YANGA MWENDO ULE ULE

0
883

Theresia Gasper, Dar es salaam

YANGA imejikusanyia pointi tatu nyingine katika ,Ligi Kuu Tanzania Bara(VPL) msimu huu, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha  pointi 13 na kukamata nafasi ya 11, miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo, ikishuka dimbani mara sita, ikishinda michezo minne, sare moja na kupoteza mmoja.

Dakika ya 10, Patrick Sibomana aliiandikia Yanga bao la kuongoza baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa JKT Tanzania.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa Yanga wakiendelea na shangwe za bao la Sibomana, Adam Adam aliisawazishia JKT Tanzania kwa mkwaju mkali wa mbali uliomshinda kipa Farouk Shikalo.

Bao hilo halikuipunguza kasi Yanga badala yake iliendelea  kulishambulia lango la wapinzani wao.

Dakika ya 21,  mshambuliaji Juma Balinya aliitendea haki pasi ya Deus Kaseke na kuiandikia Yanga bao la pili kwa mkwaju, baada ya kuwazidi kazi mabeki wa JKT Tanzania.

Dakika ya 26, mkwaju wa Sibomana ulitoka nje kidogo ya lango la  JKT Tanzania.

Kosa kosa ziliendelea kila upande lakini zaidi lango la JKT Tanzania ndio lilionekana kuwa mashakani muda mwingi.

Dakika ya 34, mshambuliaji David Molinga aliiandikia Yanga bao la tatu kwa mkwaju wa mpira wa adhabu ambao ulimshinda kipa wa JKT Tanzania, Abdulrahim Mohamed.

Dakika ya 40, pasi ya Kaseke ilimfikia Balinya lakini alikosa utulivu  baada ya mkwaju wake  kutoka nje ya lango la JKT Tanzania.

Kabla  ya  dakika 45 za kipindi cha kwanza hakijamalizika,  Danny Lyanga aliifungia JKT Tanzania bao la pili kwa kichwa.

Kwa ujumla kipindi cha kwanza, timu zote zilionekana kujenga mashambulizi  kuanzia nyuma zikitumia pasi fupi fupi, ingawa Yanga ilionekana kumiliki mpira zaidi na kufanya mashambulizi mengi  langoni mwa JKT Tanzania. 

Dakika ya 50,  Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alimtoa Mapinduzi Balama na kuingia Mohamed  Issa.

Dakika ya 52, Juma Abdul alilimwa kadi ya njano  baada ya kumfanyia madhambi Adeyum Saleh wa JKT Tanzania.

Mkwasa alifanya mabadiliko mengine dakika ya 60, alimtoa David Molinga na kumwingiza Abdulaziz Makame kabla ya JKT Tanzania kutoka Richard Maranya na kuingia Hadidh Mussa.

Dakika ya 70, Mwinyi Kazimoto wa JKT Tanzania alilimwa kadi ya njano kwa kupinga uamuzi wa mwamuzi.

Mabenchi yote ya ufundi yaliendelea kutafuta namna ya kupata mabao zaidi, dakika ya 77 alitoka Sibomana na kuingia Mrisho Ngassa kwa upande wa Yanga, wakati JKT  Tanzania alitoka Adam na kuingia Mohamed Fakhi ambaye dakika ya 87 alilimwa kadi ya njano kwa kumdanganya mwamuzi kwamba alichezewa madhambi ili ampe penalti.

Shikalo alilimwa kadi ya njano dakika ya 88 kwa kupoteza muda.

Hadi kipyenga cha mwisho kinalia  kuashiria kumalizika kwa pambano hilo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania.

Baada ya mchezo huo, nahodha  msaidizi wa Yanga, Juma Abdul alikabidhiwa Sh milioni 10 na wadhamini wa timu hiyo , Kampuni ya GSM kutokana na ushindi walioupata kwenye mchezo huo.

Katika mchezo mingine, Kagera Sugar ilichumpa hadi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikitokea nafasi ya pili, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli .

Mabao ya Kagera yalifungwa na Yusuph Mhilu dakika ya 10 na Nasoro Kapama dakika ya 62, huku lile la Lipuli likifungwa dakika ya 85 na Paul Nonga. 

Ushindi huo uliifanya Kagera kufikisha pointi 23, baada ya kushuka dimbani mara 11, ikishinda michezo saba, sare mbili na kuchapwa mara mbili.

Alliance iliibuka na ushindi wa mabao 2 – 1

Dhidi ya KMC Uwanja wa Nyamagana Mwanza, Coastal Union ikailaza Namungo mabao 3-1 Uwanja wa Majaliwa, Ndanda ikakubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Polisi Tanzania 

iliyokuwa ugenini Uwanja wa Nangwanda, wakati Prisons ilazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwadui Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here