24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MKE WA BILIONEA MSUYA AACHIWA, AKAMATWA TENA

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru mke wa bilionea Msuya, Miriam Msuya na mwenzake, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka   (DPP) kugoma kuifanyia mabadiliko hati ya mashtaka ingawa alipewa siku tatu   kufanya hivyo.

Uamuzi huo   ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa baada ya Jamhuri kudai   kwamba hauwezi kuibadilisha hati hiyo kwa sababu  iko sahihi.

Hakimu Mwambapa aliamua kuwaachia huru Miriam na Revocatus Muyela wanaoshtakiwa kumuua kwa kukusudia dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya, Mei mwaka jana maeneo ya Kibada Kigamboni, Dar es Salaam, kwa kuwa hakuna hati inayowafanya washikiliwe kwa sababu iliyopo imebainika kuwa ni mbovu.

Wakili wa Serikali, Hellen Moshi, alidai   kesi hiyo ilikuwa inatajwa lakini mahakama ilitoa amri ya kubadilishwa   hati ya mashtaka.

“Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP), imeona hati iko sahihi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa maana hiyo hatuwezi kuifanyia mabadiliko,” alisema Hellen.

Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala akishirikiana na Wakili Faraja Mangula, alidai DPP ameonyesha jeuri na nguvu aliyonayo  lakini asingeweza kupinga amri ya mahakama.

Kibatala alidai mahakama ilishatoa amri na kuwapa muda wa siku tatu upande wa Jamhuri kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na kama wasingefanya hivyo hatua nyingine ingefuata.

“Mheshimiwa hakimu DPP ameshindwa kueleza sababu ya kutotii amri ya mahakama.

“Hivyo tunaomba washtakiwa waachiwe huru kwa sababu hakuna hati inayowashtaki. DPP ameshindwa kukata rufaa au kuomba marejeo, hivyo amepuuza amri ya mahakama,” aliomba Kibatala.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mwambapa alisema Januari 9, mwaka huu, mahakama   iliagiza hati ya mashtaka ibadilishwe kwa kuwa ni mbovu.

Alisema mahakama hiyo ilitoa muda wa siku tatu kuanzia Februari 20, mwaka huu,  kwa upande wa Jamhuri kuifanyia mabadiliko hati hiyo ya mashtaka.

“Pamoja na amri hiyo mpaka leo (jana) Jamhuri haijabadilisha hati ya mashtaka hivyo Mahakama inaona hakuna hati ya mashtaka halali inayowashikilia washtakiwa, hivyo inawaachia huru,” alisema Hakimu Mwambapa.

Baada yaa kuachiwa huru saa 3.55 asubuhi,  nje ya mahakama kulikuwa na askari waliokuwa wamevalia nguo za raia ambao waliwachukua na kushuka nao hadi mlango wa kuingilia mahabusu ya mahakama ambako kulikuwa na gari la polisi.

Miriam na wenzake walipakiwa katika gari la polisi lililokuwa na askari   na kupelekwa kituoni.

Mke wa bilionea huyo, Miriam na mfanyabiashara Revocatus Muyela, wakazi wa Arusha, wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya dada wa bilionea Msuya, Aneth Msuya.

Washitakiwa wanadaiwa Mei 25, mwaka jana, maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, kwa pamoja walimuua Aneth.  

Dada wa bilionea Msuya aliuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake.

Miriam na mwenzake walipofikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kusomewa  mashitaka, Wakili wao Kibatala, aliwasilisha maombi   akiiomba itupiliwe mbali hati ya mashitaka kwa kuwa ilikuwa na upungufu katika sheria.

Kibatala alidai hati hiyo ya mashitaka ilikuwa haijitoshelezi kiasi cha kuwawezesha washitakiwa kuelewa kile walichoshitakiwa.

Hivyo aliomba itupiliwe mbali na washitakiwa kuachiwa huru.  

Akiwasilisha majibu ya upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo, alidai hati ya mashitaka iilikuwa inajitosheleza kumwezesha mshitakiwa kuelewa kile alichoshtakiwa nacho.

Mahakama hiyo   ilikubaliana na hoja za wakili wa utetezi na kuamuru upande wa Jamhuri kufanyia mabadiliko hati hiyo. Hata hivyo, upande huo tangu ilipotolewa amri hiyo kwa mara ya kwanza haikufanya mabadiliko hayo na kutaka kuongezewa muda, hali iliyoufanya upande wa utetezi kusisitiza washitakiwa wachiwe huru. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles