Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) imepangwa kuanza leo katika viwanja tofauti, ambapo michezo mitano itapigwa.
Ligi hiyo inashirikisha timu 24, ambazo zimegawanywa katika makundi matatu yaliyopewa jina la A, B na C, huku kila kundi likiundwa na timu nane.
Kundi A linaundwa na timu za African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers, JKT Ruvu, Kiluvya United, Mgambo JKT, Mvuvumwa na Mshikamano.
Kundi B lina Coastal Union, JKT Mlale, KMC, Mawenzi Market, Mbeya Kwanza, Polisi Moro, Mufindi United na Polisi Dar.
Kundi C imo Alliance School, Rhino Rangers, Pamba, Polisi Mara, Polisi Dodoma, Transit Camp, Toto African na JKT Oljoro.
Michezo itakayopigwa leo ni pamoja na JKT Mgambo itakayokuwa mwenyeji wa maafande wenzao wa JKT Ruvu, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo Mawenzi Market itakuwa mwenyeji wa KMC ya Kinondoni, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wakati Mufindi United itakuwa mgeni wa Polisi Dar kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Rhino Rangers ya Tabora itakipiga na Alliance Schools kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Polisi Mara itaikabili Toto Africans kwenye dimba la Karume mkoani Mara.
Ligi hiyo itaanza huku kukiwa na mabadiliko makubwa mawili yaliyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (TFF) la kwanza likiwa ni ongezeko la timu zitakazopanda daraja, kutoka tatu za awali hadi sita.
Hiyo ina maana kwamba, kila kundi litapandisha timu mbili tofauti na utaratibu wa awali, ambapo ilipanda timu moja.
Kutokana na mabadiliko hayo, Ligi Kuu msimu ujao itakuwa jumla ya timu 20 kutoka 16 za sasa, hivyo timu mbili ndizo zitashuka daraja tofauti na tatu kulingana na utaratibu wa msimu uliopita.
Baada ya kushuka timu mbili, zitabaki 14, ambazo zitasubiri sita zitakazopanda daraja.
Mabadiliko mengine yanahusu kanuni ya 25, ambapo kuanzia sasa timu mwenyeji atachukua asilimia 60 ya mapato yatakayotokana na viingilio vya milangoni baada ya makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na gharama za tiketi.
Hatua hiyo ina lengo la kuiwezesha timu mwenyeji kupata uwezo wa kiuchumi ili kujitangaza kwa wadhamini pamoja na kutangaza mechi zake.