22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri: Marufuku Kuchati ofisini

Profesa Makame MbarawaNA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

WAFANYAKAZI wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wamepigwa marufuku ‘kuchati’ katika mitandao ya jamii kwa kutumia simu wawapo maofisini.

Amri hiyo ilitolewa jana na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa alipokutana na wafanyakazi wake kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Alisema watakaobainika kutumia muda wa kazi ‘kuchati’ katika mitandao hiyo watatumbuliwa majipu bila kuonewa haya.

Profesa Mbarawa aliwataka wafanyakazi wa wizara yake kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuacha tabia ya kuchelewa kuripoti ofisini, na kutumia muda mwingi katika mitandao ya jamii na kupiga porojo.

“Kuna tabia ya wafanyakazi kuwasili ofisini hadi saa nane mchana, kisha wanazama kwenye porojo na kutumia muda mwingi katika mitandao ya jamii na matokeo yake muda wa kazi unaisha wakiwa hawajafanya lolote kiuzalishaji. Tabia hii ikome mara moja,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema kwamba kwa wale wanaojiona hawawezi kuendana na kasi ya Serikali ya sasa kwa kuendekeza kufanya kazi kwa mazoea, wajiondoe ili kupisha vijana wengine wengi ambao wamesoma lakini wamekosa ajira.

“Suala la ufisadi na ujanjaujanja katika wizara hii halina nafasi, vinginevyo tutakuja kutumbuana majipu, ninachohitaji kazi zifanyike kwa weledi ili ifikapo mwaka 2020/25 tuhakikishe tumewajengea wananchi miundombinu ya kisasa,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema tatizo lililozoeleka katika Serikali ni watu kupeana ajira kwa kujuana na wanaona kuwa ni sifa kufanya hivyo, kitu ambacho kwa Serikali ya sasa hakikubaliki.

Profesa Mbarawa alisema wizara yake imeamua kupeana malengo na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), hivyo kila kiongozi anatakiwa kuwajibika ili ifikapo mwisho wa mwaka kila mmoja awe amefikia malengo yake  na akishindwa watamuondoa mana hafai.

Pia aliwataka viongozi wa juu wizarani kushirikiana na wafanyakazi ili kuweza kufikia malengo na kuboresha mazingira ya kiuchumi.

Aidha Profesa Mbarawa alisema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia namba zake za simu kufanya utapeli, hivyo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo.

“Watu hao waache tabia hiyo, la sivyo tutawakamata na tutawachukulia hatua kali za kisheria. Pia namba zangu zisitumike kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) kuomba michango ya harusi, bali utumwe ujumbe wa kazi tu,” alisema Profesa Mbarawa.

Kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano duniani, Watanzania wengi hususani vijana wamekuwa wapenzi wakubwa wa mitandao ya jamii kupitia simu za mkononi na kompyuta kwa kuamini kuwa ndimo wanapata taarifa mbalimbali za ulimwengu wote.

Zuio hilo la waziri linatarajia kuzua maswali mengi kuliko majibu hasa ikizingatiwa suala la mawasiliano ya simu na mtandao ni mtambuka zaidi ambapo ikitumiwa vizuri inaweza kurahisisha shughuli mbalimbali.

Matumizi ya huduma ya mawasiliano nchini yamekua kwa kasi katika siku za hivi karibuni ambapo Watanzania wengi hivi sasa wanafaidika kwa matumizi mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii kama vile Facebook, WhatsApp, Twitter, BBM, LinkedIn na blog.

Mitandao ya kijamii pamoja na mambo mengine, inawanufaisha Watanzaia walio wengi kwani ni fursa murua ya kujifunza, kupata habari mpya na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani.

Hata hivyo pamoja na maendeleo haya, kumekuwapo na baadhi ya wafanyakazi wanaotumia mitandao hii, mawasiliano ya simu na mawasiliano mengine katika muda ambao wanatakiwa kuzalisha au kutoa huduma, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,205FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles