24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

WEMA ATUA CHADEMA

*Amsindikiza Mbowe Mbowe kortini, yeye na kundi lake kupokewa rasmi leo


Mwandishi Wetu

MSANII maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu, amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema), huku kuanzia leo kundi kubwa la wafuasi wake likitarajiwa kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.

Wema amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku 21 tangu alipotangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa ni miongoni mwa watu wanaojishughulisha na dawa za kulevya.

Taarifa za msanii huyo ambaye pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiunga na Chadema zilianza kusambaa jana baada ya kuonekana akiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, alipomsindikiza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alifika mahakamani hapo kusikiliza kesi ya kikatiba aliyomfungulia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda, akitaka chombo hicho kitamke kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.

Muda mfupi baadae Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alianza kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii juu ya kuwepo kwa shughuli ya kupokea wanachama wapya.

“Chama kupitia Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, baada ya kesi ya kikatiba namba moja ya mwaka 2017 inayotarajiwa kuwasilishwa mahakama kuu leo, kitazungumza kwa umma kupitia waandishi wa habari kuwakaribisha wanachama wapya waliojiunga leo (jana) akiwemo Wema Sepetu,” ilisema taarifa hiyo ya Makene.

Ilipofika majira ya saa 18 jioni jana, Makene aliliambia gazeti hili kwamba, wameshindwa kufanya shughuli hiyo kutokana na Mahakama Kuu kuchelewa kumaliza kusikiliza shauri hilo.

“Muda huu ndiyo tunatoka mahakamani, hatuwezi kuzungumza chochote kwa sasa ila muda wowote kuanzia kesho tutapokea wanachama wapya wakiwamo waliomsindikiza mwenyekiti mahakamani leo  na kundi jingine kubwa tu,” alisema Makene.

Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu, alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya upokeaji wa wageni wapya, alijibu kwa kifupi. “Hayo baadaye” alisema.

Kitendo cha Wema ambaye alikuwa ameandamana na mama yake mzazi kuonekana akiwa pamoja na Mbowe, kilishtua wafuasi wengi wa chama hicho waliofurika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo.

Mara kadhaa Wema alionekana akionyesha juu vidole viwili, alama ambayo ni maarufu kutumiwa na wafuasi wa Chadema.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, Wema alikuwa ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliojitokeza kuwania ubunge wa viti maalumu kupitia Mkoa wa Singida.

Katika kinyanganyiri hicho, msaani huyo alishindwa kwenye hatua za mchujo ndani ya mkoa wake baada ya kushika nafasi ya nne, akipata kura 90 huku makada wenzake  na kura zao kwenye mabano ni Aysharose Mattembe (311), Martha Mlata(235) na  Diana Chilolo (182).

Baada ya kushindwa kwenye mchujo huo, kulizuka uvumi kuwa msanii huyo angejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jambo ambalo halikutokea.

Katika kampeni za uchaguzi mkuu, Wema alikuwa ni kati ya wasanii wakubwa nchini waliokuwa wakiandamana na msafara wa viongozi wakuu kupiga kampeni kwenye maeneo mbalimbali, lengo likiwa ni kupata kura kutoka kwa vijana.

Mbali na wasanii wengine ambao waliishia kuburudisha majukwaani kabla ya viongozi wakuu kuanza kuhutubia, Wema alikuwa akifanya kampeni kwnye mtandao ya kijamii na kwenye maeneo mengine mbalimbali.

Moja ya kampeni maarufu ni ile aliyoipa jina la ‘Mama Ongea na Mwanao’ iliyolenga kushawishi vijana kuipigia CCM kura, kutokana na wengi kuonekana kushabikia zaidi upinzani kuliko chama hicho tawala.

Baada ya kwisha kwa kampeni, Wema aliendelea kuwa mwanachama wa CCM mpaka hali ilipobadilika baada ya jina lake lilipotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa ni mmoja ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Tukio la kutajwa jina lake lilitokea Februari 2 mwaka huu, ambapo baada ya kutii agizo la kwenda Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kesho yake, alishikiliwa  mpaka Februari 9, alipofikishwa kortini na kupata dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles