23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu awaonya vijana wanaotumia TEHAMA kutapeli

Na Mwandishi Wetu, Dodomo

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi hasa vijana wajiepushe na matumizi yasiyo sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama vile wizi na utapeli wa fedha unaofanywa kwa njia ya mtandao.

Majaliwa ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2021, alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa katika Viwanja vya Mazaina wilayani Chato, Geita yenye kaulimbiu isemayo ‘TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu; Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji’ ambapo pia  amezindua Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Tanzania (TAUTA).

Majaliwa amesema vijana wajiepushe na matumizi mabaya ya TEHAMA ikiwamo kujiunga na makundi yasiyofaa, kujiingiza kwenye majukwaa ya uchochezi kwani vitendo hivyo vinavuruga amani, utulivu na mshikamano wa Taifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Elisha Kato ambaye ni Mbunifu wa Mfumo wa Kudhibiti mwendo kasi katika magari, wakati alipotembelea mabanda katika uzinduzi wa wiki ya vijana kitaifa Chato, Geita Oktoba 12, 2021.  Wapili kulia ni Mbunifu Mwenza wa Mfumo huo Ronaldo Joseph.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru vifanyike katika wilaya ya Chato mkoani Geita ili kumuenzi muasisi wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere ambaye alitoa mchango mkubwa katika kulikomboa Taifa akiwa kijana. 

“Kutokana na umuhimu huo Serikali imesisitiza matumizi sahihi ya TEHAMA kwenu vijana kwani ninyi ndio watumiaji wakubwa na wahanga wakubwa wa TEHAMA. Ni ukweli usiopingika kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.

“Vijana wengi wamefanikiwa kutokana na matumizi sahihi ya TEHAMA hususan kwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao. Vijana wameweza kuanzisha na kuendesha vituo vya huduma za intaneti na pia kuanzisha wakala wa huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu.

“Hivyo, tukitumia fursa hizi vizuri na maendeleo ya TEHAMA tuliyonayo, tutasonga mbele kwa kazi kubwa zaidi. Tunayo mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, tumieni fursa hizo za mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri zetu kuwekeza katika miradi yenye tija kwa maendeleo yenu,”amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Elisha Kato ambaye ni Mbunifu wa Mfumo wa Kudhibiti mwendo kasi katika magari, wakati alipotembelea mabanda katika uzinduzi wa wiki ya vijana kitaifa Chato, Geita Oktoba 12, 2021.  Wapili kulia ni Mbunifu Mwenza wa Mfumo huo Ronaldo Joseph

Aidha amewataka vijana watumie fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira inayoikabili dunia kwa sasa.

“Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini pia tunayo fursa ya uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani,”amesema.

Majaliwa amewasisitiza vijana watembelee kwa wingi banda la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Foundation) lililopo katika maonesho hayo ili wakajifunze kupitia historia ya baba wa Taifa umuhimu wao kama vijana wa Tanzania katika kujenga misingi ya uzalendo, uwajibikaji na ujenzi wa Taifa.

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo kuhifadhi kumbukumbu ya historia na kazi za Baba wa Taifa.

 Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema katika wiki hiyo ya vijana kitaifa imewawezesha vijana kufanya tafakuri ya kina kuhusu falsafa juu ya maono ya Baba wa Taifa kupitia kazi alizozifanya kwa Watanzani.

Waandamaji wakipita mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika uzinduzi wa wiki ya vijana kitaifa katika Uwanja wa Mazaina Chato, Geita.

Kwa upande wake, Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tabia Maulidi Mwita, amesema kuwa wizara hiyo itashirikiana na vijana wate nchini wakiwamo walioshiriki maonesho hayo katika kuulinda na kuudumisha Muungano kwani una faida kubwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda amesema wiki ya vijana imeanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha na kuwapa nafasi vijana na wadau wa shughuli za maendeleo yao na kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali yanayowahusu kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Amesema maadhimisho hayo ambayo yalianza Oktoba 8, 2021 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 yamehudhuriwa na vijana zaidi 1,000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles