23.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

YANGA MAJARIBUNI SONGEA

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo inashuka dimbani kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Majimaji katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.

Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani ikifahamu kwamba inahitaji ushindi ili kurefusha pengo kati yake na mpinzani wake mkuu, Simba ambayo kesho itaumana na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Yanga ipo nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi nne, baada ya kucheza michezo  miwili, ikianza kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli FC kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji wiki iliyopita.

Kama itafanikiwa kavuna pointi tatu leo, itafikisha pointi saba, ambazo zitaipeleka juu na kuiacha Simba ikisalia na pointi nne kabla ya mchezo wa kesho dhidi ya Mwadui.

Katika mchezo huo, Yanga itataka kuendeleza ubabe wao baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji katika mchezo uliozikutanisha timu hizi msimu uliopita kwenye uwanja huo.

Majimaji kwa upande wake itaingia uwanjani ikisaka ushindi kwa sababu kuu mbili, moja ikiwa kulipa kisasi cha kulizwa msimu uliopita, pili kuwapa faraja mashabiki wake baada ya kuishuhudia timu hiyo ikikosa ushindi katika michezo yake miwili msimu huu.

Wanalizombe hao walizindua kampeni zao za Ligi Kuu msimu huu kwa kucharazwa mabao 2-0 na Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji kabla ya kulazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini na maafande wa Tanzania Prisons.

Sababu hizo zinaufanya mchezo kati ya timu hizo kuwa na upinzani mkubwa, kwani kila upande utataka kulinda heshima yake na kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi hiyo.

Habari njema kwa wapenzi wa Yanga ni maendeleo mazuri ya afya ya kiungo wao Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, ambaye alishindwa kumaliza dakika 90 katika mchezo uliopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga.

Meneja wa Yanga, Hafidhi Salehe, aliliambia MTANZANIA kwamba, wana matumaini ya kumtumia Kamusoko leo baada ya hali yake kiafya kuendelea vizuri.

“Maandalizi yako vizuri, wachezaji tuliokuja nao wapo fiti, hali ya Kamusoko imezidi kuimarika, lakini suala la kucheza au kutocheza ni uamuzi wa kocha ambaye anajua nani amtumie kulingana na mchezo husika,” alisema Hafidhi.

Wakati meneja huyo akijigamba kuwa wako tayari wa vita hiyo, benchi la ufundi la Majimaji limewapa maagizo maalumu mabeki wa timu hiyo wanaoongozwa na  kitasa, Tumba Sued, kuhakikisha wanatumia mbinu sahihi kuwazima washambuliaji wa Yanga wanaoongozwa na mkali wa mabao, Ibrahim Ajib, ili wasifurukute.

“Nimeichunguza Yanga wakati ikicheza na Njombe Mji, nimebaini mapungufu yao kwenye baadhi ya sehemu, hivyo nitatumia machache niliyoyaona kuhakikisha napata ushindi katika mchezo huo,” alisema Kondo.

Mbali na mchezo huo, ligi hiyo itaendelea katika viwanja vingine vinne, ambapo Mtibwa Sugar iliyoanza msimu kwa kishindo ikishinda michezo yote miwili itakuwa mwenyeji wa Mbao FC kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

Stand United baada ya kujeruhiwa na Lipuli kwa kulazwa bao 1-0 itakuwa mwenyeji wa Singida United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC kutoka kule Mtwata itakuwa mgeni wa Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wakati Lipuli FC itaikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,248FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles