ikiwemo ulinzi na uhusiano wa kikanda na wa kimataifa kwa kutumia mchakato wa kupima bidii inayoonekana na si matokeo na kupima uwezo wa vifaa vilivyopo.

“Wakati mwingine ni muhimu sana kupima kwa  kuangalia kigezo cha hali ya watu kwa kuwa hata kama baba unahudumia familia yako kwa kila kitu, unaweza kukuta pamoja na juhudi zako familia yako haina furaha, kwahiyo ni suala muhimu kuliangalia,” alisema.

Alisema kinadharia, tulikotoka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliwaaminisha Watanzania kwamba mfumo wa kibeberu haufai na kukataa kutii amri zao kwa vitendo suala ambalo wananchi walilielewa.

“Kwa miaka hii mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli ameonesha kwa vitendo namna anavyowajibika kufuatilia mambo na watendaji wake kwa ukaribu na siyo kumwachia Waziri Mkuu peke yake na wenzake. Amejijengea uwezo mzuri wa kisiasa na kiutawala,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika kulinganisha mwenendo wa Rais Magufuli na Mwalimu Nyerere, mwasisi huyo wa taifa alipigania chama na kuhakikisha anakuwa na chama kimoja kinachomtii, lakini ulifika wakati akabaini kwamba bila upinzani chama kimoja kinalala, hivyo akaamua kukubaliana na mfumo wa vyama vingi.

Profesa Mukandala alisema hii inaonesha kuwa ni vyema kuwa na mkakati wa kunyoosha chama, lakini pia kujenga nafasi ya kupendwa na wanachama ili uendelee kuwaongoza.

Alisema kuhusu katiba, namna ya kiongozi kujipima ni pamoja na anavyopokea na kumalizia mambo aliyoyakuta, akitaja suala la mchakato wa katiba ambalo bado limewekwa kando.

Profesa Mukandala alisema kwa sasa kuna mambo mengi ya kuangalia ikiwemo kuona kama kuna haja ya kuendelea na mchakato huo au la na iwapo kuna mabadiliko yanayotakiwa kufanyika.

“Kwa sasa ni miaka minne tangu mchakato wa katiba mpya ulipofanyika na kutuachia rasimu ya Mabadiliko ya Katiba, kuna haja ya kuangalia iwapo mchakato huo utarejewa kwa kuwa miaka minne kisiasa ni mingi, lazima utahitaji mabadiliko katika baadhi ya mambo,” alisema.

 

PROF SHIVJI ASEMA HOJA YA VIWANDA NI TANGU NYERERE

Akizungumza wakati wa maswali na maoni, mwanzuoni wa siku nyingi UDSM ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema suala la viwanda limekuwa likizungumzwa kila wakati, hivyo ni vyema kurejea katika makosa aliyowahi kuyataja Nyerere kutokana na kilichosababisha kufa kwa viwanda.

Alisema makosa ambayo aliyataja Mwalimu Nyerere ilikuwa suala la utegemezi wa viwanda, mashine, vipuri na hata uongozi hivyo kuvifanya vishindwe kujiendesha.

Profesa Shivji alisema suala jingine ni kutokuwa na uwiano baina ya sekta ya kilimo ambayo ndiyo iliyotakiwa kuwezesha viwanda kupata malighafi na viwanda, hivyo kutokuwa na uhakika wa malighafi na kushindwa kujenga soko la ndani.

Alisema suala jingine alilolitaja Mwalimu Nyerere mwaka 1982 katika uchambuzi wake kuhusu kufa kwa viwanda lukuki vilivyojengwa na Serikali, ni viwanda hivyo kuwa na uongozi mbovu hivyo kushindwa kusimamia shughuli za uendeshaji wake.

Profesa Shivji alisema katika miongo miwili baada Mwalimu Nyerere kuachia ngazi, masharti mbalimbali yaliwekwa na mashirika ya kimataifa ambayo yalisababisha kuviua kabisa viwanda hivyo.

“Kwa kuwa sasa tumeshakuwa na uzoefu, suala la msingi ni kujifunza kutokana na uzoefu huo, hasa tukitumia mfano wa awamu ya kwanza, ambao ulitupa sababu za kufa kwa viwanda ili na sisi sasa tujue wapi kwa kuanzia na namna ya kwenda mbele,” alisema.

 

PROF. KABUDI: JPM AMETEKELEZA AHADI ZAKE VYEMA

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye hakuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye ratiba ya kuwasilisha mada alipewa nafasi kwa ajili ya kumkaribisha Rais Magufuli.

Profesa Kabudi ambaye ni mwanasheria mbobezi,  alitumia nafasi hiyo kummwagia sifa Rais Magufuli akisema ametekeleza ahadi zake vyema tangu alipoapishwa kuwa Rais Novemba 5, 2015.

Alisema lengo la Serikali ni pamoja na kuendelea kukuza uchumi na kupunguza umasikini, kujenga mazingira wezeshi na uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kujenga nidhamu ya utendaji kazi na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

“Uchimbaji wa madini umeongezeka mpaka asilimia 14.5, mawasiliano asilimia 13.8. Mapato ya ndani ya kodi yameongezeka kutoka Sh bilioni 12,334 hadi Sh bilioni 15,191 mwaka 2017/18 huku makusanyo ya kodi kwa jumla yakifikia wastani Sh trilioni 1.2 kwa mwezi mwaka 2018 ikilinganishwa na Sh bilioni 800 mwaka 2015,” alisema.

Kuhusu mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge, Profesa Kabudi alisema japokuwa kuna watu wanajitahidi kupiga kelele juu ya mradi huo, Serikali itautekeleza tu.

“Niseme bila tashwishi utatekelezwa ije mvua lije jua, utatekelezwa. Wapende wasipende utatekelezwa, watake wasitake utatekelezwa. Kelele zitakuwa nyingi lakini utatekelezwa,” alisema.

Alisema wakati wa Mwalimu Julius Nyerere mradi huo ulishindikana kutokana na kukosekana fedha, lakini kwa sasa utafanikiwa kutokana na Serikali kutia nia ya kuukamilisha.

Profesa Kabudi alisema mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusisitiza kuwa iliyopo sasa haitang’olewa.

Kuhusu ununuzi wa ndege, alisema licha ya kubezwa na baadhi ya watu, lakini Serikali imenunua ndege mbili aina ya Airbus A 220-300 zinazotarajia kuingia nchini mwezi huu huku ndege ya pili ya Dreamliner ikitarajiwa kuwasili nchini mapema 2020.

Pia aligusia bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Tanga.

“Mnaotoka Tanga hata bomba halijaisha lakini hali ya vuguvugu la uchumi wa Tanga imebadilika.

“Ujenzi na madaraja makubwa, mhuri wake ni Magufuli. Tumeona Mfugale Flyover (daraja la juu la Tazara jijini Dar es Salaam) na sasa tunaona ujenzi wa interchange ya Ubungo (barabara ya juu ya Ubungo),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles