AOA MDOLI KWA HOFU YA KUFA MAPEMA

2KIJANA mmoja nchini China, ambaye jina lake halijawekwa wazi kutokana na sababu maalumu amewaacha wengi kinywa wazi.

Mkazi huyo wa Beijing, mwenye umri wa miaka 28 tu, sura na umbo lenye mvuto linaloweza kunasa au kuwa chaguo la wanawake wengi halisi warembo badala yake aliamua kufunga ndoa na mdoli.

Licha ya kwamba mdoli huyo ana mvuto, kwa wale ambao hawafahamu nini kimemsibu kijana huyo hadi kufikia kuchukua hatua hiyo walikuwa na haki ya kumshangaa kwa uamuzi wake huo.

Lakini ni kitu gani hicho kilichomsibu na kuchukua uamuzi huo wa kushangaza tena kwa kijana wa haiba yake?

Ni kutokana na ukweli kuwa kijana huyo anafahamu fika kuwa hana muda mrefu wa kuishi hapa duniani.

Kufunga ndoa tena na mwanamke halisi mrembo ni kitu alichotamani sana kijana huyu.

Lakini bahati mbaya sana, amegundulika kuwa na maradhi yanayomtafuna ndani kwa ndani ya saratani, ambayo yamefikia hatua mbaya ya kutotibika na hivyo kufupisha maisha yake.

Na moja kwa moja maradhi hayo yameharibu kikatili ndoto yake hiyo.

Kutokana na sababu hiyo, ili kuitimiza ndoto kwa namna nyingine na angalau kupata faraja ya rohoni japo kidogo kabla hajafa na wakati huo huo kutoacha maumivu makubwa ya kipindi kirefu kwa mjane ambaye angekuwa mkewe, suluhu aliyoiona ni kuoa kitu kisicho halisi.

Kwamba aoe mdoli na ikatokea yeye akafariki dunia kwa maradhi hayo katili, hakuna maumivu, ambayo atamsababishia mwanamke husika.

Inaweza kuwa kioja, lakini ndio ukweli na picha zinaonekana kama sherehe nzuri na kijana aliweza kufarijika japo si kwa namna ile ambayo angependa.

Mdoli huyo alimnunua kwa gharama ya pauni za Uingereza 5,000 sawa na Sh. milioni 15 za Tanzania.

Alimvalisha nguo za harusi mkewe huyo wa plastiki, alimshika mkono, alimbusu, alicheza naye muziki na kufuata hatua zote kama maharusi halisi.

Picha zake zilitawala katika mitandao wakati tukio hilo lilipotokea mwaka jana, mdoli akionekana amevalia shela jeupe la gharama kubwa huku akipiga magoti mbele yake.

Picha nyingine zilionesha mdoli akiwa amevalia vazi la pinki huku mumewe huyo amesimama nyuma yake akiwa amemshika kiunoni na nyingine ya staili kama hiyo akiwa kashikilia shada la maua.

Wakati picha hizo zilipoonekana mitandaoni, watu waligawanyika kuhusu uamuzi huo wa kushangaza uliochukuliwa na kijana huyo.

Wakati baadhi wakiamini kuwa picha hizo zinaweza kuwa kampeni fulani ya kukuza soko la midoli, lakini ukweli ni kwamba mwanaume huyo alidhamiria na kitu hicho ili kupata faraja kabla hajafa.

Aidha mpiga picha wa harusi hiyo alimtetea mwanaume huyo kijana kutokana na madhila yanayomkabili kuwa anapaswa kuheshimwa kwa uamuzi aliochukua na pia ni suala la uhuru wake binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here