Donald Trump na familia yake wachunguzwa kukwepa kodi

0
870

WASHINGTON, MAREKANI

MAOFISA katika jimbo la New York nchini hapa wamesema wamelazimika kuchunguza madai kuwa Rais Donald Trump alisaidia familia yake kukwepa kodi ya mamilioni ya dola katika miaka ya 1990.

Ripoti iliyochapishwa na gazeti la New York Times imemshutumu Trump kwa kuhusika na mpango wa ulipaji kodi, ubabaishaji pamoja na udanganyifu ili kuficha makadirio yanayomhusu yeye pamoja na ndugu na wazazi wake.

Ikulu ya White House imetupilia mbali madai hayo kuwa ni ya upotoshaji.

Msemaji wa White House, Sara Sanders ameongeza kusema malipo yote yalikuwa yakikaguliwa na kupitishwa na mamlaka za kodi kwa miaka mingi iliyopita.

Trump bado hajasema lolote kuhusu madai hayo, lakini mwanasheria wake Charles Harder amekana vikali mteja wake kutenda kosa lolote.

Alisema hakuna udanganyifu au ukwepaji wa kodi uliofanywa na yeyote na kusema taarifa ambazo gazeti la New York limeegemea ni za uongo na zisizo sahihi.

Gazeti hilo katika taarifa yake limesema pamoja na kuwa Trump amekuwa akijinadi kuwa ubilionea wake unatokana na jitihada zake binafsi, lakini amekuwa akipokea mamilioni ya dola kutoka rasilimali za wazazi wake tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.

Limesema katika umri wa miaka mitatu alikuwa na mapato yapatayo dola 200,000 kwa mwaka kutoka rasilimali za wazazi wake na baadae akawa milionea akiwa na umri wa miaka minane.

Gazeti hilo limekwenda mbali zaidi na kusema fedha nyingi alizipata kutokana na kuwasaidia wazazi wake kukwepa kodi.

Limesema yeye na ndugu zake waliunda kampuni bandia na kujipatia mamilioni ya dola kama zawadi kutoka kwa wazazi wake.

Wakati huo huo, mke wa Rais Trump, Melania Trump ametembelea eneo lililokuwa likishikilia watumwa nchini Ghana.

Aliita ziara yake ya jana katika ngome hiyo ya Cape Coast yenye hisia na kitu ambacho watu wanapaswa kukiona na kushuhudia, akisema ni mahali maalumu.

Melania alitumia saa moja katika ngome hiyo ya karne ya 17, ambako watumwa walishikiliwa kabla ya kuvushwa katika Bahari ya Atlantic.

Mke huyo wa Rais anaitembelea Afrika kwa mara ya kwanza na amepanga kuzuru pia Malawi, Kenya na Misri.

Melania anaangazia zaidi masuala ya afya na elimu kwa watoto na wanawake katika harakati za kuimarisha baadhi ya migawanyiko inayoshuhudiwa katika jamii.

Ziara hii inafuatia matamshi anayodaiwa Trump alitoa faraghani dhidi ya mataifa ya Afrika mwezi Februari mwaka huu.

Trump alishutumiwa kwa ubaguzi wa rangi baada ya kuripotiwa kwa kutumia neno ‘shimo la choo’ kuangazia mataifa ya Afrika akizungumzia sera ya uhamiaji.

Muungano wa Afrika ulimtaka aombe radhi kwa kutoa kauli hiyo.

Baadaye aliwaambia wanahabari; “mimi si mbaguzi mkinilinganisha na mtu mwingine yeyote mbaguzi ambaye mshawahi kumhoji.”

Agosti mwaka huu Trump aliikasirisha Serikali ya Afrika Kusini kwa kudai kwamba kuna mauaji makubwa ya wakulima wenye asiili ya kizungu nchini humo.

Haijabainika ikiwa Trump ashawahi kuzuru bara la Afrika kabla kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here