Waziri Mkuu Papua New Guinea ajiuzulu

0
442

PORT MORESBY, PAPUA NEW GUINEA

WAZIRI Mkuu Peter O’neil amelazimika kujiuzulu, kufuatia wiki kadhaa za wanachama wa ngazi za juu wa chama kinachotawala nchini hapa kuhamia vyama vingine.

Kupitia taarifa iliyowasilishwa kwa njia ya barua pepe, O’neill ambaye amehudumu katika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa miaka saba, alitangaza kujiuzulu juzi na amekabidhi mamlaka kwa aliyekuwa waziri mkuu wa kisiwa hiki kilichopo bahari ya Pacific ya Kusini, Julius Chan.

Katika taarifa hiyo, O’neill aliongeza kwamba ni matumaini yake hatua hiyo italiwezesha taifa hili kuuimarisha mchakato ambao umekuwa ukiendelea wa ajenda ya mageuzi ya kisiasa.

Shirika la Habari la Uingereza – Reuters liliripoti kwamba misukosuko ya kisiasa ni jambo la kawaida katika kisiwa hiki  chenye ukwasi wa rasilimali, lakini pia kinachokumbwa na umasikini mkubwa.

O’neill alikuwa akikabiliwa na shinikizo la kuondoka madarakani kwa muda sasa, kufuatia shutuma mbalimbali, ukiwemo ufisadi.

Umaarufu wake ulionekana kutikisika Ijumaa iliyopita wakati wanachama tisa, wakiwemo mawaziri wawili, walipokihama chama kinachotawala.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here