25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WB: Kasi ya ukuaji uchumi hairidhishi

Na ANDREW MSECHU

BENKI ya Dunia imezindua ripoti ya Mfuko wa Afrika, ikieleza kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imekuwa   kwa kasi ndogo tofauti na matarajio.

Akizindua ripoti hiyo jana, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia kwa Afrika, Albert Zeufack alisema ukuaji huo wa  kusuasua wa uchumi umerekodiwa katika maeneo yote ingawa uchumi unaonekana kukua na kuimarika kiasi ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2015/16.

Alisema uwiano wa ukuaji huo wa uchumi unaonyesha  kumekuwa na ukuaji wa angalau asilimia 2.7 kwa mwaka huu wa 2018 ikiwa ni ongezeko dogo kutoka asilimia 2.3 mwaka jana (ambayo ni asilimia 0.4).

“Ukuaji wa uchumi katika ukanda huo wa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara unaonekana kukua kwa kasi ndogo tofauti na ilivyotarajiwa.

“Ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kasi inayotakiwa, watunga sera wanatakiwa kuangalia zaidi katika uwekezaji unaowezesha mtaji wa rasilimaliwatu, kupunguza mpangilio mbaya wa vyanzo vya uchumi na kuimarisha uzalishaji,” alisema.

Alisema  watunga sera katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo, wanatakiwa kujielekeza katika kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto mpya zinazotokana na kasi ya mabadiliko ya uchumi duniani, hasa kuhusu masuala ya uwekezaji katika vyanzo vya mitaji na kudhibiti madeni.

Zeufack alisema kasi ndogo ya ukuaji uchumi ni picha ya wazi na mazingira mabaya yanayowekwa kutoka nje.

Alisema biashara na masuala ya viwanda yameonekana kupoteza kasi yake ya awali kutokana na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa za kilimo na bidhaa za chuma kutokana na vikwazo kadhaa vinavyosababisha mahitaji ya bidhaa hizo kupungua.

Akifafanua, alisema bidhaa za kilimo na chuma ndizo zinazotegemewa zaidi na nchi hizo katika soko la imataifa, huku nchi zinazozalisha mafuta zikionekana kunufaika kutokana na ongezeko la bidhaa zao.

“Wakati bei za mafuta zikionekana kupanda tunapoelekea mwaka 2019, bei ya bidhaa za chuma zinaonekana kuendelea kubaki kama ilivyo kutokana na kupungua mahitaji yake, hasa kutokana na China kupunguza ununuzi.

“Msukumo wa soko la fedha pia umekuwa ukikandamiza nchi zinazojitahidi kukua katika iuchumi na kupanda kwa thamani ya dola kunazikandamiza zaidi nchi zenye madeni makubwa,” alisema.

Alieleza kuwa ukuaji huo mdogo wa uchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (unaofikia asilimia 0.4 kwa mujibu wa rekodi ya Aprili mwaka huu) unarekodiwa kwa kuangalia ukuaji wa nchi zinazoongoza katika uchumi kwa Afrika, ambazo ni Nigeria, Angola na Afrika Kusini.

Zeufack alisema kushuka uzalishaji wa mafuta  Angola na Nigeria kumekuwa chanzo cha kupanda  bei ya mafuta na kwa Afrika Kusini, kushuka kwa mahitaji ya majumbani kumechukuliwa kama rekodi ya kushuka   bei ya bidhaa za kilimo.

Alisema katika nchi ambazo hazina rasilimali nyingi kama ilivyo   Ivory Coast, Kenya na Rwanda, shughuli za uchumi zimeendelea kuimarika kwa kutegemea kilimo na utoaji wa huduma katika maeneo ya uzalishaji mali, pia katika matumizi ya majumbani na uwekezaji wa umma katika sehemu zenye mahitaji.

Alieleza kuwa deni la taifa limeendelea kukua katika nchi nyingi na kutokana na kushuka  thamani ya fedha katika nchi nyingi, ongezeko la faida inayotokana na deni hilo limeendelea kuwa kubwa na kuziweka katika hali mbaya nchi nyingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles