22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aonya walionunua nyumba za Serikali

mbarawaNa Asifiwe George, Dar es Salaam

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewapa mwezi mmoja wale wote wanaodaiwa kutokana na kukopa nyumba za Serikali walipe mara moja vinginevyo wazisalimishe serikalini.

Mbali na hilo, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuzingatia thamani ya fedha kwa kila mradi wa ujenzi wa nyumba wanaoutekeleza nchini.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa wafanyakazi wa wizara hiyo, huku akionya iwapo hawatarejesha fedha hizo atawatangaza mmoja mmoja katika vyombo vya habari kabla ya kuwanyang’anya.

“Kama unajijua umekopa nyumba ya Serikali na umeshindwa kuilipia ndani ya mwezi huu, ondoka mara moja katika makazi hayo maana sitakuwa na muda wa kukusikiliza. Tunahitaji fedha ili ziweze kufanya shughuli nyingine za kiuchumi,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema zipo fedha nyingi ambazo bado hazijarejeshwa kupitia kwa wakopaji hao wa nyumba huku serikali ikishindwa kufanya shughuli nyingine za kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.

Profesa Mbarawa alisema kodi zinazokusanywa hazitoshi kuboresha miundombinu kwa ubora unaotakiwa, hivyo kila kiongozi  anatakiwa kusimamia majukumu yake ili zipatikane fedha za kujenga nyumba nyingine bora.

Alimwagiza Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga kuhakikisha wapangaji wote wanaoishi kwenye nyumba za wakala huo wanalipa kodi zote kwa wakati na watakaoshindwa wahame mara moja.

“Natoa mwezi mmoja kwa watumishi ambao hawajalipa watafute sehemu nyingine ya kukaa, ili wakala apangishe nyumba hizo kwa anaeweza kulipa kwa wakati,” alisema Profesa Mbarawa.

Uuzaji wa nyumba za Serikali ulitekelezwa katika uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na nyumba zaidi ya 8,000 ziliuzwa, baadhi zikiwa zimejengwa katika maeneo nyeti.
Ilidaiwa  Rais Dk. John Magufuli, wakati akiwa Waziri wa Ujenzi aliingilia mchakato wa uuzaji wa nyumba hizo ambao unatajwa ulipaswa kusimamiwa moja kwa moja na TBA, jambo ambalo lilizugua gumzo.

Uuzwaji huo wa nyumba hizo, unalalamikiwa na wananchi hadi leo kutokana na mchakato huo kuhusisha nyumba za Serikali zilizokuwa katika maeneo nyeti na kusababisha watumishi wengi wa Serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha za walipa kodi kuishi hotelini.

Kilio hicho cha wananchi kilikwenda mbali zaidi kwa kuweka matumaini makubwa kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati anaingia madarakani mwaka 2005 huenda  angeweza kubatilisha uamuzi wa mtangulizi wake kwa kuzirudisha nyumba zote za serikali zilizouzwa kwa bei ya kutupwa.

Chini ya sheria ya Executive Agency Act No. 30 ya mwaka 1997, TBA ilipewa mamlaka ya kuuza nyumba za Serikali, kujenga nyumba mpya, kukarabati zilizopo pamoja na kugawa nyumba za madaraja A, B na C kwa wafanyakazi wa serikali na si Waziri wa Ujenzi wa wakati huo.

Sheria hiyo, inaipa mamlaka ya kipekee TBA ya kufanya shughuli zote bila kuingiliwa na chombo chochote.
Kwa sheria hiyo, waziri mwenye dhamana anaruhusiwa kuteua wajumbe wa bodi ya ushauri watakaomshauri Katibu Mkuu wa Wizara juu ya namna nzuri ya TBA kusimamia mamlaka yake.

Katika mauzo hayo ya nyumba, Serikali ilitarajia kupata Sh 60,016,556,439.00, lakini taarifa zikionyesha ilipata Sh 22,684,108,115.08.

Miongoni mwa nyumba zinazomilikiwa na Serikali hadi sasa ni 1,098 zinazosimamiwa na TBA, kati ya hizo, 692 zimetengwa kwa wafanyakazi wa Serikali, 675 kama tied quarters, 111 zinatumika kama Rest House za Serikali, wakati nyumba 40 zinatumika kama state lodges. Nyumba 24 zinatumika kama ofisi na nyingine 29 kama karakana na bohari.

Katika bajeti ya mwaka 2010/2011, Wizara ya Ujenzi iliwasilisha bajeti yake bungeni mjini Dodoma na kueleza  inatarajia kutumia takriban Sh bilioni 5.7 kujenga nyumba mpya ili kuokoa mamilioni yanayotumika kuwalipia kodi watumishi wanaolazimika kukaa hotelini kwa kukosa nyumba.

Hata hivyo, kiasi hicho cha fedha kilichotengwa wakati huo kilitajwa kuwa pungufu ikilinganishwa na kile kilichotengwa awali, katika bajeti iliyotangulia ya 2009/2010, Sh bilioni 11.4 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo wa nyumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles