23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

‘WAZUNGU WA UNGA’ WALIOZIKWA KWENYE MAKABURI YENYE KIYOYOZI, YASIYOPENYA RISASI

8UNAPOYATAZAMA utadhani ni magorofa ya kifahari, ambayo watu wengi wangetamani kuishi, lakini wasifanikiwe.

Lakini nchini Mexico, ambako biashara ya mihadarati imekithiri, wakuu wa magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya huishi maisha ya kifahari, na huendelea hata wanapokuwa wafu.

Nchini humo, utakutana na makaburi yao kama picha zinavyoonesha, ambayo yangegeuzwa kuwa nyumba, matajiri wengi bado wangejivunia kuishi humo.

Ni makaburi makubwa yaliyojengwa na kuwekwa huduma za kisasa na vitu vingi vya anasa.

Kuna baadhi ya makaburi yenye viyoyozi vya kudhibiti viwango vya joto na kuingiza hewa safi, kuna vioo visivyopenya risasi na baadhi yana hata vyumba ambavyo wageni wanaofika kutoa heshima kwa wafu, wanaweza kuketi na kupata kila kitu kinachopatikana katika nyumba za kifahari.

Baadhi yanakadiriwa kugharimu hadi pauni 230,000 za Uingereza sawa na Sh milioni 633 za Tanzania.

Hali hii ni tofauti kabisa kwa maelfu ya watu wanaouawa katika makabiliano ya magenge ya ulanguzi wa dawa hizo za kulevya ambao sana huzikwa katika makaburi ya pamoja au miili yao kutungikwa na kuachwa ikiwa imening’inia kwenye madaraja.

Ni mwongo mmoja sasa tangu serikali ya Mexico ilipotuma wanajeshi wake kwenda kukabiliana na magenge ya walanguzi.

Lakini walanguzi wakuu, ambao wamejipatia fedha nyingi, wanaweza kupamba makaburi yao kutokana na fedha hizo walizolimbikiza kwa biashara hiyo.

Makaburi mengi haya hupatikana jimbo la Sinaloa, anamotoka bwana unga mkuu duniani kwa sasa, Joaquin “El Chapo” Guzman ambaye kwa sasa anazuiliwa na anatarajiwa kuhamishiwa Marekani mwakani.

Katika eneo moja la makaburi, Jardines del Humaya, katika mji mkuu wa jimbo la Culiacan, ndipo unapokutana na baadhi ya makaburi ya kupendeza zaidi.

“Ni ishara ya nguvu na mamlaka ambayo wakati mmoja walikuwa nayo na ni ishara ya matamanio yao ya kutaka kuishi daima, jambo ambalo ni kawaida kwa binadamu yeyote yule,” anasema Juan Carlos Ayala, profesa wa falsafa katika chuo kikuu cha Autonomous University cha Sinaloa ambacho huangazia sana utamaduni wa ulanguzi wa dawa.

“Pia ni onesho kwa wale ambao wanaendelea kuishi kwamba mtu huyu alikuwa mtu mashuhuri.”

Mwendelezo wa filamu za Netflix, Narcos, umekuwa ukitoa kidokezo kwa wengi duniani kuhusu maisha yalivyo kwa walanguzi wa mihadarati.

Lakini nchini Mexico, serikali inatafakari uwezekano wa kupiga marufuku filamu kama hizo, kama njia ya kuwazuia watoto kutazama maisha ya ulanguzi wa mihadarati kama ya kuvutia.

“Ulanguzi wa mihadarati unachochea jamii, kupitia utamaduni, na sasa tuna tatizo la kutazama umeanzisha wapi na umefikia mwisho upi,” alisema Ayala.

Kaburi moja ambalo linadaiwa kuwa na mwili wa mlanguzi aliyetumiwa kuua watu, lina hata kamera za kiusalama, pamoja na kioo kisichopenya risasi.

Lina pia kuba lenye taa ambazo huwaka. Ndani kuna visu vinne vilivyofungiwa kwenye kijisanduku kilichoundwa kwa vioo.

Baadhi ya makaburi yamejengwa kama nyumba za kisasa au makanisa madogo. Krismasi inakaribia, na baadhi hata yamewekewa miti bandia ya Krismasi.

Lakini kinachokosekana katika makaburi mengi ni utambulisho wa aliyezikwa ndani.

Santa Muerta, mtakatifu wa kifo, ambaye hatambuliwi na Kanisa Katoliki la Kirumi, hutukuzwa sana na mamilioni ya watu Mexico, wakiwemo wahalifu.

“Kuna mchango mkubwa wa dini katika utamaduni wa ulanguzi wa dawa, kwa sababu iwapo kuna mtu anayehitaji sana ulinzi kutoka kwa miungu au Mungu, basi ni mlanguzi wa mihadarati ambaye anaweza kuuawa kwa kupigwa risasi na magenge hasimu au maafisa wa serikali wakati wowote,” anasema Andrew Chesnut, mwandishi wa kitabu kinachokwenda kwa jina la Devoted to Death: Santa Muerte, the Skeleton Saint (Kujitolea kwa Kifo: Santa Muerte, Mtakatifu wa Kiunzi cha Mifupa).

Makala haya yameandikwa kwa hisani ya BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles