25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi jipya kuundwa kukabili ujangili

Profesa Jumanne MaghembeNA MASYAGA MATINYI, SERENGETI

SERIKALI itaunda jeshi jipya la kupambana na ujangili nchini kuanzia mwaka 2017, imefahamika.

Akizungumza katika mahojiano juzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema uamuzi huo unatokana na kuongezeka kwa kasi vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori.

Alisema jeshi hilo jipya litapewa hadhi sawa na majeshi mengine ya ulinzi na usalama, ikiwamo kuboresha uwezo, vitendea kazi, posho na marupurupu mengine.

“Kuanzia mwakani hakutakuwa tena na kikosi cha kupambana na ujangili au askari wa wanyamapori (rangers), tunaenda kuunda jeshi kamili na la kisasa ili kukabiliana na majangili ambao wanamaliza wanyamapori wetu.

“Askari wa jeshi hili watapewa mafunzo maalumu na tutahakikisha wanatumia zana za kisasa za kivita, pia tutaangalia upya mafao yao na marupurupu mengine ili kuwapa motisha kutokana na changamoto kubwa iliyopo mbele yao.

“Kwahiyo hata wenzetu ambao walikuwa wakishauri tuajiri askari wa wanyamapori kutoka maeneo zilizopo hifadhi na mapori ili wafanye kazi katika maeneo yao kama njia mojawapo ya kuzuia ujangili, ushauri huo kwa sasa hauwezekani.

“Kwa lugha rahisi tutaunda jeshi lenye sura ya kitaifa, kitu ambacho ni sifa namba moja ya jeshi lolote lile, hatuwezi kuwa na jeshi mathalan la Wamasai na Wakurya pekee, kwa sababu tu hifadhi zipo katika maeneo yao,” alisema.

Kwa kipindi kirefu Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na asasi zilizopo chini yake, imekuwa ikipambana na vitendo vya ujangili, lakini vimeendelea kushamiri.

Miongoni mwa matukio makubwa yaliyofanywa hivi karibuni, ni kuangushwa kwa helkopta ya doria ya wanyamapori na majangili katika Pori la Akiba la Maswa lililoko Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kumuua rubani wake, Roger Gower raia wa Uingereza.

Baada ya tukio hilo, Serikali ilisema kwamba kwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola na vya ulinzi na usalama, inaanzisha mkakati mpya wa kupambana na ujangili na uwindaji haramu wa maliasili, ikiwamo tembo ambao ni rasilimali muhimu kwa Taifa.

Tukio hilo lilikuwa la kwanza katika historia ya uhifadhi nchini, kwa majangili kushambulia helkopta ya doria na kusababisha mauaji ya rubani.

Miongoni mwa hatua ambazo tayari Serikali imechukua ni pamoja na majaribio juu ya matumizi ya ndege maalumu zisizo na rubani, maarufu kama Drone, zitakazotumika kwa ajili ya doria katika mbuga na misitu mbalimbali ya hifadhi nchini.

 

UWINDAJI WA KITALII DHIDI YA SIMBA

Kuhusu kuendelea kupungua kwa idadi ya simba katika hifadhi na mapori mbalimbali nchini, Waziri Maghembe alisema Serikali tayari imeanza kuchukua hatua kadhaa kukabiliana na tishio hilo.

Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha Tanzania ina jumla ya simba 16,000, na kutajwa kuwa ndiyo yenye idadi kubwa ya wanyama hao kuliko nchi yoyote duniani.

“Ukweli ni kwamba simba ni wachache sana, hata hivyo hivi tunavyozungumza kuna sensa ya simba inaendelea ili kufahamu kwa sasa tuna simba wangapi.

“Hivyo hata huu uwindaji wa kitalii dhidi ya simba tutauangalia upya 2016/17 kama una manufaa kwa uhifadhi kwa kuzingatia hali halisi tuliyonayo, haiwezekani ‘business as usual’ kuendelea, simba watakwisha.

“Unajua wawindaji huwinda simba dume wazee ambao meno yao yameshakuwa marefu kulinganisha na simba wengine, sasa unakuta simba anayeuawa ndiye baba wa familia.

“Kwahiyo ukimuua, lazima atakuja simba dume mwingine kurithi ile familia, na ili na yeye aanzishe familia yake, ni lazima ataua watoto aliowakuta ilia apate fursa ya kuzaa watoto wake.

“Kwahiyo mnaua simba mmoja, lakini matokeo yake kifo cha simba mmoja kinazaa vifo vya simba wengine 12. Pia simba wazee hawawezi kuwinda, hivyo kujikuta wakilazimika kuingia vijijini na kuua mifugo.

“Kwahiyo ukiacha simba wanaowindwa kwa vibali, wapo wanaokufa kutokana na tabia zao za asili, bado simba huyo huyo mzee anawindwa na wenye mifugo pindi wanapovamia maeneo ya vijiji na kwingineko. Tusipochukua hatua za makusudi, simba watakwisha Tanzania,” alisema Waziri Maghembe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles