24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

Kufutwa matokeo darasa la saba balaa laibuka

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SIKU moja baada ya Baraza la Mitihani Tanzania kutangaza kufutwa matokeo ya darasa la saba kwa shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, shule nane za Dar es Salaam, Mwanza na Kondoa, Serikali imetangaza kuwavua madaraka waratibu wa elimu wa kata watano.

Uamuzi huo umetolewa  baada ya kubainika kujihusisha na njama za udanganyifu na kusababisha kufutwa mitihani ya baadhi ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba wilayani Chemba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alisema  uongozi wa mkoa umesikitishwa na tukio hilo na hivyo kuamua kuchukua hatua ya kuwasimamisha kupisha uchunguzi.

Dk. Mahenge alieleza kuwa jambo hilo pia  limeisababiashia serikali hasara kubwa kwa kuingia gharama za kurudia mitihani hiyo.

“Nawaagiza wazazi na kamati za mitihani kuhakikisha watoto wote popote walipo wanarejea katika maeneo yao kwa wakati iwaweze kufanya mitihani hiyo.

“Najua baada ya kumaliza shule wapo waliotawanyika hivyo naagiza warejee  na wote wapatikane na kufanya mtihani,”alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilayaya Chemba, Dk. Semistatus Mashimbe, aliyataja majina ya waratibu waliosimamishwa na kata zao kwenye mabano kuwa ni Hussein Waziri (Goima), Deo Philip (Farkwa), Yona Koki (Paranga), Ruta Rutaigwa (Chemba) na Gido Bulaya (Churuku).

Walimu wakuu waliosimamishwa na shule wanazotoka katika mabano ni Noela Chambo (Farkwa), Jicho Mohamed (Kinkima), Joseph Mvula (Mugunika), Abdul Idrissa (Chemba) na David Kihumba (Makamaka).

Alisema licha ya hatua hizo bado uchunguzi unaendelea na hatua zaidi zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alisema  wilaya hiyo ina shule za msingi 103 ambako wanafunzi wa darasa la saba walikuwa 5,362 huku waliofanya mtihani wakiwa ni 5,171.

“Kwa maana hiyo wanafunzi 5,171 watarudia mtihani huo na sisi tupo tayari kusimamia na kuhakikisha wanafanya mtihani huo,”alisema.

DC ANENA

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, akizungumzia  mtandao wa WhatsApp uliotumiwa na walimu hao kuvujisha majibu, alisema  walimu walitumia mbinu hiyo kukwepa hatua za nidhamu ambazo zingechukuliwa endapo wilaya hiyo ingeshika nafasi ya mwisho kwenye matokeo ya darasa la saba.

“Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, Wilaya ya Chemba  ilishika nafasi ya mwisho kwenye matokeo lakini katika mtihani wa mwaka huu, ufaulu uliongezeka kwa asilimia 70 jambo ambalo si rahisi kufikiwa,” alisema.

Odunga alisema siku ya pili wakati mtihani huo ukiendelea kuliibuka tetesi za kuwapo njama za uvujishaji majibu ya mitihani kupitia makundi ya mtandao wa jamii wa WhatsApp

“Tarehe 6 asubuhi kuliibuka tetesi na fununu kwamba kuna dalili za udanganyifu katika Shule ya Farkwa. Kamati ya mitihani ilichukua hatua za haraka kufika shuleni na  kukamata na kuwapekua   wahusika wote waliokuwapo katika lile eneo na ndipo ilipobainika ulikuwa ujumbe kwenye simu ulioonyesha kana kwamba yale ni majibu ya mitihani.

“Kamati ya mitihani ikawasiliana na vyombo husika na kukamata wahusika waliobainika na simu zao zikakusanywa na haraka sana wakawasiliana na kamati ya mitihani ya mkoa na yenyewe wakachukua hatua za haraka kufika eneo la tukio.

“Mawasiliano yote yalikuwa yakifanyika kupitia makundi ya whatsap ya waratibu elimu na wakuu wa shule. Walitumia kundi hilo vibaya,” alisema Odunga.

Alisema suala hilo limeanzia kwenye kamati  ya mitihani hivyo anashukuru hatua zilizochukuliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba, Dk. Semistatus Mashimbe.

“Oktoba 1 mwaka huu aliwasimamisha waratibu elimu wa kata watano na walimu wakuu wanne.

“Juzi, Tamisemi ilitengua uteuzi wa Kaimu Ofisa Elimu Msingi, Modest Tarimo na Ofisa Taaluma Msingi, Ali Akida na uchunguzi unaendelea,” alisema.

MBUNGE NKAMIA

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alisema    tukio hilo ni la aibu na halijawahi kutokea kwenye historia ya wilaya hiyo.

Alimshukuru  ofisa usalama wa wilaya hiyo kwa kuweza kuligundua jambo hilo.

“Watendaji wanajaribu kutafuta sifa kwa njia za ujinga. Wilaya haijawahi kuwa na kashfa kama hii tangu uhuru.

“Mwaka juzi na jana ufaulu ulifikia asilimia 52 lakini kwenye matokeo ya mwaka huu umefikia asilimia 71 jambo ambalo si rahisi.

“Narudia kusema tena tumejaribu kutafuta sifa za ovyo kwa mambo ya ovyo kama wanaonyesha mitihani halafu wanajisifia, haya ni mambo ya ovyo.

“Baadhi ya watu walikuwa wanatafuta sifa za ovyo,” alisema Nkamia.

WAZAZI WAINGIWA HOFU

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wazazi walisema   wanafunzi wanaotakiwa kurudia mtihani huo walisema taarifa hizo wamezipokea kwa masikitiko na  wana wasiwasi kama watoto wao wataweza kufanya vizuri katika mtihani huo.

Hassan Sogoi, mkazi wa Kijiji cha Kambi ya Nyasa, alisema mtoto wake, Zawjat Hassan alifanya mtihani katika Shule ya Msingi Kambi ya Nyasa, hivyo   kufutwa kwa matokeo hayo ni pigo kubwa kwao.

“Wazazi mwanzo tulichanga tukawanunulia sola kwa ajili ya kusomea, pia tulichanga kwa ajili ya kuwapatia chakula na fedha kwa ajili ya mpishi na mlinzi kwa ajili ya kuwalinda kwa sababu  waliweka kambi hapa na walikuwa wakisoma kwa pamoja,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles