Utata waliomchukulia fomu Mbowe kugombea uenyekiti

0
1361

Grace Shitundu, Dar es salaam

MWENYEKITI wa Baraza la Vijana Chadema ( Bavicha) Patrick ole Sosopi amekana kuwafahamu vijana waliodai kumchukuliwa fomu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ya kugombea kwa mara nyingine nafasi  hiyo.

Pia amedai kwamba ingawa vijana hao wanahaki ya kufanya hivyo, huo sio msimamo wa baraza kwani linaheshimu taratibu.

Kauli hiyo ya Sosopi imekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila siku (sio Mtanzania) kuripoti kuwa vijana wa Chadema wamejitolea kumchukulia fomu Mbowe ambaye hata yeye hajatangaza rasmi kama atagombea tena nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mchakato huo, Daniel Naftali aliliambia gazeti hilo kuwa wao kama vijana wamezunguka nchi nzima kuchangishana fedha kwa ajili ya kumchukulia Mbowe fomu na kumshawishi kugombea nafasi ya uwenyekiti wa chama na tayari vijana 10,000 wameshatia saini kuunga mkono zoezi hilo.

Vijana hao wanatarajiwa kumchukulia Mbowe fomu na kumpelekea nyumbani kwake Novemba 24 mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi Sosopi alisema mchakato huo unaofanywa na vijana hao sio msimamo wa Bavicha.

“Si msimamo wa Baraza la Vijana, na hata hao vijana wenyewe siwafahamu, lakini kama ni wanachama wanahaki ya kufanya hivyo, hakuna sheria inayowakataza pale wanapoona mtu fulani anafaa lakini kama baraza hatuwezi kufanya hivyo”alisema Sosopi.

Alisema Bavicha wanaheshimu taratibu zilizowekwa katika uchaguzi wa viongozi wa chama na mtu yoyote anaruhusiwa kugombea ili mradi atimize vigezo vinavyohitajika.

Alisema kwa upande wa Baraza la vijana na lile la Wazee watakaowania pamoja na kuwa na kigezo cha kuwa mwanachama ni lazima umri uzingatiwe na kwa upande wa Baraza la Wanawake ni lazima uwe mwanamke.

“Lakini katika nafasi za Mwenyekiti, Makamu mwenyetiki Bara na Visiwani mwanachama yoyote anahaki ya kugombea nafasi hizo aingalii umri au jinsia mradi uwe na umri wa kupiga kura,” alisema Sosopi.

Mbowe aliwahi kuweka wazi msimamo wake kuwa hana tatizo na mwanchama yoyote atakayeitaka nafasi hiyo ili mradi afuate utaratibu wa chama na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi hiyo.

Tayari Mbunge wa Ndanda, Cecily Mwambe alionesha nia ya kuwania nafashi hiyo.

Katibu Mkuu wa chadema Dk. Vicent Mashinji alitangaza ratiba ya kuchukua fomu kuwa ni kuanzia Novemba 18 hadi 30 huku Mkutano Mkuu ukitarajiwa kufanyika Desemba 18 mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here