Na SHEILA KATIKULA-MWANZA
WAOMBAJI wa nafasi za uongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza, wamefundwa namna ya kujiepusha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).
Akizungumza juzi wakati wa utoaji semina hiyo, Ofisa Mchunguzi wa Takukuru Wilaya ya Ilemela, Doreen Ntongani, alisema Serikali inataka viongozi ambao wanachukizwa na vitendo vya rushwa kwa kuwa ni adui wa haki anayekwamisha maendeleo hivyo kuwasihi kuwa makini katika chaguzi za chama.
Alisema kila mwombaji ana wajibu wa kukemea vitendo vya rushwa kwa kuwa ndiyo imekuwa ikisababisha kupatikana viongozi wasiofaa ambao wamekuwa wakishindwa kuwatumikia wananchi na kuwatatulia kero zao.
“Kifungu cha 15 cha sheria ya kuzui na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007, kinatamka ni kosa kuchukua zawadi, manufaa, kitu chochote. Ni kosa kutoa hongo kwa mtu yeyote, kupokea, kukubali kwa madhumuni ya kutokutoa huduma zinazohusiana na majukumu ya kikazi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika kifungu hicho makosa madogo madogo yanayotajwa kwa majina mbalimbali kama vile chauchau, kitu kidogo na chai, hivyo kwani waombaji nafasi za uongozi ndani ya chama pamoja na mawakala wake iwapo watafanya vitendo hivyo wakati wa kampeni, uteuzi ili kutimiza malengo na kubainisha watashtakiwa.
“Niwaombe kujiepusha na vitendo vya rushwa ili tupate viongozi bora, watiifu, wanyenyekevu na wachapakazi ambao wakishachaguliwa watimize ahadi zao walizozitoa wakati wa kampeni, lakini wakitambua kuwa kutoa na kupokea rushwa ni kosa,” alisema.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela, Maulid Acheni, alisema ni mwiko kwa kiongozi, mgombea au mwanachama wa CCM kutoa na kupokea rushwa wakati wa uchaguzi na kubainisha kwamba ikithibitika ametoa rushwa ili achaguliwe ataenguliwa kugombea nafasi aliyoomba.
“Hata kama mgombea ameshinda uchaguzi na ikathibitika alitoa rushwa atanyang’anywa au kufutiwa ushindi aliopata na kuzuiwa asigombee tena katika uchaguzi mwingine wa chama kwa muda utakaoamuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,” alisema.